Kwa wenzetu kulipa kodi ni sawa na kifo haiepukiki

20Sep 2020
Nkwazi Mhango
Nipashe
FIKRA MBADALA
Kwa wenzetu kulipa kodi ni sawa na kifo haiepukiki

BAADA ya Serikali ya Rais John Magufuli kubana matumizi na kuimarisha ukusanyaji kodi, huwa napata malalamiko ya baadhi ya marafiki zangu kuhusu kodi. Huwa nashangaa ikizingatiwa kuwa mazuri yote ambayo nchi yetu imeyafanya na kuyafikia haraka yangekuwa ndoto kama ukusanyaji kodi usingefanyika .

Hata hivyo, sishangai sana. Malalamiko hutokana na ukweli kuwa wengi hawakuwa wamezoea kulipa kodi vilivyo hima kutokana na mfumo wa kijamaa tulioanza nao au kutojua umuhimu wa kufanya hivyo kwa faida ya nchi na wananchi wake.

Sababu nyingine ni uzembe wa kuhimiza kukusanya kodi. Hapa Kanada, kulipa kodi ni sehemu ya ustaarabu na utaratibu wa kawaida. Si kulipa kodi tu bali hata kujaza taarifa za mwaka za kodi kwa kila mwananchi na mkazi ambaye si mwananchi wa hapa. Kulipa kodi hapa kunafanyika kwa njia ya kukatwa pesa moja kwa moja toka kwenye kila unachonunua. Ukiingia dukani, utakuta bei ya kila kitu imeandikwa. Kama maandishi yanasema bei ni kiasi fulani, ukikubali kulipa, utaongezewa kodi ya serikali. Hivyo, bei huongezeka tofauti na ile iliyoandikwa.

Kitu kingine, kila unapolipia manunuzi lazima upewe risiti tena siyo lazima uiombe. Hata usipopewa, kwa wale wasiotaka kudai baadhi ya fedha zirejeshwazo kwenye manunuzi yao, muuzaji huchapisha ile risiti na kuitupa kwenye jalala. Lazima ichapishwe kwenye mashine ya manunuzi ya kielektoniki (EFD).

Hapa kila kipato lazima kitozwe kodi bila kujali ukubwa hata udogo wake. Wanaofanya biashara ya kuuza miili yao, watoa simu za biashara hiyo, wanaocheza utupu, watengeneza matoi ya ngono, waendeshaji klabu za maonyesho ya utupu na waigizaji ngono, hawa wanatozwa kodi kama watu waliojiajiri.  Wanaouza miili yao hata kama anafanya hivyo kinyume cha sheria anapaswa kutoza kodi na kuhakikisha anatoa risiti ili mteja aamue mwenyewe (kwa wanaotaka kurejeshewa fedha za manunuzi au kutunza kumbukumbu).

David Rotfleisch wa kampuni ya Rotfleisch & Samulovitch P.C anasema kuwa anayeuza mwili huruhusiwa kudai baadhi ya marejesho ya kodi yatokanayo na maandilizi ya biashara kama vile matangazo, vitendea kazi na kadhalika.

Japo biashara hiyo haiwezi kuruhusiwa Bongo, kutokana na kukinzana na maadili yetu, hata ikiruhusiwa, wanaodai risiti watakuwa wachache au wasiwepo.

Wanaofanya biashara hiyo watapenda pesa yao isikatwe kodi. Wateja watagwaya kudai risiti. Maana, baadhi ya maduka huku huchukua taarifa za mteja kama vile anwani, nambari za simu hata baruapepe. Hivyo, wasingependa taarifa zao zijulikane.

Muhimu ni kuelewa: kulipa kodi ni wajibu si wa raia tu bali hata mkazi wa nchi yoyote. Kwa Tanzania ambapo wageni inakuwa vigumu kuwapata kama hakuna utaratibu wa kukata kodi moja kwa moja kwenye bidhaa na huduma anzisheni utaratibu wa kutoza kodi kwenye bidhaa badala ya kuhimiza watu binafsi walipe kodi.

Eneo jingine ambalo lazima mhusika alipe au kusamehewa kodi ni kuhusiana na kutoa huduma fulani kwa jamii au kutoa zawadi. Ukitoa huduma kwa jamii, serikali inakupunguzia kodi. Ila ukitoa zawadi au kununua kitu ambacho si muhimu au cha anasa kama sigara au pombe na magari na matoi ya bei mbaya, kodi huwa kubwa kweli kweli. Mfano hapa ninapoishi, kopo moja la bia yenye ujazo wa juu kidogo ya nusu lita inauzwa zaidi ya dola 3.5 za hapa ambazo ni sawa na takribani shilingi za Kitanzania 7,000 na ushei kutegemeana na kupanda na kushuka kwa shilingi yetu.

Kulipa kodi, licha ya kuwa wajibu wa mwananchi, hutuhakikishia huduma za pamoja toka serikalini. Unapolipa kodi, una haki ya kudai huduma za pamoja kama elimu, ulinzi, miundombinu na mengine kama hayo toka serikalini. Ndiyo maana Rais John Pombe Magufuli amekuwa akiwaambia Watanzania kuwa miradi mikubwa mikubwa aliyofanikisha, imefanikishwa na Watanzania wenyewe kupitia kodi zao. Hivyo, kwa mtu yeyote anayetaka maendeleo katika nchi yake, lazima alipe kodi bila kushurutishwa. Wamarekani wanao usemi kuwa vitu viwili haviepukiki kwa binadamu yaani kifo na kulipa kodi.