Ma-RC watekeleze maagizo ya Rais kwa makini

20Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Ma-RC watekeleze maagizo ya Rais kwa makini

MWANZONI mwa wiki hii Rais John Magufuli aliwaapisha wakuu wa mikoa aliowateua na kuwapa maagizo mazito ya kufanya kazi ili kutatua kero za wananchi, na si kwenda kufanya siasa.

Katika maagizo hayo, Rais aligusia mambo mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa na wakuu hao wa mikoa ikiwamo kushughulia tatizo la wafanyakazi hewa kwenye Halmashauri zote nchini.

Lakini leo nataka kuzungumzia hili la kukamatwa kwa vijana watakaokutwa wakicheza pool asubuhi badala ya kufanya kazi.

Amri hii inaonyesha ni jinsi gani Rais alivyo na uchungu kwa maendeleo ya nchi hii, hasa kwa kuzingatia kwamba kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru wa nchi hii, bado kuna maendeleo ni ya kusuasua.

Ni kweli wapo vijana wengi ambao wanarandaranda kutwa nzima bila kufanya kazi yoyote huku wengine wakiishia kucheza pool.

Katika kundi hilo, wapo wasiotaka kufanyakazi kwa kuwategemea ndugu ama wazazi na wale wanaofanya kazi kwa zamu, ingawa kundi kubwa linaweza kuwa la wale wasio na ajira.

Pamoja na kwamba lengo la Rais ni zuri, nadhani ipo haja ya kuangalia kwa umakini utekelezaji wa maagizo yake kwani inawezekana yakawakumbuka hata wale wasiohusika iwapo halitatekelezwa kwa umakini.

Ninasema hivyo kwa sababu kama nilivyosema, wapo baadhi ya vijana wanaofanya kazi kwa zamu na hasa sehemu za mijini wakiwamo madereva wa daladala, bodaboda na bajaji.

Hata maeneo ya vijijini wapo vijana hasa wale wanaojishughulisha na uvuvi ambao wakati mwingine hufanya kazi hiyo wakati wa usiku na kisha asubuhi wakaendelea na mambo mengine.

Lakini pia kuna kundi la vijana ambao wenyewe hataki kabisa kuajiriwa ama kujiajiri, wao kila kukicha ni kwenda vijiweni na kupiga soga wakisubiri tu bila kujali kwamba wanapoteza muda wao bure.

Vijana walio katika kundi hili ndio wanaotakiwa kushughulikiwa mapema sana kwa sababu wao ni nguvu kazi ya taifa, lakini kwa sababu wanazozijua wenyewe wanaamua kukaa vijiweni.

Bahati mbaya wataalam wa sheria wanasema kuwa hakuna sheria ya kumzuia mtu kucheza pool table asubuhi, hivyo wakati mwigine maagizo ya Rais yanaweza kugonga ukuta ingawa lengo lake ni zuri.

Cha msingi ni kwamba ipo haja ya kuwachambua na kuwatambua wanaofanya kazi kwa zamu na wale ambao hawana kazi na wasiopenda kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba kila mmoja anashughulikiwa kulingana na mazingira yake.

Katika mlolongo huu, ikumbukwe kwamba kuna kundi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira pia, ambao wamekuwa wakihangaika huku na kule bila kupata kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uchache wa ajira na huku wengine wakiwa hawana sifa.

Hata kwa maeneo ya vijiji, wapo vijana ambao hata kama wangependa kujiajiri katika kilimo, hawana ardhi ya kulima kutokana na ukosefu wa eneo wa namna yoyote.

Binafsi ninadhani zipo njia nyingi za kuweza kuwasaidia vijana hasa wale wanaopenda kuajiriwa ama kujiajiri ikiwa ni pamoja na kusubiri Sh. milioni 50 za Rais Magufuli kwa kila kijiji ili wakopeshwe na kuwa wajasiriamali.

Kwa wale ambao hawataki kujishughulisha kabisa, wawe mijini ama vijijini, basi wakamatwe kwa nguvu na kupelekwa katika mashamba wakalime kama ambavyo Rais ameagiza.

Vijana waliojaa kwenye vituo vya mabasi wakipiga debe, kwa mfano, ambao ni rahisi kuwatambua, hao wanastahili kuchukulia hatua mapema ili wakafanye kazi halali ikiwamo ya kilimo.

Ikiwezekana, Sheria ya Nguvukazi ya mwaka 1969 ambayo ilifutwa, irejeshwe ili kudhibiti kundi la watu wasiotaka kujishughulisha, kwani sio siri kwamba utegemezi na uvivu vimejengeka miongoni mwa Watanzania.