Kuwa staa mechi moja, hakukufanyi ucheze Ulaya

24Feb 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuwa staa mechi moja, hakukufanyi ucheze Ulaya

WAKATI mwingine huwa nacheka, nikisoma baadhi ya makala za wachezaji wa Kitanzania wanapokuwa wanahojiwa baada ya kucheza vizuri kwenye mechi moja tu.

Wachezaji wa timu za mikoani, wakicheza na timu za Simba au Yanga na kuwa nyota wa mchezo wa siku hiyo, wakihojiwa utasikia wanasema kuwa malengo ni kwenda kucheza Ulaya.

Na hata baadhi ya wachezaji wa timu za Simba, Yanga na Azam nao siku wakionyesha kandanda la hali ya juu, nao wanasema kuwa malengo yao ni kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Halafu wachezaji wengine wanaosema hivyo ni wale ambao walishatoka nchini kwenda kucheza soka la kulipwa nchini za jirani tu, lakini wameshindwa na kurejea tena nchini Tanzania.

Wengine ukitazama hata umri wao ni kwamba hauruhusu kabisa wao kwenda kucheza soka huko, lakini bado wanadai wana ndoto za kucheza soka Ulaya tena baadhi wanakwenda mbali zaidi na kuzitaja timu kubwa barani Ulaya.
Wakati mwingine Wabongo wanaaminishwa ndoto za mchana.

Mtanzania Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anaichezea Aston Villa, yeye mwenyewe pamoja na kufika huko bado anajuta kwa nini hakutoka nchini mapema, kwani kwa umri wake wa miaka 27, anaonekana alichelewa kufika Ulaya.

Hapa Tanzania ukiangalia wachezaji wengi wana zaidi ya umri huo na hata wale ambao wana umri mdogo zaidi ya huo, walitakiwa tayari wawe wameshatoka kwenye ligi ya Tanzania, angalau wamesogela kwenye ligi kadhaa bora za Afrika, lakini bado wameendelea kung'ang'ana na ligi ya Tanzania na kutuaminisha kuwa wanataka kwenda kucheza Ulaya.

Wenzetu wana baadhi ya wachezaji wenye umri wa miaka 19 hadi 23, wanacheza Ligi Barani Ulaya tena kwa kiwango cha hali ya juu, kwenye timu kubwa ambapo kwa umri huo kwa Watanzania bado wanakuwa kwenye timu za vijana tu.

Kwa umri walionao wachezaji wanaocheza Ligi ya Tanzania walitakiwa wawe tayari wapo Ulaya wakizichezea klabu za Uturuki, Ubelgiji, Sweden, Denmark na nyingine.

Unashangaa kama kwa umri walionao bado wapo hapa, wanawezaje kutoka kufika ligi za Ulaya bila kupitia njia ngumu kama walizopita kina Samatta na Msuva?

Tusidanganyane, kwa sasa anaoweza kucheza Ulaya ni Nickson Kibabage na Kelvin John ambao bado wana umri mdogo na tayari wameshaondoka kwenye soka la Kibongo. Kingine cha kushangaza ni kwamba mchezaji wanayetamba kucheza Ulaya, anacheza vizuri mechi sita tu kwa msimu za kukamia, mechi zilizobaki anacheza kwenye kiwango cha kawaida sana, hapo huwezi kucheza hata soka la Afrika Kusini, achilia mbali Ulaya.

Kuna wachezaji wanaosubiri mechi za Simba, Yanga au Azam ndiyo aonyeshe ufundi wake, zingine anakuwa mchezaji wa kawaida sana.

Hakuna klabu yoyote Ulaya inayoweza kumchukua mchezaji ambao anaonyesha kujituma na kucheza soka safi kwenye baadhi ya mechi tu.

Kinachotakiwa mchezaji ni kuonyesha uwezo ulionao kwa msimu mzima, kwa sababu huwezi kujua kuwa kuna watu wanakufuatilia.

Tatizo lingine kubwa kwa wachezaji wa Kibongo ni kujitunza na kulinda kiwango. Hili linaoathiri hadi timu ya taifa, Taifa Stars. Mchezaji anachaguliwa akiwa kwenye kiwango kizuri, lakini baada ya mechi moja au mbili kiwango kinashuka.

Mchezaji hawezi kwenda Ulaya kama anashindwa kulinda kiwango chake na kujitunza mwenyewe bila ya kuwekwa kambini.
Ndiyo maana hata wachezaji wa kigeni wanawashindia wachezaji wa Kitanzania hapo tu.

Mchezaji wa kigeni anaweza akawa na kiwango cha kawaida kuliko Mbongo, lakini mgeni anaweza kukupa kiwango chake kile kile kila mechi, tofauti na Mbongo ambapo inakuwa maji kupwa na kujaa.

Nadhani kwanza wachezaji wa Kitanzania waliangalie hili kwanza kabla ya kutuambia kuwa wana ndoto za kucheza soka la kulipwa Ulaya.