Lazima tukiri hatua ya kuthubutu kwa nchi yetu

07Dec 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lazima tukiri hatua ya kuthubutu kwa nchi yetu

MIAKA 57 imetimia tangu nchi hii ipate uhuru Desemba 9 mwaka 1961, ikiwa imepita hatua mbalimbali za maendeleo, tofauti na miaka ya nyuma kabla na miaka michache baada ya kupata uhuru.

Vipo vitu vinavyoonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua za kimaendeleo, ikiwamo elimu na vingine vingi, ambavyo Watanzania wanapaswa kujivunia.

Lakini, nitajikita zaidi katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ambayo kwa kiasi kikubwa imeufanya usafiri kuwa rahisi, tofauti na miaka ya nyuma.

Miaka ya nyuma Watanzania walikuwa wakitumia siku nyingi kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, lakini hilo leo halipo tena.

Ninasema halipo, kwa sababu karibu mikoa yote imeungwanishwa kwa mtandao wa barabara za lami, hivyo yawe masika au kiangazi, bado watu wanaweza kusafiri bila kukwama njiani.

Siyo abiria tu bali hata wasafirishaji wa mizigo nao wamepata unafuu katika hilo ingawa bado kuna maeneo machache ambayo bado hayajaunganishwa na mtandao wa barabara za lami, lakini kwa kiasi kikubwa mambo ni mazuri.

Wakati Watanzania wanaadhimisha miaka 57 ya uhuru wa nchi yao, hawana budi kujivunia mambo mbalimbali ya maendeleo likiwamo hilo la nchi kuunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami.

Hata serikali ya awamu ya tano imekuwa ikikazania sana uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini, ili kurahisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka sehemu kwenda nyingine.

Kwa mfano jijini Dar es Salaam barabara mbalimbali zikimekuwa zikijengwa kwa kiwango cha lami ikiwamo pia upanuzi wa barabara ya Morogoro unaoendelea sana lengo likiwa ni kurahisha usafiri.

Barabara zinapoboreshwa zinasaidia pia kurahakisha shughuli za maendeleo, kwa kuwa inakuwa ni rahisi watu kusafiri na kufika haraka katika biashara au ofisi kwa ajili ya taifa.

Vilevile uboreshaji huo unasaidia katika usafirishaji wa mizigo yakiwamo mazao ya wakulima na kuyafikisha kwa wakati kule yanakopelekwa.

Leo hii, mtu anaweza kusafiri kutoka Mwanza hadi Dar es Saalama akafika siku hiyo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo abiria walikuwa wanakaa njiani kwa siku nyingi kutokana na ubovu wa barabara, hasa kutokuwa na lami.

Miaka ya nyuma abiria wa kwenda mikoa ya kusini walikuwa wakitoka Dar es Salaam na kukwama eneo ambalo sasa linajulikana kama Daraja la Mkapa, kwa kuwa hakukuwa na daraja kwenye Mto Rufiji.

Lakini sasa, eneo hilo limejengwa daraja kubwa linalofaa kuwa la utalii, abiria sasa wanaokwenda mikoa ya Lindi na Mtwara hawalali tena njiani na pia yapo magari ya abiria yanayokwenda Lindi na kurudi Dar es Salaam siku hiyo hiyo.

Nimetaja maeneo hayo kadhaa, lakini kwa ujumla mikoa yote imeunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami, hii inaonyesha ni jinsi gani nchi imepiga hatua na inaendelea kupiga hatua za maendeleo.

Inawezekana wapo baadhi ya watu ambao hawalioni hilo, lakini ukweli unabaki palepale kwamba upande wa miundombinu ya barabara, nchi inakwenda vizuri na hatua ya kujivunia.

Ninatambua kwamba yapo baadhi ya maeneo ambayo bado yana changamoto, katika maendeleo ya nchi, lakini kwa hili la barabara, kila Mtanzania hana budi kujivunia.

Abiria wanasafiri na kufika kwa wakati, wanaosafirisha bidhaa nazo zinafikishwa kwa wakati, kutokana na ubora wa miundombinu ya barabara, ambayo kabla na miaka michache baada ya huru ilikuwa duni.

Kwa ujumla ninaweza kusema, kwa miundombinu ya barabara, Tanzania imethubutu, imeweza na sasa inazidi kusonga mbele katika kujiletea maendeleo ikiwa ni miongoni wa nchi changa.