Lawama imekaa upande gani, Zimamoto na janga Kariakoo?

15Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lawama imekaa upande gani, Zimamoto na janga Kariakoo?

JESHI la Zimamoto na Uokoaji limekuwa likilalamikiwa na jamii kwa mambo mawili, mojawapo ni kwa kuchelewa kufika kwenye matukio na pia kutokuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kuzima moto.

Lawama hizo huwa zinasukumwa kwenye jeshi hilo, kutokana na kwamba, wakati mwingine sababu hizo ndizo zinazochangia baadhi ya majengo kuteketea bila askari wake kufika kwa wakati au wakiwa hawana maji.

Ni katika mazingira hayo, askari wa jeshi hilo waliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kwamba walinusurika kupigwa na wananchi wenye hasira mjini Shinyanga, baada ya kuchelewa kufika kwenye tukio la nyumba iliokuwa ikiungua moto huku watoto wakiwa ndani.

Yawezekana kuchelewa kufika kwenye matukio ya kuzima moto kukawa na sababu za msingi kama vile miundombinu ya barabara ambayo huchangia magari kukosa sehemu ya kupita.

Kwa mfano katika jiji la Dar es Salaam, barabara zake huwa zimejaa magari, lakini wakati mwingine maeneo ambayo kuna tukio la nyumba kuwaka moto halina barabara ya kupitisha magari.

Zipo sababu nyingine za kuchelewa kufika katika tukio, zinazoelezwa Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, John Masunga kwamba, ni kutopewa taarifa mapema kwa kuwa wananchi huanza kushughulikia tatizo wenyewe kabla ya kushindwa na kisha ndipo hupiga simu.

Katika mazingira ya aina hiyo, wakati mwingine inaweza kuwawia vigumu askari wa kikosi hicho kufika kwa wakati ili kutoa huduma na hivyo, kujikuta wakilaumiwa kwa sababu ambazo ziko juu ya uwezo wao.

Lakini pamoja na hayo, ni vyema jeshi hilo likawa na maji ya kutosha kwa ajili kuzimia moto. Ninadhani hilo liko ndani ya uwezo wao, kwa maana kwamba wanatakiwa kuhakikisha yanakuwapo muda wote.

Wiki iliyopita, Soko Kuu la Kariakoo, lililopo jijini Dar es Salaam, liliungua kwa moto, uliozuka kuanzia wastani wa saa 3.00 usiku, lakini kama ilivyozoeleka, lawama zilielekezwa kwa jeshi hilo.

Jeshi hilo lililalamikiwa kwa madai ya kutokuwapo maji ya kutosha kuzima moto huo kwa haraka, hali ambayo kama ina ukweli ndani yake, basi ingefaa kurekebishwa ili kuondokana na lawama za kila mara.

Hata hivyo, niliusikia uongozi ukitamka kuwa, tayari ukifafanua walakini katika vigezo vingine na si shida ya maji.

Pia Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, ameshatoa sababu ya kuchukua muda mrefu kudhibiti moto huo kuwa ni namna ya kutokuwa na sehemu sahihi za kuchukua maji ndani ya Kariakoo.

Ni hali iliyolazimisha wafuate eneo la Ukonga, palipo
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, wastani wa kilomita 10 kutoka penye tukio, huku moto ukiendelea kuteketeza mali za wafanyabiashara ndani ya maduka sokoni.

Daima, binadamu huwa wanajifunza kutokana na makosa, hivyo si vibaya makosa hayo ya kukosa maji jirani na Kariakoo, ikageuka kuwa funzo linalolenga mabadiliko chanya, kwa kutenga sehemu ya maji karibu na maeneo yote.

Hebu tufikirie jambo hilo kwa kina, kwamba kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Upanga hadi sokoni Kariakoo si mbali sana, wastani wa chini ya kilomita moja, askari wa Zimamoto na Ukoaji wanaenda mbali zaidi ya kilomita 10 kufuata maji ya kuzimia moto.

Jeshi hilo lina jukumu la kutoa huduma kwa jamii katika nyanja mbalimbali, zikiwamo kuokoa maisha ya watu na mali zao, kuzima moto, kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga moto.

Vilevile, Zimamoto na Uokoaji, hufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto, kusoma ramani za majengo na kutoa ushauri, huduma ya kwanza katika majanga na ajali barabarani, kutoa mafunzo ya kukabiliana na majanga moto, uchunguzi katika majanga ya moto na huduma za kibinadamu.  

Hivyo, zinapojitokeza kasoro kama za Kariakoo, ziwe fursa ya kufanya marekebisho, ili kuondoa lawama zisizo za lazima kutoka kwa watu, ambazo baadhi yao wanaamini kwamba jeshi hilo halifanyi kazi yake kikamilifu.

Inavyofahamika, magari ya zimamoto yanapofika kwenye tukio, hufanya kazi kama mtambo wa kuzimamoto kutokanana jinsio yalivyotengezwa yakiwa na matangi ya maji yenye ujazo kuanzia lita 1,500 hadi lita 7,000.

Ilivyo, katika ufafanuzi huo wa kitaalamu, ili maji hayo yatoke kwa nguvu na kuweza kuzima moto, kwa kawaida magari ya jeshi hilo huwa yamefungwa pampu zenye uwezo wa kusukuma lita 2,000 hadi lita 6,000 kwa dakika.

Hayo yakifanyika kama inavyotakiwa, hakutakuwapo lawama kwa jeshi hilo, lakini kwenye suala la kuchelewa kufika kwa wakati mwingine, inaweza kuwa nje ya uwezo wa jeshi husika.