Mabasi ya shule yakaguliwe kuwalinda watoto na ajali

14May 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Mabasi ya shule yakaguliwe kuwalinda watoto na ajali

HATA kama nchi itakuwa na wakaguzi wengi wa mabasi ya shule haitakuwa na maana kama wenye mabasi hayo na madereva watakosa maadili na ubinadamu wa kuwathamini na kuwapenda watoto.

Katika suala la kuwasafirisha watoto kwa kutumia usafiri wa mabasi, kuna mambo kadhaa ya kuzingatia, moja wapo ni chombo chenyewe kinachotumika kubeba watoto hao.

Jambo la pili ni madereva wanaotumika kuwachukua watoto hao kama wana vigezo vya kuaminiwa kuwachukua watoto hao na jambo la tatu ni wakaguzi wa magari hayo wawe na maadili kwa kuzingatia sheria na miiko bila kushawishiwa kutenda kitu chochote kinyume na hayo.

Wazazi wanapoamua kuamini usafiri wa shule kuchukua watoto wao, hata wamiliki wa shule pia wanatakiwa kuonyesha uaminifu huo kwa kuzingatia maadili ya usafirishaji.

Shule nyingi zimekuwa zikiwatoza wazazi fedha za usafiri wa watoto wao kwenda shule na kurudi nyumbani ili kuwapunguzia kazi wazazi hao kuwapeleka na kuwarudisha.

Hata hivyo, baadhi ya shule zinazotoa huduma za usafiri kwa watoto, mabasi yao huwa chakavu kiasi cha kuhatarisha usalama wao.

Pamoja na shule nyingi kutumia magari ya kukodi ambayo madereva wake huajiriwa na mmiliki wa gari, wamiliki wa shule wanapaswa kuwakagua kabla ya kuwapa jukumu la kuwabeba wanafunzi wake.

Wazazi wanaamini kuwa watoto wao wanapochukuliwa na mabasi ya shule wanakuwa kwenye mikono salama, hivyo wamiliki pia wanatakiwa kuhakikisha jukumu la wanafunzi kuchukuliwa na kurudishwa nyumbani salama ni la kwao.

Suala la kutanguliza fedha kuliko uhai wa mtu, limesababisha maisha ya watu wengi kupotea kutokana na uzembe.

Kuna matukio kadhaa yamewahi kutokea ya usafiri wa mabasi ya shule kuhatarisha maisha ya watoto, likiwamo la gari moja aina ya Noah kukutwa likiwa limerundika wanafunzi hadi kukosa pumzi.

Usalama wa wanafunzi hao wanapokuwa barabarani pia si salama kutokana na mwendo wa madereva wanaowabeba kuwa wa kasi.

Madereva hao hawajali kuwa wamebeba wanafunzi, wanayapita magari mengine bila kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kuhatarisha maisha ya watoto hao.

Baadhi ya mabasi ya wanafunzi hao, hayana hata michoro au alama zinazo tahadharisha kuwa yamebeba wanafunzi ili hata magari yanayopishana nayo yaweze kuwa na tahadhari.

Shule nyingine zinakuwa na wanafunzi wengi na mabasi machache, lakini kwa sababu ya kutaka kuingiza fedha nyingi za usafiri, zimeendelea kupokea fedha za wazazi na matokeo yake wakati wa kusafirisha wanafunzi hao huwazungusha ruti ndefu.

Mtoto anaweza kuchukuliwa nyumbani saa 11 alfajiri na kufika shule saa mbili asubuhi akiwa amechoka kwa usingizi.

Vivyo hivyo wakati wa kurudishwa nyumbani, atachukuliwa saa 10 alasiri na kufika nyumbani saa 12 hadi saa moja jioni kutokana na mzunguko wa kuwateremsha watoto wengine.

Mtoto huyo kwa uchovu wa mzunguko, ukizingatia basi lenyewe chakavu na barabara mbovu anakuwa hoi, hata muda wa kujisomea nyumbani anakosa.

Pamoja na kwamba baadhi ya shule hazina mabasi yanayoyamiliki, hata yale wanayoamua kuingia nayo mkataba, wahakikishe yako katika hali nzuri badala ya kuangalia gharama.

Mabasi mengi yanayobeba wanafunzi, baada ya kazi hiyo, hugeuka magari ya kusanya abiria ili dereva aweze kupata hela yake.

Baadhi ya madereva wanapojiona wamechoka kwa kufanyakazi usiku, huamua kuwapa `deiwaka’ kuwachukua wanafunzi ambao wengi wao hawana leseni za udereva.

Kuna kila sababu ya wamiliki wa shule wanaotoa usafiri wa wanafunzi, kuchunguza magari na madereva wanaochukua wanafunzi wao.

Ndiyo maana baadhi ya wazazi huamua kujitoa wenyewe kuwapeleka watoto wao kuepuka matatizo kama hayo.

Usalama wa watoto ni wa kila mtu aliyepewa jukumu la kuwaangalia, kuanzia walimu, madereva, wazazi, askari wa usalama barabarani na wananchi wote kwa ujumla.

Kila mtu anayegundua basi lililochukua watoto haliko kawaida, ana wajibu wa kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe mara moja. Mabasi mengi yameandikwa namba za simu nyuma, ili mtu aweze kutoa taarifa iwapo dereva ataonekana anaendesha mwendo usiofaa.

Mawasiliano: [email protected], 0774 466 571.