Lugha za waandishi zachusha

11Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Lugha za waandishi zachusha

‘CHUSHA’ maana yake ni chukiza; udhi, chosha. Pia ni kiumbe kisichopendeza kwa watu kutokana na vitendo vyake; kirihisha. Kuna maana ingine pia lakini siitumii kwani yaweza kuniletea uhasama (hali ya kufarikiana nao) kwa kukosoa Kiswahili chao.

Ilivyo ni kama Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limerithiwa na waandishi wa magazeti wanaoonekana kuanzisha lugha yao na kuwakanganya (duwaza mtu asijue la kufanya, fanya mtu achanganyikiwe) wasomaji. Maneno halisi yameachwa na kutumiwa ya mitaani au kuzusha (anzisha kitu kipya ghafla; anzisha na sambaza taarifa za uzushi) ‘mapya’ kama watakavyo.

Kila lugha ina maandishi na matamshi yake. Lugha inapokosewa kuandikwa, huweza kumtatanisha msomaji kutoelewa maana iliyokusudiwa au kuleta maana tofauti. Kwa mfano, ‘gamu’ ni neno tofauti kabisa na ‘ghamu’ kwani maana ya ‘gamu’ ni uzito wa kufanya jambo kutokana na hisia ya woga au hofu wakati ‘ghamu’ ni majonzi.

Lugha ina maneno yasiyokuwa na wingi kama maji, mate, taa, siku n.k. Kwa sababu hiyo wingi wa ‘maji’ ni maji badala ya ‘mamaji’ au ‘mimaji.’ Pia ‘mate’ yawe kidogo au mengi hubaki kuwa mate tu. ‘Taa’ moja husemwa ‘taa hii’ na nyingi huitwa ‘taa hizi.’ Kusema ‘mataa’ si Kiswahili. Kadhalika ‘siku moja’ yaitwa ‘siku hii’ na zaidi ya moja husemwa ‘siku hizi.’ Hakuna ‘masiku’ kama isemwavyo mitaani.

Kwa utaratibu huo, wingi wa ‘kitu’ ni ‘vitu’ na si ‘mavitu’ au ‘mavituz’ kama iandikwavyo kwenye magazeti ya michezo, tena kwa upotoshwaji mkubwa. Kwa hakika neno ‘kitu’ lina maana nne: i) jambo; ii) mali au fedha; iii) mnyama mweusi wa jamii ya paka na iv) ni chochote ambacho si mtu au mnyama.

Sasa soma lugha ‘mpya’ ya waandishi wa magazeti ya michezo: “Zahera aleta Yanga SC mavitu ya AFCON.” Vitu ni wingi wa ‘kitu’ kama nilivyoeleza hapo juu. Waandishi wa michezo hupenda sana kutumia neno ‘mavitu’ kwa maana ya wacheza kandanda mahiri, kumbe ni sitiari (matumizi ya neno kwa maana isiyokuwa ile ya msingi).

“Simba mpya kujifua Uturuki.” Neno ‘jifua’ hutumiwa sana na magazeti ya michezo, tofauti na maana yake halisi. ‘Fua’ ni neno lenye maana sita; i) rangi ya kahawia inayopatikana kwenye mizizi ya miti inayotumika kupikia kili (wingi wa ukili); utepe mpana uliosukwa kwa chane za ukindu, muwaa au kiwanda.

‘Fua’ ii) kutengeneza vyombo au mapambo kwa kutumia madini; iii) kuondosha makumbi kwenye nazi kwa kifulio; iv) kutoa taka kwenye nguo kwa maji na sabuni; v) kumfanyia mtu dawa ili kuondoa nuhusi/nuksi na vi) kutoa taka kutoka kwenye kisima.

Haieleweki wacheza kandanda hujifuaje kama nguo! Au huenda ughaibuni kutengeneza vyombo vya mapambo au kuondosha makumbi kwenye nazi kwa kifulio au kufua madafu? Kutoa taka kwenye nguo kwa maji na sabuni? Kuwafanyia watu dawa ili kuwaondolea nuhusi au kutoa taka kwenye visima!?

Sasa waandishi washindwa hata kuandika mtiririko mzuri wa sentensi zao! “Kama ulidhani Simba pekee yake ndiyo itawakilisha Bara Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, basi maamuzi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huenda yakakushutua.”

Si ‘shutua’ ni shitua. Maneno ‘pekee yake’ hayaendani pamoja. Maana ya ‘pekee’ ni bila –ingine, peke yake; pweke. ‘Peke’ ni bila mwenzi, -enyewe tu; bila kuwepo –engine. Neno ‘yake’ lina maana mbili: i) kivumishi kimilikishi cha nafsi ya tatu umoja; ii) kiwakilishi kimilikishi cha nafsi ya tatu umoja.

Kwa hiyo mwandishi hakuwa sahihi kuandika: “Kama ulidhani ni Simba pekee yake ndiyo itaiwakilisha Bara Ligi ya Mabingwa … basi uamuzi wa …” (Nimetumia neno sahihi ‘uamuzi’ badala ya maamuzi.) Badala yake angeandika” “Kama ulidhani ni Simba pekee …” au “Kama ulidhani ni Simba tu ndiyo itakayoiwakilisha Bara …”

“Juzi kati kwa pamoja jamaa walisema kwa upande wao wachezaji kuumwa ugonjwa unaotisha hivi sasa (Dengue) kuwa wanapenda sana kuvaa vipensi ndiyo sababu kubwa ya kuumwa na mbu huyo anayeuma mchana.” Hii ni taarifa ya mwandishi wa michezo alipowahoji wachezaji Ndemla na Ajib kuhusu ugonjwa wa Dengue.

‘Juzi’ ni siku moja iliyopita kabla ya jana. Nielewavyo ni kuwa kuna ‘juzi asubuhi,’ ‘juzi mchana,’ ‘juzi jioni’ na ‘juzi usiku.’ Hili la ‘juzi kati’ silielewi ingawa latumiwa sana na waandishi.

“Manara aingia chaka Taifa” ni kichwa cha habari kwenye gazeti la michezo kilichofuatiwa na habari: “Umewahi kuona mtu akipotea kwao? Ndivyo ilivyomtokea Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba Hajji Manara alipoingia Uwanja wa Taifa na moja kwa moja kwenda katika jukwaa la mashabiki wa Simba na kukutana na mashabiki wa Yanga, huku wale wa Simba wakikaa upande wa Yanga.”

Uwanja wa Taifa hauna msitu wenye msongamano wa miti. ‘Chaka’ ni neno lenye maana mbili, tofauti na lilivyotumiwa na mwandishi. Maana ya kwanza ya ‘chaka’ ni sehemu ya msitu yenye msongamano wa miti na mimea; mahali penye mkusanyiko wa majani na miti mingi iliyosongamana. Kuna methali isemayo ‘chaka la simba halali nguruwe.’ Pia ni majira ya jua kali na joto; kipindi baina ya Desemba hadi Februari; kaskazi.

Mwandishi pia katumia neno ‘vipensi’ linalonitia bumbuazi (mshangao mkubwa unaomfanya mtu awe kimya na asijue la kufanya). Kwani aliona wasomaji wasingeelewa kama angeandika ‘nguo fupi’ badala ya ‘vipensi’?

Methali: Tamu ikizidi tamu huwa si tamu tena.

[email protected]

0784 334 096