Maajabu ya tango katika kupambana na maradhi

07Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Afya
Maajabu ya tango katika kupambana na maradhi

MATANGO yamekuwa maarufu kwa watu wengi kutokana kutumiwa kama chakula, juisi, tunda au saladi wakati wa mlo. Kila mtu hutumia kadri anavyoweza na namna anavyotengeneza wakati wa kuyatumia.

Wakati mwingine badhi ya watu huchanganya vuipande vya tango na vile vya ndimu au limau na kuchanganya na maji kisha kuweka kwenye chupa kwa saa kadhaa na kuanza kunywa. Wanaotumia hivyo husema wanakunywa ili kupungiza uzito.

Pamoja na sababu hiyo na kutumiwa kwa namna mbalimbali, huenda wengi hawajui faida zake. Lakini ukweli ni kwamba tango lina faida nyingi kiafya katika mwili wa binadamu.

Miongoni mwa faida hizo kiafya ni kama zifuatazo;-

Kuondoa Sumu

Kwa mujuibu wa wataalamu wa sayansi za afya, tango ambalo huwekwa katika jamii ya mboga na matunda, lina virutubisho muhimu kwa afya ya mwanadamu ikiwamo kuondoa sumu mwilini.

Kutokana na umuhimu huo, watu wanashauriwa kutumia tango ana liwe katika mfumo wa juisi kama baadhi wanavyotengeneza, kula likiwa bichi au kukatakata vipande na kisha kutafuna.

Kwa ujumla, kama yalivyo matunda mengine na mboga za aina mbalimbali, tango lina maji mengi ambayo humsaidia mtu ambaye mwilini ana sumu kutokana na kula vyakula, unywaji wa pombe na sumu za kimazingira, kuondokana na sumu hivyo kuwa na afya njema.

Kuongeza Maji Mwilini

Maji ni muhimu katika mwili wa binadamu. Kuwapo kwa maji mengi mwilini, huwezesha mmeng’enyo wa chakula kufanyika vizuri na pili kufanya joto kuwa katika hali nzuri.

Ulaji wa tango, husaidia mwili kuwa na maji yenye vitamini na viinilishe ambavyo huuwezesha mwili kuwa katika afya njema. Kwa mantiki hiyo, inashauriwa mtu kula tango mara kwa mara kwa ajili ya kufanya mwili kuwa na maji.

Kwa mujibu wa gazeti la afya ya ‘Healthline’, ulaji wa matunda na mboga huchangia asilimia 40 ya maji mwilini. Utafiti unaonyesha kuwa tango lina asilimia 96 ya maji huku asilimia zilizobaki zikiwa ni vitamin na viinilishe tu.

Faida za kuwa na maji mengi mwilini pia husaidia mtu kupata haja kubwa kwa urahisi na bila matatizo.

Kutokana na umuhimu huo, wanasayansi wanashauri kuwa wakati wa kiangazi, watu wanapaswa kula matango na matunda mengine kwa wingi ili kuwa na maji ya kutosha mwilini.

Kupunguza Uzito

Je, una uzito kuzidi mwili na urefu wako? Basi njia mojawapo ya kupunguza ni kula mboga na matunda kwa wingi .

Tango kama yalivyo matunda mengine na kama baadhi ya watu wanaovyodhani kuwa ni jamii ya mboga, ina virutubisho vingi ambavyo husaidia kupunguza uzito katika mwili. Hiyo ni kutokana na kuwa na ‘kalori’ chache.

Kupambana na sukari

Utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa mtu mwenye tatizo la sukari mwilini, anakuwa katika nafasi nzuri ya kupunguza ugonjwa huo na kudhibiti tatizo kuwa kubwa.

Katika moja ya utafiti uliofanywa, kwa mujibu wa Healthline, ulaji wa tango mara kwa mara unasaidia kupunguza tatizo la sukari kwa mgonjwa. Utafiti huo ulihusisha panya ambaye aliwekewa sukari na kupewa matango. Baada ya muda Fulani, sukari katika mwili wa panya huyo ilipungua kwa kiasi kikubwa.

Shinikizo la Damu

Tango ni chanzo cha madini ya potasiamu, magnesiamu pamoja na nyuzinyuzi. Vitu hivyo ni virutubisho muhimu katika kupambana na shinikizo la damu katika mwili wa binadamu.

Utafiti unaonyesha kuwa utumiaji wa mara kwa mara wa tango hasa juisi yake, husaidia kupunguza tatizo la shinikizo la damu hasa lwa wazee ambao tayari wanasumbuliwa na maradhi hayo.

 

Kuimarisha Ngozi

Utumiaji wa mara kwa mara wa tango husaidia ngozi kuwa nyororo na yenye afya. Hiyo ni kutokana na virutubisho ambavyo huifanya ngozi kutokutoka jasho kwa wingi.

Sambamba na hiyo, unywaji wa juisi ya tango husaidia ngozi kuwa ng’avu wakati wote na kupunguza vipele na muwasho.

Kwa ujumla, ulaji wa tango mara kwa mara una faida nyingi kwa mwili wa binadamu. Miongoni mwa manufaa hayo ni kupunguza uzito wa mwili, kuwa na uwiano mzuri wa maji mwilini,  mfumo wa chakula kuwa bora na kupungua kwa kiwango cha sukari mwilini.