Maadhimsho haya ya mazingira yasaidie kumaliza biashara mkaa

05Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maadhimsho haya ya mazingira yasaidie kumaliza biashara mkaa

NASEMA haya nikisimama juu ya jukwaa la kilele maadhimisho ya leo, Siku ya Taifa ya Mazingira.

Hapo tunajua chanzo rahisi cha nishati ya kupikia, pia biashara kwa umma mijini na vijijini, kuna nishati mkaa.

Hiyo inahusisha wasambazaji wake wakubwa, rejareja na jumla. Kuna wanaopika majumbani, pia biashara; mamalishe na hotelini.
Kimsingi, mkaa ni chanzo kikuu cha nishati ya kupikia nchini. Pamoja na umuhimu wake huo, sasa kuna haja ya kuangalia matokeo ya ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa wa biashara.

Siyo siri kwamba ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa ambao unauzwa kwa ajili ya kupikia, unasababisha uharibifu wa mazingira, ikiwamo uwezekano wa maeneo yanayokatwa miti kubaki jangwa.

Biashara ya mkaa inashamiri kutokana na ukweli kwamba, gharama yake inaweza kuwa nafuu kuliko nishati nyingine, lakini ikumbukwe kuwa ukataji miti usiozingatia utaratibu, ni hatari kwa misitu na mazingira kwa jumla ambayo siku yake inaadhimishwa leo.

Mkaa umekuwa ukisafirishwa kwa baiskeli, pikipiki na magari, hivyo kila msafirishaji ana bei yake kulingana na gharama anayoitumia, usambazaji huo unaweza kuufanya mkaa kuuzwa kwa bei nafuu kuliko nishati nyinginezo.

Kwa hali hiyo, matumizi ya mkaa yatakuwa ni makubwa na kuna uwezekano wa kusababisha uharibifu mkubwa wa misitu, hivyo kuwapo changamoto nyingine za mazingira.

Uharibifu wa mazingira unaanza kule inakokatwa, inachomwa na mkaa unauzwa, hivyo ni muhimu wahusika wa biashara hiyo kuwa makini.

Biashara ya mkaa ni matokeo ya ukataji miti, pia unaweza kusababisha upotevu wa rutuba, upotevu wa mimea asilia, upotevu wa viumbe asilia, upungufu wa majisafi na salama.

Wakati huu wa maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, ni muhimu wakataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, watambue kwamba wanachangia uharibifu wa mazingira.

Mikoa kama vile Singida, Dodoma, Shinyanga, Manyara, Simiyu na Geita, imekuwa ikitajwa kuathiriwa na biashara ya mkaa, kwa vile inakumbwa na ukame na jangwa la ukataji miti ya mkaa.

Wakati umetimu sasa, nishati mbadala ufikiriwe namna ya kushusha bei Watanzania waweze kuipata kwa gharama nafuu.

Watu wanakimbilia kwenye mkaa, kwa sababu bado bei yake wanaweza kuimudu na umekuwa ukiuzwa kuanzia shilingi 1,000 kwa kipimo kuliko mafuta ya taa ambayo bei yake ni zaidi ya Sh. 1,000.

Hiyo ni bei kwa jiji kama Da es Salaam, ambako jamii imetakiwa ihamasishwe kupanda miti kwa wingi kwa kutumia kaulimbiu ya 'panda miti kata mti.' Utaratibu huo unaweza, walau ukasaidia kulinda mazingira ya nchi.

Vilevile wanaofanya biashara ya mkaa nchini wanapaswa kuzingatia matumizi bora ya mkaa katika misingi bora na endelevu, ili misitu iendelee kuwapo, ingawa inawezekana siyo suluhisho kamili la kumaliza jangwa.

Kiuhalisia, nishati mbadala ni suluhisho la yote. Kuna haja ya kujali na kuthamini umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda uoto wa asili.

Ipo kaulimbiu moja ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyowahi kunadiwa 'Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa Manufaa ya Baadaye.' Hii ina maana muhimu sana, ikipingana na ukataji miti usiolingana na kiasi kinachopandwa.

Moja ya mambo ambayo Wizara ya Nishati, inahimiza, ni kuendeleza vyanzo vingine vya nishati ikiwamo umeme, gesi na mafuta, lakini bado matumizi yake hayajaenea kwa Watanzania wengi.

Ingawa marufuku biashara ya mkaa bado haijafikiwa, lakini uvunaji holela wa miti kwa ajili ya mkaa unaweza kuzuiwa, huku juhudi kuwapo kwa nishati mbadala zikiendelea kuchukuliwa.