Kwa Simba hii, kimataifa bado

27Jan 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kwa Simba hii, kimataifa bado

TUMEIONA timu ya Simba kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi na Kombe la FA siku ya Jumamosi ilipoichapa Mwadui mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Sven Vandenbroeck, ameonyesha kutoridhishwa na baadhi ya madhaifu yaliyopo kwenye kikosi chake, hasa kuruhusu magoli katika mechi kadhaa ambazo imecheza mpaka sasa, japo inashinda.

Lakini akasema kuwa kwenye mechi hiyo kipindi cha kwanza timu ilicheza taratibu sana, huku pia tatizo lingine ni kutotumiwa vema kwa nafasi ambazo zinatengenezwa.

Hii si mara ya kwanza kwa kocha huyo kulalamikia timu yake kutokuwa na kasi kwenye baadhi ya mechi zake.

Kwa jinsi Simba ilivyo haswa kwa mchezaji mmoja mmoja, ni hatari na tishio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, na hata Kombe la FA japo kuna wakati inapata ushindi kwa tabu.

Kuna uwezekano mkubwa kwa jinsi kikosi kilivyo kwa soka la Tanzania, ikawa bingwa na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, au Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa jinsi inavyocheza sasa zidhani kama Simba hii ina kikosi cha kufanya vema kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika, labda baada ya hapo yafanyike mabadiliko katika baadhi ya idara zenye mapungufu.

Vinginevyo, haiwezi kucheza hata na timu za Ethiopia, Comoro, Djibouti, Botswana au Eswatini ikawa na uhakika wa moja kwa moja kuibuka na ushindi.

Simba ina mapungufu mengi ambayo yanashindwa tu kuadhibiwa na timu za Tanzania ambazo zina hofu zikicheza nayo, badala yake zinakuwa zinatafuta sare tu, badala yake wachezaji wa timu pinzani wanafanya kazi kubwa ya kupoteza muda kuliko kucheza mpira.

Kama ikikutana na timu ambayo inataka hasa ushindi kwa Simba, na ikashambulia mfululizo, inakuwa kwenye matatizo makubwa muda wote.

Shida ya Simba inaanzia kwa mabeki hasa wa kati ambao inaonekana ni kama wamechoka na hawana kasi tena.

Mashambulizi ya kushtukiza ya wapinzani wanayofanya kwenye lango la Simba, yanaweka mabeki hao matatani na kushindwa la kufanya.

Pia mabeki hao hawamfuati adui ili kumsumbua na kutomruhusu kuliona goli na kupiga kwa uhuru, badala yake wote wamekuwa wakirudi nyuma na kumtazama adui nini atafanya, matokeo yake mashuti mengi yamekuwa yakipigwa langoni mwao kwa sababu ya kuwapa uhuru wapinzani wao kuchagua cha kufanya. Hapa ukikutana na wachezaji au timu yenye uwezo mkubwa umekwisha.

Viungo wakabaji wa timu hiyo wamekuwa hawafanyi kazi yao barabara na kuwaweka kwenye heka heka kubwa mabeki na kipa wao.

Viungo washambuliaji wa Simba, pamoja na uwezo wao mkubwa wa kupiga chenga, kuchezea mpira, lakini wamekuwa na tatizo la kupiga pasi za mwisho.

Ni kwa sababu hawazipigi kwenye muda sahihi, wanapenda sana kukaa na mpira bila sababu yoyote na hawana kasi.

Hata Simba inaposhambuliwa na kupokonywa mpira, viungo wa Simba wanashindwa kupiga pasi ndefu kwa ajili ya kufanya mashambulizi la kushtukiza, badala yake wanaanza pasi fupi na kuwafanya wapinzani wao kurejea nyuma haraka na kujipanga vizuri.

Kwenye nafasi ya ushambuliaji kwa sasa inaonekana ni butu kwa sababu inachezesha straika mmoja, Meddie Kagere ambaye kiasili ni mfungaji tu, lakini si mpambanaji na mwenye uwezo wa kuweka mpira miguuni, huku akiminyana na mabeki kama John Bocco.

Kwa maana hiyo Simba kama itapata nafasi ya kucheza kimataifa inahitaji mabeki wawili wa kati wenye uwezo mkubwa, viungo mkabaji mmoja kwenye viwango vya kimataifa, lakini mastraika wawili wa kuwasaidia waliopo, na kutowachezesha kwa pamoja viungo washambuliaji ambao hawana kasi.

Hapa inawezekana ikawa kwa asilimia kubwa imetibu tatizo linaloonekana wazi linaikumba kwa sasa.