Mabeki wa pembeni Simba chanzo kikuu kipigo Yanga

27Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabeki wa pembeni Simba chanzo kikuu kipigo Yanga

NI kama tayari Yanga wameshaizoea Simba, wameshaisoma udhaifu wao ambao wapinzani wao hawajashtukia, au mpaka sasa hawajui jinsi gani ya kuupatia dawa.

Kwa mara nyingine, Yanga iliondoka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuwaacha wanachama na mashabiki wa Simba wakiwa hawaamini kilichotokea.

Kwa miaka ya hivi karibuni wanachama na mashabiki wa Simba wanaamini kuwa timu yao ni bora zaidi kuliko Yanga, inawezekana ikawa hivyo, lakini kwa mwaka huu wa 2021, Yanga imepata ushindi mara tatu dhidi ya Simba. Kwa mwaka huu, zimeshakutana mara nne, huku zikitarajiwa kukutana tena Desemba 11 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

Zilianza kukutana Januari 13, kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, ikiwa ni fainali ya Kombe la Mapinduzi, na Yanga kulitwaa kombe hilo kwa kuifunga Simba kwenye matuta, baada ya dakika 90 kwenda sare ya bila kufungana. Yanga ilishinda kwa mikwaju 4-3 ya penalti.

Mechi ya pili ilikuwa Julai 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliyokuwa ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu wa 2020/21. Kwenye mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lililofungwa na Zawadi Mauya.

Mara ya tatu ni kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA, Julai 25, Uwanja wa Tanganyika, Simba ikishinda bao 1-0. Mechi ya Jumamosi ilikuwa ni ya nne kwa watani hao msimu huu na ya tatu kwa Yanga kuibuka na ushindi.

Kuna baadhi ya mashabiki wanadai kuwa pengo la Clatous Chama na Luis Miquissone limeonekana na ndilo lililosababisha Simba ifungwe.

Hata hivyo, ukiangalia hata Luis na Chama kabla hawajaondoka, Simba imekuwa ikipata ugumu kuifunga Yanga na hata mechi ya Julai 3 ikifungwa bao 1-0 walikuwapo. Ikumbukwe hata mechi ya Machi 8, mwaka jana, Bernard Morrison akiwa Yanga, Simba ililala bao 1-0, Chama na Luis walikuwapo pia.

Ni ukweli mchungu pia kinachoonekana kuwahangaisha Simba kwenye mechi dhidi ya Yanga ni mabeki wao wa pembeni.

Tayari Yanga wameshagundua kuwa Shomari Kapombe na Mohamed Hussein wanapenda kupanda mbele, lakini kwa siku za karibuni ama wamekuwa wazito kurudi kukaba au hawako kwenye viwango vyao vya kawaida.

Hata sajili za Yanga zinaonekana zaidi kulenga pembeni kwa mawinga wenye mbio, ili kuwahangaisha mabeki wa wapinzani wao.

Ndiyo maana walimsajili Tuisila Kisinda ambaye alikuwa akiwahangaisha sana mabeki wa pembeni wa timu hiyo, hata alipouzwa haraka walimsajili Jesus Moloko kwa kazi hiyo hiyo.

Bado wakamsajili Djuma Shaaban wakiamini atasaidia kumnyanyasa Tshabalala kama alivyofanya wakati akiwa AS Vita Club kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Na kweli, hilo Yanga wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana ukiangalia mpira mingi ya Yanga ilikuwa ikipitia pembeni na kuwa ni ya hatari kubwa. Ukiiangalia sasa Simba ina udhaifu mno kwa mabeki Tshabalala na Kapombe hasa kwenye kukaba kwa siku za karibuni.

Ikumbukwe kuwa Tshabalala kiasili si mzuri sana kukaba, lakini ni mzuri kupandisha mashambulizi, lakini kadri muda unavyozidi kwenda upande wake unaonekana unapitika kirahisi zaidi.

Kapombe naye tangu msimu uliopita hakuwa kwenye kiwango chake cha kawaida, kwa sasa amepungua uwezo na ana makosa mengi sana.

Kwa maana hiyo wamekuwa wakiwapa tabu sana kina Thadeo Lwanga, Paschal Wawa, Joash Onyango na hata alipoingia Kennedy Juma, walilazimika kuwasaidia wenzao, na hata wakifanya hivyo, wanakuwa wakiacha mapengo kati.

Kama Yanga wasingekuwa waoga, kuiogopa Simba na kuamua kushambulia muda wote, kwenye mechi hizi zote wangekuwa wanafunga mabao mengi.

Ukiangalia mechi ya Jumamosi, Yanga walikuwa hawashambulii muda mwingi, lakini wanapoamua kushambulia, wanakuwa hatari zaidi na hawazuiliki hasa wakipitia pembeni. Ashukuriwe Wawa na Kennedy ambao walifanya kazi kubwa mno kuwazuia mastraika wa Yanga, na pia mawinga wao ambao Tshabalala na Kapombe walishindwa kabisa kuwazuia.

Niliona Kocha Mkuu, Didier Gomes akiamua kumtoa Tshabalala na kumwingiza Israel Mwenda ambaye alikuja angalau kuleta uhai na kutuliza mashambulizi.

Hii ni kengele ya hatari kwa benchi ya ufundi la Simba kuwa Yanga wameshagundua udhaifu wa timu yao upo kwenye beki wa kulia na kushoto. Na ndiko wanakotumia zaidi, Simba inakwenda kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy. Wakati tatizo la ufungaji likitafutiwa ufumbuzi, lakini kuna tatizo mama la kuruhusu mashambulizi kirahisi pembeni. Ikumbukwe hata TP Mazembe bao lao lilipitia pembeni. Udhaifu wa Kapombe ulimlazimu Aishi Manula atoke golini.

Inawezekana timu za nje, zisigundue sana udhaifu huo wa Simba kwa sasa au wakachelewa kuugundua, lakini Yanga ndiyo imekuwa ikiutumia hata kama wakiambiwa kesho wanarudiana na Simba.

Desemba 11 timu hizo zinakutana tena, kama Gomes hatotafuta dawa ya Tshabalala na Kapombe, basi wala haitoshangaza Simba ikafungwa kwa mara nyingine tena mechi hiyo.