Lililotokea Uwanja wa Sokoine liwe funzo

30Dec 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lililotokea Uwanja wa Sokoine liwe funzo

GUMZO kubwa lililowaacha watu hoi wiki iliyopita ni Uwanja wa Sokoine Mbeya kutumiwa kwenye tamasha la muziki, kiasi cha kushindwa kuchezwa kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Prisons dhidi ya Yanga.

Kutokana na uharibifu huo, mechi hiyo ilihamishiwa kwenye Uwanja wa CCM Samora mjini Iringa na Yanga iliondoka na pointi tatu baada ya kushinda bao 1-0.

Picha zilizopigwa baada ya tamasha hilo zilionyesha uwanja umeharibika kiasi cha kuwasikitisha wadau wa soka.

Hakukuwa na nyasi zaidi kuonekana kama bonde au jangwa. Meneja wa uwanja naye alipoulizwa, majibu yake yalionyesha kuwa na yeye kukerekwa na jambo hilo, lakini akionekana kama vile hakushirikishwa.

Cha kujiuliza ni nani aliyeruhusu tamasha la muziki, tena la bure kufanyika kwenye uwanja huo ambayo ulitengenezwa sehemu ya kuchezea 'pitch' miaka michache iliyopita na kuwa moja ya viwanja vizuri nchini?

Inawezekana labda waandaaji wa tamasha walilipa pesa. Lakini thamani ya kuutengeneza uwanja huo unaweza kuwa chini kuliko gharama za malipo ya tamasha hilo? Hili mimi siamini.

Tayari Bodi ya Ligi imeufungia uwanja huo. Nimewaelewa Bodi ya Ligi. Si kwamba wameusimamisha mpaka pale utakapokuwa umetengenezwa, la hasha.

Ni kwamba imeufungia kabisa na hata ukishatengenezwa na kuwa tayari kuchezeka, itabidi uongozi na wamilikiwa wa uwanja mkoani Mbeya waandike barua ya kuomba radhi kwa kilichotokea kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ili kuomba ufunguliwe na kutumika kwa michezo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, alikaririwa akisema kuwa anasikitika kwa tukio hilo ambalo linaonekana kama uongozi wa uwanja umeonyesha dharau kwani ulitambua kabisa kuwa kesho yake kulikuwa na mechi, lakini ukaruhusu tamasha la muziki ambalo liliruhusu watu kuingia uwanjani, wakikanyaga nyasi na kucheza, kiasi cha kutoacha hata nyasi moja, lilipomalizika.

Mguto alisema kuwa inaonyesha kuwa uongozi haukuona umuhimu wa mechi hiyo zaidi ya umuhimu wa tamasha kwa sababu ratiba ya mechi hiyo ilifahamika tangu zamani, hivyo akasema wanaufungia hadi viongozi waone umuhimu wa uwanja huo kuchezewa mechi za Ligi Kuu.

Binafsi ninaipongeza Bodi ya Ligi kwa kuufungia uwanja huo na nadhani hii itakuwa ni fundisho kwa viwanja vingine.

Ni kweli inawezekana viwanja vingi mikoani havipati pesa nyingi kwenye mechi za mpira wa miguu, labda zikicheza Simba na Yanga, lakini pamoja na hayo haiondoi ukweli kuwa hivyo ni viwanja vya soka na si kumbi za burudani, ndiyo maana vina magoli.

Matamasha kama haya yalitakiwa yapelekwe kwenye viwanja vya wazi, lakini nadhani viongozi wa viwanja hivi huamua kuchukua pesa za matamasha kwa sababu zinakuwa nyingi kuliko zile za mechi ya mpira, lakini madhara yake ndiyo haya, unapotokea uharibifu hasara inakuwa kubwa kuliko kilichoingia.

Ukiachilia mbali Uwanja wa Sokoine hautopata tena mapato yatokanayo na soka, labda uongozi uendelee sasa kukodisha matamasha, lakini mashabiki wa Mbeya watakosa mechi mbalimbali za Ligi Kuu kwenye uwanja huo, nadhani hata na baadhi ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza.

Kuna wafanyabiashara ndogo ndogo ambao walikuwa wakiuza jezi, vyakula, vinywaji, na hata wale wa usafiri kama bodaboda, bajaji na mabasi madogo wakati timu za mikoani zikifika Mbeya, lakini kwa sasa hawatoweza tena kufanya hivyo na haijulikani tena hali itatengemaa lini.

Timu za Mbeya City na Prisons na mashabiki wao itabidi waingie gharama zisizo za lazima za kwenda kucheza mechi nje ya mkoa huo kwa uzembe wa watu wachache tu.

Sina uhakika kama ratiba ya ligi nayo itakwenda sawa sawa, kwani Uwanja wa Samora pia hutumiwa na Lipuli, hivyo timu zingine mbili kwenda kutumia uwanja huo huo ni lazima kuwe na marekebisho ya ratiba pia.

Wakati wakazi wa Mbeya wakiteseka kwa kutopata burudani ya soka licha ya kuwa na timu mbili za Ligi Kuu, hili liwe fundisho kwa viongozi wa viwanja vingine nchini Tanzania kutokubali kuruhusu kuharibika kutokana na kutumika kwa mambo mengine ambayo yako nje ya kusudio la kujengwa kwa viwanja hivyo ambavyo kiasili vimetengenezwa kwa ajili ya kuchezwa soka tu.