Mabaraza ya Ardhi Kata yaboreshwe

10May 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabaraza ya Ardhi Kata yaboreshwe

MABARAZA la Ardhi ya Kata yalianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kesi au mashauri yanayohusu migogoro ya ardhi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji au mitaa yanapatiwa utatuzi wa kisheria katika ngazi za chini. Hiyo ni kwa kuzingatia sheria na kanuni ziheshimu mipaka yake kiutendaji.

Kimsingi, lengo la kuanzishwa mabaraza hayo lilikuwa sahihi, lakini mifumo iliyowekwa ya upatikanaji wa viongozi wanaoendesha mabaraza hayo, imeonekana kukosa nguvu hivi sasa, katika wakati huu dunia inapogeuka kuwa kijiji.

Watu wengi wana wana ufahamu mkubwa wa sheria, hivyo wanatambua haki zao au hata mipaka ya mamlaka mbalimbali za kisheria.

Mabaraza hayo yalianzishwa mwaka 1985 kwa Sheria ya Bunge Namba Saba, wakizingatia kwamba migogoro mingi ya ardhi ipo katika ngazi za chini, ambako wananchi wengi wanaishi au kuendesha shughuli zao ndogo zinazowapatia vipato, zikiwamo biashara, kilimo na ufugaji.

Kwa maana hiyo, chombo hicho katika hatua hiyo, kingesaidia kupatikana ufumbuzi wa kisheria na kupunguza wingi wa kesi kama hizo, kwenye ngazi za wilaya, mkoa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Nadhani umefika wakati kwa serikali kuangalia uwezekano wa mabaraza hayo kuongozwa na watalaam wenye weledi mkubwa wa sheria.

Hivi sasa, wenyekiti wa mabaraza wanaweza kuwa watu maarufu wakati makatibu kwenye baadhi ya kata, ni maofisa wasio na weledi katika eneo hilo la kitaaluma.

Kwa sasa, kwenye baadhi ya kata, makatibu ni Maofisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata, ndio wameteuliwa kuongoza. Ni mfumo ambao sidhani unafaa kuendelea.

Ikumbukwe kuwa, sheria iliyounda Mabaraza ya Kata imeweka ukomo wa mashauri ya kusikilizwa katika ngazi hiyo, ikiwa na thamani ya shauri linalopokelewa na kusikilizwa hapo. Viongozi wanaweza kujibebesha majukumu wasiyoyastahili kisheria.

Wadau, wanapaswa waishauri serikali ibadilishe mfumo wa viongozi wa mabaraza hayo, ili halmashauri za miji na wilaya ziweke utaratibu wa kuyasimamia moja kwa moja, kwa kuteua wanasheria kutoka halmashauri na makatibu wakawa wajumbe wenye elimu, angalau astashahada ya sheria. Kumekuwapo migogoro kwenye baadhi ya Mabaraza ya Ardhi Kata, katika maeneo mengi nchini.

Mmoja wa wadau, Oliver Limwagu, anakumbusha wakati fulani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitishia kufuta mabaraza hayo mkoani mwake, baada ya kugundua kuwa ni vyanzo vikubwa vya migogoro.

"Wakati mwingine baadhi ya viongozi wamejikuta wakikwaruzana na wateja, kwa sababu mmoja kati ya washitakiwa au walalamikaji wanatoa siri wakati mashauri yakiendelea, jambo ambalo limekuwa likizalisha migogoro pia," anasema Limwagu.

Anasema, mabaraza ya viongozi wasio na weledi kuna wakati yanajikuta yakishughulikia mashauri yasiyowahusu kisheria, ikiwamo migogoro ya ardhi inayosajiliwa au thamani yake inazidi Sh. milioni tatu.

"Yanapojitokeza mazingira kama hayo, sijui kama uwepo wa mabaraza una maana na endapo hali itaendelea hivyo, kuna hatari kubwa ya kuibua migogoro mikubwa zaidi katika siku zijazo, hasa kutokana na ardhi kupanda thamani kila kukicha, huku mabaraza yakiwa hayatambui.

“Mahakama ni kama familia zetu, mume, mke na watoto wana mipaka yao. Kwa nini Mabaraza ya Kata yasiwe na mipaka kiutendaji?” anahoji.

Wakili Godfrey Francis, anasema mazingira ya mwaka 1985 kuanzishwa Mabaraza ya Kata, yaikuwa sahihi, lakini muda uliopo uana sura ya kupitwa na wakati. Mfumo wa uendeshwaji wake, usimamizi na utoaji haki, unapaswa kuboreshwa.

"Ikumbukwe kuwa, kubadilishwa mfumo wa uendeshwaji wa Mabaraza ya Kata, hauwezi kubadilishwa kisiasa kupitia matamko ya viongozi wa kisiasa majukwaani, bali kufanyia marekebisho Sheria ya Mabaraza ya Kata (Amendment)," anasema Francis

Ushauri wake ni sheria iruhusu wenyeviti wa Mabaraza ya Kata, wawe wataalamu wa sheria, kama wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya walivyo, ni wanasheria kwa taaluma. Anahoji kwanini kwenye kata wasiwe wanasheria?

"Sheria iruhusu uwakilishi wa mawakili kwenye kata kama kwenye mahakama za mwanzo wanataka waruhusu mawakili basi na kwenye mabaraza ya kata ni wakati muafaka umefika mawakili waruhusiwe ili matatizo yanayojitokeza sasa hivi ya sijitokeze tena," anasema.

Anasema hivi sasa, Mabaraza ya Kata yapo chini ya usimamizi wa halmashauri na kwamba huo ni mgongano, akitoa mfano, kesi inayoanzia Baraza la Kata, inaweza kupingwa maamuzi yake na kujikuta jalada limefika Mahakama Kuu, ambayo haipo chini ya usimamizi wa halmashauri.

Mdau mwingine, Esha Dismas, mtaalamu na Mshauri wa Sheria Vijijini, anakiri muundo wa sasa wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata, umepitwa na wakati na njia pekee ni kuyafanyia mabadiliko.