Lawama za mashabiki zashangaza!

27Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lawama za mashabiki zashangaza!

“ASIYEKIRI ushinde hakuwa mshindani.” Mtu asiyekubali baada ya kushindwa si mshindani. Methali hii hutumiwa kuwanasihi binadamu kukubali wakishindwa au kuukiri udhaifu wao.

Jumamosi iliyopita Simba na Yanga (watani wa jadi) walipambana Uwanja wa Taifa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kama ilivyokuwa duru la kwanza, ni Yanga ndio waliotoka uwanjani vifua mbele baada ya kuwafunga Simba mabao 2-0 kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza.

Ushindi wa Yanga umepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa Simba kwa madai kuwa: Kwanza, Yanga walibebwa na pili, mwanamke hafai kuchezesha mechi za wanaume!

Wanaodai kuwa Yanga ilibebwa wanasema eti Abdi Banda hakustahili kuoneshwa kadi nyekundu iliyomfanya atolewe uwanjani. Simba walicheza pungufu kwa dakika 75 za mwisho. Hata hivyo walipambana kama Simba halisi wa mwituni kuhakikisha hawafungwi mabao mengi zaidi.

Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, alipohojiwa baada ya mechi alikubali kushindwa. Hakusema ‘walinyongwa’ na mwamuzi mwanamama, Jonesia Rukya Kabakama wa Kagera kama inavyodaiwa na mashabiki. Alisema kitendo cha Banda kutolewa kwa kadi nyekundu kiliwaathiri wachezaji kwa kuwa pengo lake lilionekana dhahiri. “Tunakubali kushindwa,” alisema.

Kwa nini mashabiki huwa wagumu kukiri timu zao zinaposhindwa? Je, ni kweli kwamba mwamuzi mwanamama hakutenda haki kumtoa n-nje ya uwanja Abdi Banda wa Simba?

Othman Kazi, mwamuzi mahiri wa kandanda anafafanua kati ya sheria 17 za soka zilizowekwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

“Sheria za soka ni 17 na kati ya hizo, idadi kubwa ya matukio ya uwanjani inabebwa na sheria mbili tu. Sheria namba 11 ya kuotea (offside) na sheria namba 12 ya mchezo m-baya na tabia mbaya. Katika sheria hizo mbili, mwamuzi anahusika zaidi katika sheria ya 12.”

Mwamuzi Kazi anasema Banda alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Donald Ngoma dakika ya 22 ya mchezo. Dakika tatu baadaye, Banda anamchezea tena Ngoma mchezo m-baya aliyekuwa anaelekea lango la Simba. Banda akaoneshwa kadi ya pili ya njano.

“Kosa la kumsukuma Ngoma akielekea lango la Simba, hakika lilistahili kadi ya njano. Kwa kuwa ilikuwa ni kadi ya pili, ilikuwa lazima Banda atolewe kwa kuoneshwa kadi nyekundu,” anasema mwamuzi Kazi.

Jambo lingine la kushangaza ni mashabiki wa Simba kusema mwamuzi wa kandanda la wanaume hafai kuwa mwanamke! Mbona wanakuwa wepesi wa kusahau? Ni huyu huyu Jonesia aliyechezecha mechi ya ‘Nani Mtani Jembe’ na Simba kuifunga Yanga 2-0.

Hawa wanaomponda sasa, ndio haohao waliomsifu mno katika mechi ile kuwa mwanamama huyo anachezesha kwa haki kuliko hata baadhi ya waamuzi wanaume!

Kuna mashabiki wa Simba wanaodai kuwa Banda na Hassan Kessy walipewa ‘chochote kitu!’ Eti alicheza mchezo m-baya mara tatu ndani ya dakika zisizozidi tano. “Kwa nini?” wanauliza. Aidha, Kessy alimrejeshea kipa wake mpira kwa ‘kumchuuza!’

‘Ulimi wa msingizia’ kama ilivyoandikwa kwenye Biblia Takatifu yasemwa: “Mlaani mchongezi aliye mnafiki, madhali amewaharibu wengi waliokaa kwa amani. Ulimi wa msingizia umewatikisa wengi, na kuwatawanyisha toka taifa hadi taifa; umebomoa miji yenye nguvu, na kuangamiza nyumba za watu mashuhuri” (Yoshua Bin Sira 28:13-14.)

Lengo la mchezaji yeyote ni kupata ushindi, hasa zinapopambana Simba na Yanga. Kwa kuwa wachezaji huahidiwa fedha ‘nzuri’ wakishinda, sidhani kama kuna atakayefanya ujinga wa ‘kununuliwa’ na timu pinzani. Vilevile ni katika michuano ya Simba na Yanga ndiyo huvuta ‘maskauti’ (wapelelezi) wanaotafuta wachezaji wa kuwauza nchi za n-nje. Kwa hiyo kila mchezaji hujitahidi kucheza kwa bidii na nidhamu ili waonekane.

Angalizo: Hali hii haiko kwa mashabiki wa Simba tu kwani hata wa Yanga ndivyo walivyo. Hawapaswi kuchekana kwa sababu leo likiwa huku kesho litahamia kwingine … ni muda tu.

Kandanda ni mchezo wa bahati na makosa. Tukijua hivyo, hatuna sababu ya kutoa visingizo visivyokuwa na msingi. Kuna kushinda na kushindwa na ndo maana ya mashindano yoyote. Wasalam.

[email protected]
0715/0784 33 40 96