Lipuli ina cha kujifunza kutoka kwa Watford

20May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lipuli ina cha kujifunza kutoka kwa Watford

JUMAMOSI iliyopita dunia ilishuhudia fainali ya Kombe la FA nchini England, wakati Manchester City ikiisulubu bila huruma Watford kwa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Wembley.

Ni mechi ambayo iliwaacha hoi watu waliokuwa wanaitazama, maana ilifika wakati ikaonekana kana kwamba Man City inacheza mazoezi na si mechi ya fainali.

 

Kwenye vibanda umiza nako hakuishiwi maneno, watu wakaanza kuulizana timu ile iliingiaje kwenye fainali, hali ya kuwa imeonekana ni dhaifu sana. Wengine wakazikumbuka timu kadhaa za England ambazo tayari zimeshatolewa kuwa kama zingetinga fainali basi zingeipa kazi sana Man City.

Wengine wakasema Watford ilipata bahati ya kutokutana na timu ngumu, lakini baadhi wakapinga na kusema England timu zote ni ngumu, ila ilikuwa ikikomaa na kuzikamia baadhi ya timu na kufika hapo ilipofika.

Vyovyote itakavyokuwa, lakini ni fainali iliyoboa, ambayo wengi hawakuitarajia kuwa itaisha kama ilivyoisha. Ni kweli England kwa sasa Man City ni timu ya kuogopesha ukikutana nayo, lakini kwa hali ilivyokuwa ilisikitisha. Man City, ilicheza inavyotaka. Ikatawala mpira ilivyotaka, wachezaji wakacheza wanavyojisikia, wakafunga mabao wanavyotaka, huku Watford wakionekana kukimbikiakimbia tu kama swala wanaokimbia mwituni wakisalimisha maisha yao yaliyokuwa hatarini dhidi ya mnyama Simba.

Nikaanza kuwaza fainali ya Kombe la FA la Tanzania ambayo inatarajiwa kupigwa Juni Mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi kati ya Azam na Lipuli.

Wengi wanauchukulia kama utakuwa ni mchezo mgumu kutokana na njia ngumu aliyopitia Lipuli hadi kufikia fainali.

Moja kati ya njia ngumu ni kukutana na Yanga ambayo tayari uelekeo wake wa ubingwa wa Tanzania Bara ulikuwa tayari umeshapotea, hivyo njia pekee iliyobaki kwao ni kutwaa Kombe la FA kwa ajili ya kucheza Kombe la Shirikisho  msimu ujao.

Hilo halikufanyika kwani Lipuli, kwa namna ambayo haikutegemewa na wengi iliichapa Yanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora na kuzima ndoto zao, huku yenyewe ikiweka rekodi ya kutinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo.

Lakini wakati kila mmoja anauchukulia kuwa utakuwa mchezo mgumu, Lipuli ikifanya masihara inaweza ikajikuta ikiwa kama Watford na fainali ikawa nyepesi kwa Azam.

Ni kwamba wachezaji wa timu hizi huwa wanacheza kwa bidii na juhudi kubwa wakicheza na klabu zenye wachezaji wenye majina makubwa na mashabiki wengi, lakini zinapokwenda kucheza na klabu zingine viwango vyao vinabadilika kabisa. Wachezaji wengi wa Kitanzania hawaichukulii Azam kama ni klabu yenye uwezo mkubwa na viwango vya hali ya juu kama ilivyo Simba au Yanga, badala yake huichukulia poa tu kwa sababu tu haina mashabiki wengi. Hicho ndicho kinaweza kuigharimu kabisa Lipuli. Makocha wa Lipuli wakiongozwa na Selemani Matola wanapaswa wawe makini na wachezaji wao si kwenye ufundi tu, bali kuwatia morali na kuifanya mechi hiyo kuwa kali ya kusisimua kama inavyotarajiwa kuwa. Vinginevyo tunaweza kushuhudia fainali kama ile ya England ikawa rahisi mno kwa Azam na baadhi wakaanza kujiuliza Lipuli ilifikaje fainali.

Ikumbukwe kuwa Azam kwa muda sasa haijawakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na haina nafasi yoyote kwenye ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo bahati kama hii ya kufika fainali haiwezi kuja mara mbili, hivyo watakwenda wakiwa wamejizatiti ili kurudisha heshima yao, hivyo Lipuli inabidi iende kwa tahadhari na isije kukipata kichapo kama kilichomtokea kwa Watford.