Maambukizi ya njia ya mkojo, matibabu yake

06Mar 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Maambukizi ya njia ya mkojo, matibabu yake

‘UTI’ ni maambukizi katika njia au mfumo wa mkojo ni kifupisho cha maneno ya kitaalamu ya Urinary Tract Infection. Maambukizi haya hutokea katika sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo kama figo, kibofu na mrija wa mkojo.

Hata hivyo mengi huhusisha sehemu ya chini yaani kibofu na mrija wa mkojo au urethra. Katika hali ya kawaida, wanawake wapo katika hatari zaidi ya kupata UTI kuliko wanaume.

CHANZO CHA UTI

Kwa kawaida mkojo haupaswi kuwa na vijidudu vyovyote. Ndiyo maana wataalamu wanasema maambukizi ya mfumo wa mkojo huanzia katika sehemu ya mwili ambazo mkojo hupitia ukitoka nje ambayo ni mwanzo wa mrija wa mkojo. Ugonjwa hutokea baada ya vimelea kuvamia njia hii ya mkojo kuanzia kwenye mrija huo.

Baada ya uvamizi huanza kuzaliana kwenye kibofu cha mkojo na imethibitika kuwa chanzo kikubwa cha UTI ni vimelea vya Escherichia Coli au E. coli. Vimelea hivi kwa kawaida huishi mwilini kwenye utumbo wa binadamu.

Bakteria huyu husogezwa kutoka sehemu ya haja kubwa hadi unapoanzia mrija wa mkojo lakini, sababu kuu mbili zinazomsogeza ni uchafu mhusika kutojisafisha kikamilifu baada ya haja kubwa na pia kujamiiana.

Ifahamike kuwa mkojo unapotoka mwilini husaidia kupunguza idadi ya vimelea vilivyovamia njia hiyo kwa kutoka nao lakini hauwezi kusafisha wadudu wote katika njia hiyo.

Kwahiyo bakteria husafiri kutoka njia hii ya mkojo hadi kwenye kibofu ambako hukaa, huzaliana na kusababisha maambukizi ambayo huendelea pale wanapozidi kusambaa kuelekea sehemu ya juu ambayo ni figo. Wanapoingia kwenye figo, husababisha madhara na hatari zaidi kama mgonjwa hatatibiwa.

HALI ZINAZOLETA UTI

Zipo hali mbalimbali ambazo ni pamoja na maumbile ya wanawake watu hawa wana mrija mfupi wa kutolea mkojo kuliko wanamume. Hii hupunguza umbali wa bakteria kusafiri na hivyo kufikia haraka kibofu cha mkojo na kusababisha madhara.

KUJAMIIANA

Wanawake wanaofanya mapenzi na wenza wengi mara kwa mara wapo kwenye hatari ya kuambukizwa UTI zaidi ya wasiofanya ngono. Kujamiiana na wanamume zaidi ya mmoja kunaongeza uwezekano wa kupata maradhi hayo. Hata hivyo, kwenda haja ndogo kila baada ya tendo hilo kunaelezwa kuwa hupunguza uwezekano wa kupata maambukizi.

KUZIBA NJIA YA MKOJO

Watu wenye mawe ya figo pamoja na tezi dume wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya njia ya mkojo.

MRIJA WA KUJISAIDIA

Wagonjwa wanaotumia mrija wa kusaidia kutoa mkojo ‘catheter’kukojoa wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizo hayo.

UPUNGUFU WA KINGA

Upungufu wa kinga mwilini unasababisha kuwa kwenye hatari kubwa pia ya kupata UTI. Watu hawa ni wale wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU), kisukari pamoja na walio katika matibabu yanayohusisha kupunguza kinga ya mwili kama saratani

DALILI ZA UTI

Hizi ndizo dalili zinazojitokeza baada ya mtu kupata maambukizi ya njia ya mkojo, kwanza ni kujisikia kukojoa mara kwa mara, kujisikia kuwaka moto wakati wa kukojoa, kupata mkojo unaotoka kidogo mara kwa mara, kukojoa mkojo wenye harufu kali, maumivu ya nyonga hasa wanawake, kukojoa damu au mkojo mwekundu pamoja na homa nyepesi na kujisikia uchovu.

KUJIEPUSHA

Jifunze namna ya kujisafisha kwa wanawake wanaojisafisha kutoka nyuma kwenda mbele (baada ya haja kubwa) wapo katika hatari kubwa ya kupata UTI. Usifute ama kunawa kutoka nyuma. Jifute ama jisafishe mbele kwanza kisha rudi kwenye eneo la haja kubwa.Usiweke kinyesi sehemu ya haja ndogo. Fanya hivyo hata kwa mtoto mchanga au binti unapomtawaza.Kumbuka namna sahihi ya kujisafisha baada ya haja kubwa kwa mwanamke ni kutoa uchafu mbele kwenda nyuma.

AINA ZA UTI

Maambukizi hutofautiana kutokana na sehemu ya mwili ilipoathiri. Kutokana na hili,zipo aina tatu nazo ni maambukizi kwenye figo na dalili zake ni maumivu upande wa juu na nyuma katikati ya mwili, homa kali, kichefuchefu na kutapika
Maambukizi kwenye kibofu yanayojionyesha kwa njia kwenye kukojoa mara kwa mara na kupata maumivu wakati wa haja ndogo, damu kuonekana kwenye mkojo, kujisikia maumivu chini ya tumbo.Maambukizi kwenye mrija wa mkojo hujitokeza kwa kujiskia kuwaka moto wakati wa haja ndogo.

MADHARA

UTI inapotibiwa hupona na ni mara chache inaweza kuleta madhara kwa mtu. Lakini isipotibiwa inamsababishia muathirika madhara makubwa yakiwamo: Kuharibu figo, marudio ya ugonjwa mara kwa mara, kuongeza uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu au njiti (kwa wajawazito), kupungua upana wa njia ya mrija wa kutolea mkojo, kufeli kwa figo na pia kifo.

MATIBABU

Haya hutegemea hali ya mgonjwa (umri, ujauzito au maradhi kama kisukari au saratani) na kusambaa kwa Vimelea. Mgonjwa anayeumwa sana huhitaji sindano za na hata kulazwa hospitalini kwani anaweza kuwa na maambukizi kwenye figo na baadaye ndani ya damu.

Kwa mgonjwa mwenye UTI isiyo kali ya kwenye kibofu au mrija wa mkojo hutibiwa kwa kumeza dawa za kuangamiza vimelea antibiotic.

Kwa wale wenye UTI iliyosababishwa na vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya kujamiiana (STIs)’ hawa huhitaji dawa zaidi ya moja. Hata hivyo wajawazito na watoto hawapaswi kutumia baadhi ya ‘antibiotics’ kutokana na madhara yanayoweza kutokea.

KUPUNGUZA MAMBUKIZI

Njia za kujiepusha au kupunguza uwezekano wa kupata ‘UTI’ ni pamoja na kunywa maji kwa wingi: Tiba hii huondoa ugonjwa kwa vile mtu hukojoa mara kwa mara na kusaidia kusafisha njia ya mkojo.

Kutochelewa kwenda haja ndogo nako ni kinga kwani husaidia kupunguza idadi ya wadudu wanaoweza kufika kwenye kibofu au kuzaliana.

Kadhalika kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma (baada ya haja kubwa kwa wanawake).
Pia vaa nguo za ndani zisizobana sana na zilizotengenezwa kwa pamba na siyo zile zisizopitisha hewa.