Maadhimisho yaje na mbinu mpya zaidi kunusuru wajawazito, watoto

05May 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maadhimisho yaje na mbinu mpya zaidi kunusuru wajawazito, watoto

KATIKA kupambana na vifo vya wajawazito, serikali imechukua hatua mbalimbali, zikiwamo kuanzisha kampeni maalum ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mbali na kampeni hiyo, serikali imejenga vituo vingi vya huduma za afya ngazi zote, ambayo wajawazito wanajitokeza kuhudhuria kliniki, ili kuhakikisha wanakuwa salama, tangu mimba hadi kujifungua.

Katika kuimarisha mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji taarifa za wajawazito, wameshaanza kuimarisha na kufuatilia maisha ya kila mmoja tangu anapopata ujauzito, muda wa kuanza kliniki, kujifungua hadi kuvusha siku 42 baada ya kujifungua.

Binafsi, ninaamini ni mfumo unaoweza kusaidia kuokoa maisha ya wajawazito nchini, kutokana na kupitia mfumo huo serikalini, inapata taarifa za wajawazito kujua ni aina gani ya dawa zinazohitajika kumhudumia mjamzito.

Kwa nini? Sababu kubwa ni kwamba, serikali inasema mfumo huo utaeleza uhalisi wa miundombinu iliyopo na unaohitajika, hali kadhalika uwajibikaji wa watumishi wa afya kwa ujumla wao, hata mmoja mmoja, ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wajawazito.

Ni wazi kwamba, njia hiyo inaweza kuwa na manufaa katika kupunguza vifo vitokanavyo uzazi kwani inalenga kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa kila mjamzito, ili kuokoa maisha yao na watoto wachanga.

Wakati leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani, huku wadau wa afya ya uzazi wakiwa na maoni yao wanayoamini kwamba yakifanyiwa kazi, yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi nchini.

Miongoni mwa maoni hayo, ni serikali kuwekeza zaidi katika kuboresha mazingira ya kazi na ubora wa vitendea kazi kama njia mojawapo ya kukabiliana na vifo, hivyo vinavyogusa pia watoto wachanga.

Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), kinasema licha ya kuwapo taarifa zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali, zikionyesha kuongezeka hospitali na vituo vya afya kitaifa, lakini viwango vya  vifo vya uzazi bado vimeendelea kuwa juu.

Hata hivyo, inakiri na kutambua hatua kubwa ambazo Tanzania imeendelea kuzipiga, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wenyue umri chini ya miaka mitano, lakini inatamani juhudi zaidi zifanyike, nchi ifikie lengo la maendeleo endelevu la asilimia 70 kwa vizazi 100,000 na kuondoa vifo vinavyoweza kuepukika mwaka ifikapo mwaka 2030.

Hivyo basi, wakati dunia inaadhimisha Siku ya Wakunga Duniani, ninadhani ipo haja kwa ushauri huo ukafanyiwa kazi, ili kuendelea kuokoa maisha ya Watanzania wanaojifungua na hata watoto wachanga waliopo hadi wenye umri wa miaka mitano.

Suala la kuwekeza zaidi katika ukunga kama inavyoshauri TAMA, mara zote ni jambo muhimu, kwani wakunga wanahimiza wakiwa wengi, inawasaidia kupunguza vifo inavyotokana na uzazi.

Nakumbuka, Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Afya, Uzazi na Idadi ya Watu (UNFPA) Tanzania, Dk. Wilfred Ochan, anahimiza Siku ya Wakunga Duniani, ina nafasi ya kuangalia takwimu na jinsi uwekezaji ulivyo kwenye ukunga nchini.

Anatilia mkazo, vifo vingi vinavyotokana na uzazi vinazuilika, hasa kukiwapo huduma bora kutoka kwa wataalamu waliowezesha, ili wasaidie kutoa huduma tangu hatua ya mimba hadi mtoto anapozaliwa.

Anakiri, ripoti ya UNFPA ya mwaka kuhusu Shirikisho la Wakunga na WHO, ina angalizo iwapo serikali duniani zitawekeza kwa wakunga, maisha ya watu mlioni 4.3 yanaweza kuokolewa kila mwaka kuanzia mwaka 2035.

Kwa maana hiyo, ni wazi kwamba uwekezaji zaidi unatakiwa kufanyika  kwenye afya za wajawazito, ili kuhakikisha wanajifungua salama, pia watoto wanaozaliwa nao wanabaki salama.