Kuzembea elimu hii, ina maana kukikumbatia kipindupindu

06Jun 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuzembea elimu hii, ina maana kukikumbatia kipindupindu

WIKI hii kuna taarifa ya watu kukumbwa na ugonjwa kipindupindu jijini Dar es Salaam. Wameongezeka kutoka 34 mwishoni mwa Mei hadi 55, watatu wameshapoteza maisha.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alikaririwa akiwataka watu kutotiririsha majitaka mitaani.

 

Wataalamu wa afya wanasema ni miongoni mwa magonjwa  yanayosababishwa na aina ya bakteria aitwaye ‘Vibrio cholerae’ na anaweka wazi kwamba, ugonjwa ni wa kuambukizwa.

Njia kubwa ya uambukizaji ugonjwa huo, inatajwa na wataalamu ni viini vinavyoenezwa kupitia kwa kinyesi, kutoka kwa wagonjwa wenye kipindupindu kwenda kwa mtu mwingine.

Dalili za ugonjwa huo ni kuharisha sana hadi mwili unashindwa kujihimili, mgonjwa akiwa amedhoofika.

Namna nyingine ya afya, ni mgonjwa anajihsi kuwa na uchovu wa hali ya juu, anashindwa kutulia na ngozi ya nje na ndani zinajikunja, macho yanaingia ndani na anayeumwa anahisi kichefuchefu, kisha baadhi huangukia katika kiharusi.

Kimsingi, namna ya kuepuka kipindupindu ni kunawa mikono kwa sabuni, viganja, upande wa nyuma wa mkono, katikati ya vidole na kucha kwa sekunde baada ya kumaliza haja kubwa na kabla ya kula.

Vilevile, inaelekezwa kabla ya kutayarisha au kula chakula, kusafisha vyombo kama sahani, vikombe na vingine vingi mtu anashauriwa kunawa, kwa sababu ya kuepuka mlipuko wa maradhi.

Haijaishia hapo, jamii inatakiwa kuacha kutiririsha majitaka mitaani, kutumia vyoo safi na kuchemsha maji ya kunywa, lengo ni kuepuka ugonjwa huo. 

Cha kushangaza ni kwamba, baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, imekuwa ni jambo la kawaida watu kutiririsha majitaka mitaani, iwe kipindi cha mvua na hata wa kiangazi.

Elimu nyingine inayotolewa kwa jamii, tabia ya kufunika vyakula ,ili nzi wasiweke bakteria. Hapo tena, inasikitisha baadhi ya watu wasiozingatia na mwisho wa siku inaibuka maradhi ya kipindupindu.

Tufahamu kuwa mtu anapozembea elimu hiyo ni kuendelea kuhatarisha maisha au kuweka maisha rehani. Hivyo, ni muhimu jamii ikabadilika kuzingatia kile ambacho wataalam wa afya wanaelekeza.

Mtindo wa kuvizia mvua na kuelekezea uchafu wa vyooni kwenye mkondo wa maji ya mvua, ni jambo linalowaweka wakazi wa jiji, katika hatari kubwa ya magonjwa ya mlipuko.

Ninajua katika jamii wapo baadhi wasiotaka kunywa maji yaliyochemsha, wakidai hayakati kiu. Niwaambie kuwa, ni mazoea yanayowapoteza. Wanapaswa kuzingatia elimu inayotolewa na wataalam afya.

Kiafya, nikumbushe usafi ni adui mkubwa wa kipindupindu, hivyo jamii ikizingatiwa ni wazi ugonjwa huo utakoma, lakini kuendelea kukumbatia uchafu ni sawa na kuukaribisha.

Kwa sasa ni rasmi kipindupindu kipo jijini Dar es Salaam na tayari serikali imeshatoa onyo inayowataka wakazi wake kuzingatia kanuni za afya, ili kuepuka ugonjwa huo ambao chanzo chake ni uchafu.

Kipindupindu kitatoweka, iwapo kila mmoja atazingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya. Tatizo kubwa ni jamii kutokuwa makini.

Oktoba mwaka 2017, ulifanyika mkutano wa kumaliza ugonjwa wa kipindupindu ifikapo 2030, uliojumuisha maofisa kutoka nchi mbalimbali duniani na kufanyika nchini Ufaransa.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaeleza matumaini yake ya kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya kipundupindu duniani na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 90 ifikapo 2030, kwa vile ni aibu kuwa na ugonjwa katika karne hii.

Wakati juhudi hizo zikifanyika, jamii nayo iwe tayari kumkabili adui maradhi kwa kukubali elimu inayotolewa na wataalam wa afya, vinginevyo adui atakuwa anaondoka na kurudi kama ilivyodumu nchini.

Kuwapo kipindupindu katika karne ya 21, kunaelezwa ni 'aibu kubwa duniani.