Lukuvi ameacha alama isiyofutika

09Jun 2020
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Lukuvi ameacha alama isiyofutika

UPO usemi kuwa mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, hili halina ubishi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi. Ni miongoni mwa viongozi ambao wamepewa eneo na wamelisimamia kwa weledi.

Kila ukifungua mitandao ya kijamii na hasa Utube unakutana na video za Lukuvi akieleza mambo mbalimbali ya ardhi ambayo yanagusa maisha ya watu na hasa waliopora haki zao na wenye nguvu ya fedha na mamlaka.

Kwenye eneo la ardhi dhuluma, uonevu na mengine mabaya yalitawala kiasi cha watu kudai haki zao mahakamani na njia nyingine kwa miaka mingi bila mafanikio.

Dhuluma mojawapo ni kula njama baina ya madalali na taasisi za mikopo au watu binafsi ambao hukimbilia kuuza mali za watu hasa ardhi na kubadilisha umiliki kwa haraka bila kujali kuwa wanawaachia maumivu makali walioporwa mali zao.

Mathalani, kuna wakati vyombo vya habari vilitawaliwa na habari za mtu mmoja aliyeporwa haki yake kwa kuchukua ghorofa lake na rafiki yake ambaye alishirikiana na watumishi wa idara ya ardhi kutengeneza hati feki.

Kama siyo Waziri Lukuvi ambaye ameamua kusaidia wahitaji, mhusika huyo huenda asingerejeshewa mali yake hiyo.

Nyingine ni mkoani Arusha ambako kuna taarifa za mama mzee kunyang’anywa mali yake na kwa zaidi ya miaka 30. Alidai mahakamani bila kufanikiwa, lakini Waziri Lukuvi, amempa bibi huyo mali yake.

Huenda ardhi ni moja ya maeneo yenye ugumu na lililojaa wajanja wenye kushirikiana na madalali ambao miaka mingi wanakula kwa jasho la wengine kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa Idara ya Ardhi.

Yote haya ni uonevu dhidi ya wananchi ambao wanakesha kwenye mabaraza ya ardhi kusaka haki yao kwa gharama kubwa, lakini wasiipate kutokana na ukweli kuwa waliopo kwenye mfumo wanashirikiana na wanaowanyanyasa raia.

Kwenye miji na majiji kuna kesi nyingi za watu kuporwa ardhi zao, wamiliki wawili kuwa na hati, na wengine kujeruhiwa au kufanyiwa ubaya licha ya kuwa ni haki yao.

Tangu kuingia madarakani kwa Waziri Lukuvi siku zote anatembea huku na kule kupambana na uhalifu huo uliokuwa umeshika atamu, na amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuhakikisha wenye haki zao wanazipata.

Mfano mtu anamiliki ardhi yake tangu miaka ya 90 na ana hati, lakini ghafla anatokea mwingine naye ana hati ya miaka ya 2000 hapo haihitajiki elimu ya sheria kujua nini kilifanyika hadi eneo la mwingine likamegwa pasipokuwa na mauziano yoyote.

Kwa sasa eneo la ardhi linaogopeka kufanya vinginevyo kwa kuwa wanajua iwapo itajulikana hatua zitachukuliwa dhidi ya muhusika.

Kila siku yanaibuka mapya katika sekta hiyo na yote yamevaa sura ya uonevu dhidi ya watu wengi wanyonge wakiwamo wanawake, wajane, yatima na wazee.

Kwa maeneo ya ardhi ambayo ni muhimu sana kiuchumi, nako ukifuatilia kwa kina waliojipatia maeneo hayo ni watu wenye nguvu ya fedha ambazo wamezitumia kuwapora kinyemela.

Naamini Waziri huyu akipewa nafasi na kuendelea kuchapa kazi kama anavyofanya Tanzania itapiga hatua kubwa kwenye kumaliza migogoro ya ardhi ambayo mingi inatengenezwa kwa manufaa ya wachache.

Kwa kuwa mipango miji mingi nchini ilipangwa kabla ya ongezeko la watu na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, ipo haja ya kufanyika kwa mipango mipya ya kupanga mjini na majiji na hasa kwenye maeneo mapya ambayo bado hayajaendelezwa.

Kwa kazi kubwa anayofanya Waziri Lukuvi ni wazi kuwa amejitengenezea maadui ambao walipora haki za watu na kwa kuwa wana fedha wanaweza kufanya lolote wakati wowote.

Kwa misingi hiyo ni vyema zikafanyika jitihada za kumlinda kwa namna yoyote ili aendelee kutetea wanyonge ambao wameporwa haki yao, kikubwa kinachotakiwa ni kutenda haki kwa kila anayestahili pasipokumwonea yeyote.