Ma-RC, DC simamieni malipo pamba ya wakulima nchini

09Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ma-RC, DC simamieni malipo pamba ya wakulima nchini

MSIMU wa kilimo katika baadhi ya maeneo nchini ambayo hupata mvua za masika kati ya mwezi Oktoba hadi Machi, tayari umeshaanza na wakulima katika hekaheka mbalimbali za uzalishaji katika mashamba yao.

Na kama takwimu kutoka vyanzo mbalimbali zinavyobainisha, kilimo ni shughuli kuu ya kiuchumi kwa takribani asilimia 70 ya Watanzania karibu milioni 55 kwa sasa, wengi wakiishi vijijini ambako ndiko hasa kilimo kinaendeshwa kwa kiwango kikubwa.

Mojawapo ya maeneo hayo ni Kanda ya Ziwa ambayo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula kwa ajili ya usalama wa chakula na lishe, bila kusahau mazao ya biashara, likiwamo zao maarufu la pamba katika kanda hiyo.

Hata hivyo, wakati msimu ndio huo umeshaingia na harakati mbalimbali za kilimo zikiendelea zikiwamo za ununuzi wa pembejeo kwa maana ya mbegu bora, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao na mbolea bado kuna kilio kwa baadhi ya wakulima wa pamba.

Wakulima kutoka katika baadhi ya maeneo yakiwamo ya Kanda ya Ziwa.

Kilio anachokizungumzia Muungwana ni cha baadhi yao kutolipwa fedha mpaka sasa wakati msimu wa kilimo ukianza, baada ya kuwa wameuza pamba kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS).

Hali iko hivyo hata baada ya ahadi ya serikali kuwa wakulima wote watakuwa wamelipwa haki yao hiyo kabla ya msimu huu wa kilimo ili wajiandae vyema.

Msimu ambao pamoja na mengine, unamhitaji mkulima awe na fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kilimo, yakiwamo yaliyobainishwa hapo juu.

Septemba 21, mwaka huu, akiwa Chato katika moja ya ziara zake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa ahadi kuwa wakulima wote waliouza pamba kwenye vyama vya ushirika watalipwa fedha zao.

Kwamba serikali ilikuwa imeingilia kati na kuruhusu wanunuzi wa pamba wachukue fedha benki ili pamba yote inayonunuliwa kwa wakulima iweze kulipwa.

Kwa mujibu wa taarifa alizozipata Muungwana kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, kuna baadhi ya kampuni za ununuzi hazijapeleka fedha kwa wakulima sasa ikiwa ni zaidi ya mwezi mzima.

Kwa mfano katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, kuna baadhi ya kampuni za ununuzi hazijawapelekea wakulima fedha zao kwa zaidi ya wiki sita sasa, pamoja na kuwa zimeshasomba pamba ya wakulima kutoka kwenye maghala ya AMCOS.

Kwamba wanunuzi wameshachukua pamba ya wakulima na kuipeleka kwenye viwanda vyao na baadhi ya kampuni zinaendelea kusomba pamba hiyo kutoka katika maghala ya AMCOS, lakini kuwapelekea wakulima fedha zao, bado imekuwa ngumu.

Kama ilivyobainishwa hapo juu, baadhi ya maeneo tayari yako kwenye msimu wa kilimo, lakini kuna wakulima ambao hawajalipwa fedha zao!

Muungwana anaona hali hii kimsingi inakwamisha juhudi za wakulima za kuongeza uzalishaji katika shughuli hii wanayoitegemea kwa udi na uvumba ili kuboresha maisha yao, na hivyo kuondokana na lindi la umaskini.

Katika moja ya maelekezo yake kuhusiana na sakata hili, Waziri Mkuu aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwasimamia wanunuzi.
Kwamba kuwasimamia ili kuhakikisha kuwa fedha wanayochukua kutoka benki kwa dhamana ya serikali ili wakawalipe wakulima wa pamba, inatumika kwa kusudi hilo.

Sasa inapotokea kwamba kuna baadhi ya wakulima wana zaidi ya mwezi hawajalipwa fedha zao, wakati wanunuzi tayari wamesomba pamba yao, Muungwana anaona hapo kuna upungufu katika usimamizi wa maelekezo ya Waziri Mkuu.

Ni kwa maana hiyo Muungwana anawaasa wakuu hawa wahakikishe wanunuzi wanawalipa wakulima fedha zao, ili waweze kugharamia pamoja na mengine mahitaji ya kilimo, ikichukuliwa msimu wa kilimo tayari umeshafika kwenye baadhi ya maeneo.