Mabadiliko ya sheria yachagize kudhiti ulevi kwa madereva

31Jul 2019
Mashaka Mgeta
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabadiliko ya sheria yachagize kudhiti ulevi kwa madereva

KWA kipindi cha takribani miezi mitatu, nimeshiriki fursa ya uhamasishaji wenye lengo la kuleta mabadiliko ya fikra, sera, kanuni  na sheria ili kukidhi azma ya kuifanya Tanzania iondokane na ajali za barabarani.

Mabadiliko hayo yanalenga kuchagiza kasi ya utekelezaji wa mipango mbalimbali inayofanywa na polisi wa usalama barabarani, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wadau wengine kupunguza kama si kuondoa kabisa uwapo wa ajali hizo zinazogharimu maisha na uharibifu wa mali.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeainisha vyanzo kadhaa vya ajali za barabarani ambavyo kama vitashughulikiwa na kada tofauti, kila moja kwa nafasi yake, basi ni rahisi kuipata sehemu ya dunia kama Tanzania isiyokuwa na ajali hizo.

Kwa mujibu wa WHO inayofanya kazi na kuwa na mafungamano ya mahusiano na Tanzania, vyanzo hivyo ni pamoja na mwendokasi, kutovaa kofia ngumu upande wa pikipiki, kutofunga mikanda ya kwenye gari, ulevi, miundombinu mibovu, miongoni mwa mengine mengi.

Nikiwa katika ushiriki huo unaoratibiwa na Wakfu wa Vyombo vya Habari (TMF), nimefanikiwa kujikita zaidi katika nafasi ya ulevi kwa jinsi inavyochangia kutokea na ongezeko la ajali za barabarani.

Nimepitia maandiko kadhaa, nimezungumza na vyanzo vya habari kutoka kada tofauti na kubaini kuwa, hatari bado inazidi kulikabili taifa ikiwa suala la ulevi kama sehemu ya vyanzo vya ajali za barabarani, halitapewa kipaumbele na nguvu zaidi za kisheria katika udhibiti wake.

Mathalani, kifungu cha 44 hadi 49 ya Sheria ya Usalama Barabarani vinaeleza kuwa ukomo wa kiwango cha kilevi kinachopaswa kubainika kwa dereva ni kinachofikia 0.008, zaidi ya hapo kunakuwa na mwanya wa kutolewa adhabu kwa mhusika.

Lakini kwa upande wake, WHO imeweka kiwango kwa ajili ya udhibiti wa ulevi kwa madereva kuwa ni 0.005. kiwango hiki kinatumika pia kwenye nchi kadhaa duniani.

Pasipoweka taarifa za kitaalamu kuhusu ujazo wa kiwango hicho, tafsiri rahisi inayoweza kueleweka kwa haraka ni kwamba Tanzania inatumia kiwango kikubwa cha utambuzi wa kilevi kwa madereva kuliko ilivyo kwa WHO.

Nilipozungumza na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu, akasema miongoni mwa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani yanayopendekezwa sasa ni kuhusu kupunguza kiwango hicho angalau kufikia 0.005 kama ilivyo kwa WHO.

Lakini kwa mtazamo wake binafsi, Kamanda Musilimu akasema ingefaa sana kiwango hicho kuwa 0.00, lakini kwa vile kuna sababu za kibaiolojia kuhusu mwili wa binadamu kuwa na ming’emenyo inayotengeneza kilevi mwilini, basi angalau 0.005 itafaa kwa nchi.

Inapofikia hatua ya Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani kufikiria hivyo, ni ishara kwamba nafasi ya kilevi katika kusababisha ajali nchini bado ipo kwa kiwango kisichofaa.

Lakini hoja kama hiyo ipo pia kwa mukhtadha wa athari za kiuchumi, ambapo Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Magonjwa ya Ajali wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Dk. Kennedy Nchimbi, anasema matibabu ya mifupa kwa majeruhi wa ajali zikiwamo zilizosababishwa na ulevi, yanagharimu fedha nyingi zinazoweza kuelekezwa kwa huduma nyingine za kijamii.

Dk. Nchimbi anatoa mfano kuwa, chuma kimoja kinachowekwa kwenye eneo la mfupa unaovunjika hasa kwenye ajali, kinagharimu Sh. milioni mbili wakati matibabu yake yanagharimu Shilingi laki tatu.

Hata hivyo, Dk. Nchimbi anasema gharama za chuma hazifahamiki kwa watu wengi kwamba zinatolewa kwa msaada wa watu wa Marekani, ndio maana kiasi cha Sh. laki tatu pekee kinatozwa kwa majeruhi hao.

Ni kwa mifano hiyo michache inatoa taswira kwamba umefika wakati wa kila mwenye dhamana ya udhibiti wa ajali za barabarani, kusimama, kupaza sauti na kuhakikisha anachangia kwa namna yoyote, kutokemeza ajali na kuifanya Tanzania mahali salama kwa usafiri na usafirishaji.