Lifti malori kwa wanafunzi, tahadhari ni jambo muhimu

12Mar 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lifti malori kwa wanafunzi, tahadhari ni jambo muhimu

KUMEKUWAPO na tabia kongwe na inayoendelea kujengeka kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupanda malori yanayosafirisha mchanga, wakati wanafunzi hao wanaenda na kurudi shule.

Tunatamka hayo, huku tukijua kwamba suala la usafi kwa baadhi ya maeneo, imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi, inapotokea wanapoamka asubuhi kwa safari ya kwenda shule na kuagana wanapomaliza masomo, shida kubwa kwao ni namna ya kufika wanakoelekea.

Mjumuiko wa fikra hizo zote, ndizo zinazozaa mustakabali kamili wa changamoto mbele yao wanafunzi. Kwa vipi? Mambo huanza pale wako katika sare rasmi na wanaomba lifti kwa baadhi ya magari ama wanapoenda au kutoka shule.

Ni kwamba, pale wanapotaka kupanda magari ya abiria kuelekea nyumbani au shule, baadhi ya magari hayo yanawakataa.

Hayo yanajitokeza, huku kwa baadhi ya wanafunzi shule zao ziko mbali zaidi na kuna changamoto ya kuwa mbali sana, hali inayosababisha usumbufu kwa wanafunzi.

Changamoto nyingine kwa watoto hao ni miundombinu yao kutokuwa mizuri, kunachangia wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule na kurejea kwao. Hiyo, inatokana na maeneo hayo ya usafiri kutokuwapo wa uhakika.

Katika baadhi ya maeneo, wapo wazazi wanaotambua adha hiyo ya umbali kwa watoto wao hadi shule, baadhi ya wazazi wamewanunulia baiskeli wanafunzi, wazitumie kwenda shule na kurudi nyumbani.

Nianze kwa kuwashukuru hao wenye malori au magari ya kubeba mazao mashambani, kwa kuona changamoto ambazo zinawakuta wanafunzi na kuamua kuwabeba kwa safari zao za kimasomo.

Pamoja na wema huo wa kuwabeba wanafunzi, tunapaswa kwanza kijiuliza, je, usalama wao unakuwa unaangaliwa na nani wakati gari zinapokuwa zinaondoka?

Ni kawaida kuwakuta wanafunzi wamepanda malori nyuma na hakuna watu wa kuwaangalia. Wanafunzi hao wanarukaruka wakati gari linatembea. Je, ikitokea anaanguka chini na kudhurika, atalaumiwa nani?

Watoto wana hulka ya kutotulia, kwa sababu hawana mtu wa kuwasimamia, gari linatembea wanafunzi wanaendelea na michezo ya kuruka huku gari linaendelea na safari.

Tena, unakuta gari hizo zinachukua wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Hapo inajenga swali lingine, nini kinachotakiwa kuangalia usalama wa watoto hawa?

Mara nyingi wanahitaji uangalizi muda wote na hata ikiangaliwa na wanaotumia usafiri wa shule, kuna watu maalumu wa waandaliwa kuwasimamia, mpaka wanapofika kwao.

Katika haya malori au gari, inawezekana wanafunzi wa sekondari wakawa wanajitambua, lakini hao wa shule ya msingi uelewa wa kufikia kujitambua kikamilifu, bado ni mdogo.

Kinachotakiwa ni kuwaangalia, maana chochote kikitokea, lawama mtazibeba nyie wenye magari hata kama mkijitolea kuwasaidia usafiri.

Niseme kwenu waendesha magari, mnapoyasimamisha, mhakikishe kuna mtu nyuma ambaye anawaangalia watoto ili wasije wakaanguka barabarani wakapoteza maisha.

Tunashukuru msaada ambao mnautoa kwa wanafunzi kwa kuwapatia lifti, lakini msaada huo baadaye unaweza kugeuka kesi mbaya.