Kwa nini Manula tu na si kocha wa makipa Simba?

26Oct 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kwa nini Manula tu na si kocha wa makipa Simba?

MARA baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Prisons Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa wakimtolea povu kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa kupoteza mechi hiyo.

Wanadai kuwa aina ya goli alilofungwa halistahili kwa kipa mkongwe na mzoefu kama yeye, tena akiwa ni namba moja kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, achilia mbali kwenye klabu hiyo.

Wanasimba wanaomlaumu Manula wanadai kuwa hawalalamiki kwa sababu wamefungwa, bali wanacholalamikia ni aina ya mabao ya kipa huyo anayofungwa kuwa ni yale yale na amekuwa hajirekebishi.

Simba imefungwa mbao matatu mpaka sasa kwenye mechi za Ligi Kuu, lakini wanadai mabao mawili ambayo mpaka sasa timu yao imefungwa ni uzembe wa Manula.

Ni hilo dhidi ya Prisons ambalo, Manula alitoka golini bila mahesabu, lakini alipogundua hawezi kuupata mpira alirudi tena nyuma, na tayari Samson Mbangula alikuwa ameshaenda hewani na kuupiga kichwa mpira uliokwenda wavuni goli likiwa tayari tupu.

Bao lingine ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ilipopata sare ya 1-1, aina ya goli alilofungwa pia hawakuridhika nalo. Ni kwamba Manula alitoka golini kwenda kuufuata mpira kwenye eneo ambalo hakutakiwa kwenda.

Badala ya kuelekea mbele ili aufikie mpira kabla ya mchezaji, yeye alienda eneo ambalo alikuwa anasubiria mchezaji aukose ili yeye ndio audake.

Haya yote, ukichanganya na baadhi ya makosa ya msimu uliopita, wakijumlisha mpaka yale ya Ligi ya Mabingwa Simba ilipokuwa ikipokea vipigo vya mabao 5-0 ugenini, vimewafanya wanachama na mashabiki wengi wawe na wasiwasi naye, huku timu hiyo ikiwa inakwenda tena kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika yeye akiwa ndiye kipa tegemeo.

Ni ukweli usiopingika Manula amekuwa na makosa mengi binafsi yanayoigharimu timu wakati mwingine. Ni makosa ambayo hayatakiwi kwa kipa mkubwa anayedakia timu kubwa kama ya Simba kuyafanya. Kipa huyo amekuwa dhaifu kwenye mashuti ya mbali, kona, faulo na krosi.

Imefikia hatua wanachama na mashabiki wa Simba timu yao inapopigiwa faulo au kona wanakuwa na wasiwasi. Hii si dalili nzuri kwake. Siku zote, makipa wa timu kubwa ni wale ambao wanaweza kuisaidia timu kwenye nyakati ngumu.

Mfano Simba ilipokuwa na kina Idd Pazi, Mohamed Mwameja au Juma Kaseja. Ni makipa ambao walikuwa na uwezo wa kuifanya timu ishinde kwenye mechi ambayo ilitakiwa itoke sare. Na waliifanya timu itoke sare kwenye mechi ambayo ilitakiwa ifungwe. Hizo ndizo sifa za kipa wa timu kubwa siku zote. Tatizo lingine ninaloliona ni kwamba Manula si jasiri golini. Halitawali goli na kuwafanya washambuliaji kutomhofia.

Wakati wanachama na mashabiki wa Simba wakimjia juu Manula, pamoja na mapungufu yake, lakini nina wasiwasi na Kocha wa Makipa wa Simba Mwarami Mohamed kama anafanya kazi yake sawasawa. Mapungufu mengi ya Manula yameanza kujitokea akiwa Simba, lakini hayakuwa mengi alivyokuwa Azam FC.

Kwa kuthibitisha hilo hata kipa namba mbili wa timu hiyo, Beno Kakolanya kabla hajajiunga na timu hiyo alikuwa kipa tegemeo wa klabu ya Yanga. Lakini alipojiunga na Simba kwa sasa uwezo wake umepungua na si kama ule aliokuwa nayo alikotoka.

Ukweli ni kwamba makipa wengi, wamekuwa wakishuka uwezo wanapojiunga na Simba tofauti na huko walikotoka. Hii inanipa wasiwasi juu ya mafunzo ya kocha wa makipa ambaye amekuwa akiona uwezo wa makipa wake mara kwa mara ukipungua badala ya kuimarika na hakuna chochote ambacho kimekuwa kikirekebishwa.

Imekuwa rahisi timu inapofanya vibaya lawama kumwangukia kocha mkuu katika klabu husika, hadi kufikia hatua ya kutimuliwa, lakini kipa anapofanya makosa ya kujirudia mara kwa mara na kuigharimu timu, husikii kocha wa makipa akitajwa!

Hivyo, baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba wameanza kushinikiza klabu kutafuta kipa mwingine kipindi cha dirisha dogo lakini husikii akitajwa kocha wa makipa! Huku wakitaka kuondolewa kwa Ally Salim ambaye ni kipa wa tatu, wengi wakimpendekeza Daniel Mgore wa Biashara United, lakini binafsi naona hata yeye kama akienda Simba anaweza pia kushuka kiwango kama benchi la ufundi halitoongezwa wataalamu au makocha wa makipa kwenye kikosi hicho.

Ikumbukwe kuwa kwenye Ligi ya Mabingwa timu nyingi hasa za Afrika Kaskazini maarufu kama za Waarabu, ni wazuri sana kwenye faulo, krosi na kona, hivyo kama kocha wa makipa na Manula hawatokuwa makini wanaweza kuwapa wakati mgumu wachezaji wengine wa Simba, wanachama na mashabiki wao.