Maambukizi ya njia ya mkojo, matibabu yake-2

13Mar 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Maambukizi ya njia ya mkojo, matibabu yake-2

Wiki iliyopita tulijifunza maana ya UTI, kifupisho cha kitaalamu cha ugonjwa wa maambukizi ya njia ya mkojo kuwa ni ‘Urinary Tract Infection’.

Aidha tulijifunza kuwa chanzo cha UTI ni maambukizi ya mfumo wa mkojo katika sehemu ya mwili ambayo mkojo hupitia na kwamba ugonjwa huo huweza kumpata mtu endapo hali mbalimbali zitajitokeza, ikiwemo zifuatazo:

Maumbile, ambapo wanawake huweza kupata UTI kirahisi kutokana na kuwa na njia fupi ya mkojo kuliko wanaume, wanawake wenye kufanya mapenzi mara kwa mara na wenza wao, kuziba kwa njia ya mkojo kutokana na kuwapo kwa mawe kwenye figo ama maradhi ya tezi dume, wagonjwa wanaotumia mfuko wa haja ndogo, kuwa na upungufu wa kinga mwili kufuatia mashambulizi ya VVU.

Aidha, wiki iliyopita tuliona pia kuwa baadhi ya dalili za kuugua UTI ni kupata haja ndogo mara kwa mara, kuhisi kuwaka moto njia ya mkojo wakati wa kujisaidia na kukojoa mkojo wenye harufu mbaya.

Namna ya kujiepusha na ugonjwa huu, tulijifunza, ni pamoja na wanawake kuwa na tabia ya kujisafisha kutoka mbele kwenda tundu la haja kubwa baada ya kujisaidia.

Aina za UTI tulijifunza kuwa ni 3; maambukizi kwenye figo, maambukizi kwenye kibofu na maambukizi kwenye mrija wa mkojo. Leo tuangalie madhara ya ugonjwa huu…

MADHARA

UTI inapotibiwa hupona na ni mara chache inaweza kuleta madhara kwa mtu. Lakini isipotibiwa inamsababishia muathirika madhara makubwa yakiwamo:

Kuharibu figo, marudio ya ugonjwa mara kwa mara, kuongeza uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu au njiti (kwa wajawazito), kupungua upana wa njia ya mrija wa kutolea mkojo, kufeli kwa figo na pia kifo.

MATIBABU

Haya hutegemea hali ya mgonjwa (umri, ujauzito au maradhi kama kisukari au saratani) na kusambaa kwa Vimelea. Mgonjwa anayeumwa sana huhitaji sindano za na hata kulazwa hospitalini kwani anaweza kuwa na maambukizi kwenye figo na baadaye ndani ya damu.

Kwa mgonjwa mwenye UTI isiyo kali ya kwenye kibofu au mrija wa mkojo hutibiwa kwa kumeza dawa za kuangamiza vimelea antibiotic.

Kwa wale wenye UTI iliyosababishwa na vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya kujamiiana (STIs)’ hawa huhitaji dawa zaidi ya moja. Hata hivyo wajawazito na watoto hawapaswi kutumia baadhi ya ‘antibiotics’ kutokana na madhara yanayoweza kutokea.

KUPUNGUZA MAMBUKIZI

Njia za kujiepusha au kupunguza uwezekano wa kupata ‘UTI’ ni pamoja na kunywa maji kwa wingi: Tiba hii huondoa ugonjwa kwa vile mtu hukojoa mara kwa mara na kusaidia kusafisha njia ya mkojo.

Kutochelewa kwenda haja ndogo nako ni kinga kwani husaidia kupunguza idadi ya wadudu wanaoweza kufika kwenye kibofu au kuzaliana.

Kadhalika kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma (baada ya haja kubwa kwa wanawake).
Pia vaa nguo za ndani zisizobana sana na zilizotengenezwa kwa pamba na siyo zile zisizopitisha hewa.