Mabilioni ya Deci ni jipu lililoiva

28Jan 2016
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabilioni ya Deci ni jipu lililoiva

MWAKA 2009, Serikali ilizima ndoto za Watanzania waliokuwa wamepanda mbegu katika Taasisi ya Development Entrepreneurship Community Initiative (Deci), iliyoonekana kama mkombozi wao kutokana na mavuno mazuri yaliyokuwa yanapatikana baada ya muda mfupi.

Deci iliyokuwa inawajaza wanachama wake ‘mahela’ kwa mtindo wa kupanda na kuvuna, iliwajengea matumaini makubwa lakini mwaka 2009 ilisababisha msononeko ambao haujasahaulika hadi leo.
Hilo lilitokea baada ya Mamlaka ya Masoko ya mitaji na Dhamana nchini (CMSA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kusitisha biashara ya Deci kwa madai kuwa, taasisi hiyo ilikuwa ikiendesha shughuli zake bila leseni wala usajili wa kuendesha biashara hiyo nchini.
Baada ya kusitishwa kwa shughuli hizo, serikali iliwafungulia kesi wakurugenzi wa Deci na Agosti mwaka 2013, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh. milioni 21 vigogo wanne waliothibitika kuwa na makosa.
Kadhalika, mahakama hiyo iliiagiza serikali ifanye mchanganuo wa mali za Deci ambazo inazishikilia, kwa kuwa zipo mali zilishikiliwa zisizo za kampuni hiyo bali za watu wengine zikiwamo fedha Sh. bilioni 19 ambazo ni mbegu za wanachama ziliamuriwa zirejeshwe kwa wenye nazo.
Hata hivyo, kwa masikitiko makubwa, ni kama serikali ilipuuza agizo la Mahakama ,kwani hadi sasa fedha hizo hawajakabidhiwa wanachama.
Pamoja na kwamba mimi siyo mmoja wa wenye mbegu hizo, lakini ni vyema umma ukaelezwa zilipo fedha hizo kwa sababu inawezekana wajanja wachache wameshazipiga.
Hii ni kwa sababu mara kadhaa, gazeti hili limefuatilia kujua ziliko fedha hizo, pamoja na riba; na majibu ya serikali yalikuwa ni kwamba ziko salama na wakati wowote zingelipwa.

Mara kadhaa, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alieleza kuwa, fedha hizo zimehifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kwamba kilichokuwa kinafanyika ni uchambuzi wa kina ili kila mwanachama apate haki yake.
Sasa najiuliza, ni uchambuzi gani tangu mwaka 2013 hadi sasa? Je, hili sio jipu?
Sh. bilioni 19 ni fedha nyingi ambazo zingeweza kufanya jambo kubwa nchini, kama serikali imeamua kuzitaifisha, basi zipangiwe bajeti ijulikane kabisa kwamba fedha hizo zimeelekezwa kwenye barabara, zahanati, dawa au kilimo; kuliko kuendelea kukaa kimya.
Napendekeza kuwa ,serikali ya awamu ya Tano itumbue jipu hili, kisha itengeneze namna ya kusaidia watu wa kipato cha chini kwani wengi waliojikita Deci ni wajasiriamali wadogo wadogo.
Ni wakati muafaka sasa kwa wataalamu wetu kutafakari namna ya kuwasaidia wananchi wa chini, kwani wengi wana uchu na maendeleo na wakiwezeshwa watafanikiwa na nchi itapiga hatua kiuchumi.
Nasema hivi kwa sababu, hata sasa kuna utitiri mkubwa wa vikundi vya kusaidiana, kuweka na kukopa na upatu; ambavyo baadhi havijasajiliwa na vinaendeshwa bila utaalam. Hii yote ni kwa sababu wananchi wanatafuta njia ya kujikwamua kiuchumi.