Lugha ya Kiswahili ipewe hadhi inayostahili

10May 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lugha ya Kiswahili ipewe hadhi inayostahili

LUGHA ya Kiswahili inakua kwa kasi na kutambuliwa katika sehemu nyingi za dunia.Inafundishwa, kuzungumzwa na kuandikwa katika vyuo mbalimbali vikiwemo vyuo vikuu vya mataifa makubwa yaliyoendelea.

Kwa miaka zaidi ya 50 nchini Tanzania tangu uhuru, lugha hiyo imeendelea kukubalika kikamilifu kwamba ni lugha rasmi ya mawasiliano.

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Taifa(Unesco) zinaonyesha kuwa, Kiswahili, kinazungumzwa na watu wapatao milioni 180 duniani kote.

Mwaka 1986, Unesco ilipitisha azimio kwamba, Kiswahili kitumike kwenye vikao vyake vyote.Hata katika Umoja wa Afrika(AU), lugha hii ni rasmi kwa ajili ya mawasiliano wazungumzaji wanaweza kuitumia kutoa hotuba au kuchangia mijadala mbalimbali.

Kiswahili huzungumzwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki, Kusini na Kati pamoja na visiwa vilivyo karibu na Tanzania na kwingineko.

Nenda katika nchi kama za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati na Zambia, Afrika Kusini lugha hii inazungumzwa na inafahamika na wenyeji wa maeneo hayo.

Nchi nyingine ni katika Visiwa vya Ngazija(Komoro), Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe Kiswahili kinazungumzwa.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusaidia kukuza na kueneza kwa lugha hii, ni kutokana na taasisi za elimu katika shughuli za kiuchumi kupitia wafanyabiashara, watalii wanaofika nchini pamoja na shughuli zingine kuitumia lugha hii.

Katika shule kuanzia ngazi ya awali yaani shule ya msingi hadi vyuo vikuu, kumekuwa na ufundishwaji kwa kutumia lugha hii, ikiwamo kozi maalum mbalimbali .

Muingiliano wa lugha hii kupitia wafanyabiashara wanaoingia na kutoka nchini ili kufuata bidhaa tofauti pamoja na watalii ni sababu nyingine inayochangia kukua kwa lugha hii.

Lugha hii imeendelea kusambaa kwa kasi zaidi duniani kupitia vyombo vya habari vya nchi tofauti hususan idhaa za kimataifa.

Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi wakati fulani alitoa wito kwa wanazuoni nchini, kuendelea kukuza lugha hii kwa kuandika vitabu kwa lugha ya Kiswahili ikiwa ni fursa pekee inayoweza kutumika kuiendeleza lugha hiyo kupitia taaluma zao.

Kupitia uandishi anauita kuwa ni fahari kwa nchi ya Tanzania hasa kwa wazuoni wazalendo kupitia taaluma zao, kuandika vitabu kwa kutumia lugha adhimu ya Kiswahili, kuelezea taaluma katika maandishi kwa manufaa ya Taifa ni muhimu.

Kwa hakika lugha ya Kiswahili inahitaji kuendelezwa na wanazuoni, pamoja na Watanzania kwa ujumla ili kuikuza kupitia sanaa, elimu hata michezo.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba,lugha hii ni muhimu sana duniani kwa sasa na kama watanzania tutachukua hatua za makusudi za kuhakikisha kuwa tunachangamkia kuendeleza lugha hii tutakuwa tunafanya jambo la maana sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya lugha hii.

Kila mtu kwa nafasi yake ni kwamba anatakiwa afanye kila awezalo katika kuchangia maendeleo ya lugha hii kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.