Ma-RC, DC, simamieni agizo la serikali ununuzi wa pamba

23Jul 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ma-RC, DC, simamieni agizo la serikali ununuzi wa pamba

KWA zaidi ya wiki nne zilizopita, safu hii imekuwa ikibainisha kwa mapana kilio cha wakulima wa pamba, kinachotokana na kusuasua kwa ununuzi wake katika mikoa inayolima zao hilo.

Hali hiyo imesababisha pamba nyingi kuendelea kubaki mikononi mwa wakulima lakini pia katika maghala ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), baada ya baadhi ya wakulima kuipeleka kwa minajili ya kuiuza, lakini wakaishia kukopwa.

Kwamba wakaishia kukopwa baada ya kampuni za ununuzi kutopeleka fedha zikidai bei ya kununulia zao hilo ya Sh. 1,200 kwa kilo iliyowekwa na Serikali, haina faida kwao kutokana na kuporomoka bei katika soko la dunia.

Ni vyema kwamba Serikali hii sikivu ya Dk. John Magufuli iliyojinasibu kwa maneno na vitendo kuwa iko kwa ajili ya Watanzania wote na hasa wanyonge ambao kwa sehemu kubwa ni wakulima imeingilia kati suala hili.

Suala ambalo lilikuwa linaelekea kukatisha tamaa juhudi za wakulima wa pamba za kuongeza uzalishaji, hivyo kipato na hatimaye kuboresha maisha yao na ya taifa kwa ujumla, wakati taifa likielekea kwenye uchumi wa viwanda.

Si kwenye uchumi wa viwanda tu, lakini katika dhima nzima ya kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, takribani miaka sita ijayo.

Usikivu na utetezi wa serikali kwa wakulima wa zao hili, wengi wakiwa wadogo wadogo umeonekana katika msimamo wake ambapo bila kumumunya maneno imeendelea kusisitiza kwa wanunuzi kwamba bei ya kilo moja ya pamba ni kuanzia Sh.1,200 na si vinginevyo.

Kuna taarifa kwamba wanunuzi wamesuasua kununua zao hili kwa bei hiyo elekezi ya Serikali wakitaka walinunue kwa chini ya Sh. 1,000 ambayo kimsingi haimlipi mkulima ukilinganisha na gharama na nguvu anazowekeza kwenye uzalishaji wa zao hilo.

Lakini eneo jingine ambalo Serikali imeonyesha inatembea katika maneno yake linapokuja suala la kupigania maslahi ya wanyonge ni baada ya kulipatia ufumbuzi tatizo la kusuasua kwa masoko ya zao hilo.

Ni baada ya kuwa imefanya mazungumzo na wadau muhimu wa zao hilo na kufikia muafaka katika dhima nzima ya kuhakikisha pamba yote ya wakulima inanunuliwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu na wakulima wanalipwa fedha zao zote.

Hakikisho hili la Serikali lilibainishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ziara yake ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, aliyoifanya katika kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga, mkoani Tabora Julai 15.

Akasema kuwa baada ya mazungumzo, walikubaliana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuanza kutoa dhamana kwa benki nchini ili zitoe mikopo kwa wanunuzi wa zao hilo na hivyo kuwawezesha kuinunua pamba yote kwa pesa taslimu.

Aidha, akawaonya wanunuzi kutumia pesa watazopata kwa madhumuni lengwa.

Vilevile akawaagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yote yanayolima zao hilo wasimamie ipasavyo wanunuzi wote ili fedha zinazotolewa zitumike kwa manunuzi ya pamba na si vinginevyo.

Hata hivyo, taarifa ambazo Muungwana amezipata kutoka katika maeneo mbalimbali ni kwamba fedha zimeanza kupelekwa katika baadhi ya maeneo lakini si kwa kiwango cha kutosha.

Kwa hali hiyo bado kuna wakulima wengi waliokuwa tayari wamepeleka pamba yao kwenye maghala ya AMCOS hawajalipwa mpaka sasa, pia bado kuna wakulima wengi walio na pamba yao majumbani, wakisubiri fedha zipelekwe ili waiuze.

Muungwana anatoa rai kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwasimamia wanunuzi wa pamba ambao tayari wamepata mikopo ili kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa ya kununua pamba ya wakulima.

Ni muhimu wafanye hivyo ili kuhakikisha ahadi ya Serikali inatimia kwamba ifikapo Julai 30 pamba yote ya wakulima iwe imenunuliwa kwa ustawi wa wakulima wa zao hilo na maendeleo ya taifa kwa ujumla.