Mabegi yanabeba vitu vya kihalifu, tuchukue tahadhari

06Jan 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Mabegi yanabeba vitu vya kihalifu, tuchukue tahadhari

MOJA ya mtindo ambao sasa umezuka kwa vijana wa mijini na hasa jijini Dar es Salaam, wakiwamo wanafunzi ni wa kubeba mabegi mgongoni wakiwa wameweka vitu mbalimbali.

Wanafunzi mara kwa mara huweka daftari na vifaa vingine vya shule katika mabegi hayo.

Lakini pia wapo vijana wanaoitwa 'mabishoo', ambao hutumia mabegi kubeba kompyuta mpakato, vitana, simu na vitu vingine.

Katika makundi hayo ya vijana, wapo wanaobeba mabegi kwa sababu za msingi ambazo haziepukiki kama hao wanafunzi wanaoweka madaftari, vitabu ama kompyuta mpakato na vitu vingine muhimu.

Lakini pia wapo vijana wanaobeba mabegi kwa kuiga tu, huku wakiwa hawana vitu vya kuweka humo ndani zaidi vitana na vingine vya kawaida, ili mradi wawe na mabegi mgongoni kwa vile ni fasheni.

Sasa vijana wanaovaa mabegi wamekuwa wakisumbuana na makondakta, kwa madai kwamba wanapanda wakiwa wameyabeba mgongoni na kusababisha abiria wengine kukosa nafasi ndani ya daladala.

Hata hivyo zimeanza kuwapo fununu kwamba wapo baadhi ya vijana wanaotumia mabegi kubebea vitu vya wizi ama vitu vya kufanyia vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya watu wamekuwa wakisema kuwa katika mazingira haya ambayo inaonekana ubebaji huo ni fasheni, ndiyo ambao wajanja wachache wanautumia kubebea vitu visivyo vya halali na fanyia hatari kwa jamii.

Kwa hali ilivyo sasa, siyo rahisi kumtambua mwanafunzi ama mtu mwingine wa kawaida, au aliye hatari kwa jamii, zaidi ya kufanya ukaguzi katika mabegi.

Kama nilivyosema hapo juu, hii ni kwa sababu imekuwa ni jambo la kawaida kila kijana kubeba begi mgongoni.

Sasa kwa sababu inaonekana kwamba ni fasheni, imekuja haina budi kuchangamkiwa na wengi.

Na ndiyo maana katika mazingira haya ndipo ninapoona kuna ulazima wa kuwa na namna nzuri ya kubaini watu wabaya wanaobeba vitu vya wizi ama kuficha silaha kwenye mabegi yao ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidai kwamba hata vijana wahuni wamekuwa wakibeba mabegi kwani wanajua hakuna wa kuwauliza kwa vile vijana kubeba mabegi mgongoni kwa sasa ni kitu cha kawaida.

Kuna mtu mmoja aliwahi kutoa tahadhari kuwa wakati umefika pale mtu unapoambiwa umsaidie mtu kubeba begi lake hata kama ni ndugu yako, uhakikishe unajua kilichomo ndani, usije ukajikuta mikononi mwa vyombo vya dola.

Alisema na kufafanua kuwa waliwahi kumkamata kijana akiwa na begi mgongoni wakati wa usiku na walipompekua wakakuta kuna kisu, vipande vya nondo, nyembe na mifuko laini ya kuvaa usoni ili asitambuliwe anapofanya tukio la uhalifu.

Kijana huyo kukutwa na vifaa hivyo ni dalili tosha kwamba fasheni hii ya vijana wa shule kuvaa mabegi mgongoni, imeingiliwa na watu wasio wema ambao wanaitumia kufanikisha mambo yao haramu.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wahuni kujichanganya ili waonekane ni watu wema na kumbe wana lengo la kufanikisha vitendo vya uhalifu kama hivyo vya kuwaibia raia wema mali zao.

Kwa mfano uliwahi kuibuka mtindo wa watu kubeba mabegi madogo mkononi, baadaye wahuni nao wakaiga wakawa wanasimama kwenye vituo vya daladala kana kwamba wanasubiri usafiri na kumbe wanatafuta njia za kuwaibia abiria.

Walikuwa wakisimama katika vituo kwa muda mrefu, bila kupanda magari na mwisho wa siku wakimuona mtu anashangaashangaa wanamwibia pesa kwenye pochi ama mfukoni.

Maana yake ni kwamba, watu wa aina hiyo wamekuwa wakivizia kila fasheni inayobuniwa kama wanaona inaweza kuwa na manufaa kwao, nao wanajichanganya humo ili waonekane kama raia wema.

Matukio ya uhalifu kwa kutumia mabegi yanayovaliwa mgongoni hayajashamiri, lakini ipo haja ya kutoa tahadhari na ikiwezekana watu wanaotiliwa mashaka wawe wanakaguliwa ili kujua kile ambacho kimo katika mabegi yao.