Ma –DC mmesikia maelekezo, wajibikeni

08Feb 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ma –DC mmesikia maelekezo, wajibikeni

HIVI karibuni, Rais Dk. John Magufuli, aliwalekeza wakuu wa wilaya nchini, kuacha kutumia vibaya madaraka yao, kwa kuweka watu mahabusu kwa saa 24, pasipo kuwafikisha mahakamani.

Ni jambo lililopigiwa kelele sana nchini, kwa tabia ya muda mrefu kuwapo matukio ya viongozi hao ambao ni wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yao ya kazi.

Ilifikia hatua baadhi ya wakuu wa wilaya wanaugeuka ‘Mungu Mtu’ katika eneo lake, akisahau yeye ni mwakilishi wa rais kwenye eneo alilopo na kila analolifanya inapokuwa kinyume cha sheria au lina sura ya uonevu, ni kumuaibisha aliyemteua.

Kutokana na hali hiyo, watu wengi wamejikuta wakiumia wakati mwingine kwa viongozi hao kutanguliza maslahi binafsi na pasipo kufuta sheria, lakini kwa kuwa anaweza kumuweka ndani mtu basi anaweza kufanya atakavyo.

Jambo hilo liliwaumiza wananchi wengi, hata kwa hisia na kwa bahati mbaya, hawana pa kukimbilia au kwenda kulalamika kirahisi, kuligana na mazingira yaliyopo.

Kwa kauli ya Rais, ambaye dhahiri ameonyesha kukerwa na kinachotokea, maana yake ni viongozi hao waache mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanawafanya watu waichukie serikali, kumbe ni mambo yanayotegemea tabia binafsi na serikali haiko kwenye kasoro hizo.

Baadhi ya viongozi walienda mbali zaidi, kwa kuwaweka watumishi wenzao ndani, jambo lililosababisha uhasama na kushindwa kufanyika kazi kwa utulivu na ufanisi.

Kazi za serikali, ofisi au taasisi yoyote, zinategemeana. Hivyo, kuna umuhimu kila mmoja kutimiza wajibu wake, pasipo kujiona yuko juu ya sheria au ana uwezo wa kumuonea yeyote.

Mtu anapokuwa kiongozi, kuna wakati kiwango chake cha uvumilivu kinapaswa kiwe juu zaidi na kutanguliza hekima, kuliko mihemko ya kibinadamu.

Mtu akitanguliza mihemko hiyo, atashindwa kufanya maamuzi sahihi kwa watu unaowaongoza na kuishia kuwaonea wale ambao kuna wakati hawana makosa.

Mtu anapohukumu kwa hisia pasipo vigezo vya kujitosheleza kufikia uamuzi huo, kwa kiasi kikubwa kunasababisha wato hao wasielewane.

Uzuri ni kwamba, nchini Tanzania kuna sheria na misingi thabiti iliyowekwa katika kutekeleza kazi zozote.

Inapendeza zaidi kuwaona viongozi wetu wakuu wa wilaya, wondoke kutoka upande wa kutaka kuogopwa na wahamie kwenye mazingira ya kuwa watumishi wa wa umma uliowaajiri, yaani wananchi.

Sidhani kama kwa vitisho na ‘kusweka’ watu ndani itasaidia sana watu kushirikiana shughuli za maendeleo.

Pia, unapokuwa kiongozi wa mfano, ni rahisi kuungwa mkono na wananchi wengi, hivyo kuwa na urahisi katika utekelezaji wa majukumu husika.

Wapo wakuu wa wilaya wanaofanya vizuri, pia wapo wachache wanaotanguliza hisia za hasira, maneno makali na yenye kuwaogopesha wananchi, kwa mambo ambayo wala hayakuhitaji kutumia nguvu au lugha hizo.

Kiongozi ni vyema ukaongoza kwa mfano na kwa vitendo, moja kwa moja wananchi wataiga mazuri yake.

Mfano hai, kiongozi anaweza kuzungumzia usafi wa mazingira mahali pake na wanakuona nawe umetoka, unashirikiana nao kufanya usafi na kupanda miti, lazima nao wataungana nawe.

Una hamasisha wananchi kujenga zahanati na wanatakiwa kutoa nguvu kazi, unaandaa siku ambayo utashirikiana nao kufanya kazi hizo kwa vitendo.

Maana yake ni kwamba, wataona umejishusha na kulingana nao, hivyo wao wanapaswa kufanya zaidi kwa kuwa kiongozi kafanya zaidi.

Unazungumzia kilimo, lakini hakuna siku umefika shambani au kushiriki hata katika shamba la mfano, mwishowe unajikuta unaongoza kwa nadharia kwa mambo ambayo yangeweza kufanyika kwa vitendo na kuleta mafanikio makubwa.

Haitoshi kutumia sheria na kuumiza watu, lakini kutumia busara na hekima tele, katika kushirikiana. Siyo rahisi kiongozi akajikuta kwenye migogoro ya ‘kuwasweka’ ndani, badala yake soma lugha zao na wanavyocheza, kisha anza kuwabadilisha wacheze vizuri na kama wanakosea, pia nawe iga yanayofaa kutoka kwao.

Baadhi ya maeneo nako kuna changamoto kubwa za mgogoro baina ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, kutokana na baadhi kutaka kuamrisha mwingine na hata kutaka ofisi yake ihudumiwe na ofisi ya mwingie.

Migogoro hiyo imeathiri utendaji kazi, kwa kuwa wamejikuta wanawagawanya watumishi kwenye makundi, kiasi cha kuwa na migogoro binafsi.

Tujiulize, namna hii inapotokea, kuna kila picha kwamba wanawaagusha viongozi waandamizi kitaifa, kuanzia Rais na Makamu wake, Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

Ni vyema wakatambua wanafanya kazi ya kutumikia umma na wanawajibika kwenye mamlaka iliyowateua.