Mabinti sasa wanafanya vizuri shuleni, tukune vichwa wavuke

21Jan 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabinti sasa wanafanya vizuri shuleni, tukune vichwa wavuke

KWANZA ni siku chache zilizopita, nitamke kwa furaha kwamba mabinti wanatuwakilisha vyema kwa kung’arisha jina na jinsia yetu wanafanya vyema katika mitihani ya kidato cha nne.

Nikirejea hoja yangu ya msingi, ni vyema inapokuwa walimu wanapeana mikakati pasipo kujali shule wanazofundisha, wanaweza kuleta ufaulu mkubwa katika matokeo ya darasa la saba, kidato cha pili, cha nne na sita.

Shule nyingi zinazofaulisha wanafunzi wake, mara zote wanakwambia mikakati waliyojiwekea ndio hiyo iliyozaa matunda ya ufaulu.

Hivyo inafaa walimu mjiangalie katika shule mtokazo kinachotakiwa ni kuwa na umoja wa kuibua mikakati itakayosaidia kuwafaulisha wanafunzi wenu.

Hivi karibuni katika semina za jinsia na maendeleo (GDSS), waliandaa mada iliyojadili matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni kwa jicho la kijinsia, mahali pa kusherehekea na pa kujipanga.

Ni busara shule zingejifunza kwa walimu wenzao, mbinu wanazotumia katika shule zao, naamini wanawake wakiwezeshwa kuleta maendeleo au mabadiliko makubwa yanakuja katika sehemu waliopo.

Flora Ndapa, kutoka Asasi ya TGNP Mtandao anasema  kuwa sehemu ya kusherehekea ipo, kutokana na watoto wa kike kufaulu kwa idadi kubwa, pia hata 10 bora watoto wa kike wameingia wanane.

Mama huyo anajinasibu na fahari hiyo akitamka kauli:" Pa kusherehekea papo, ukiangalia jicho la kijinsia, watoto wanane wa kike katika 10 bora wameingia humo.

“Pia wako watoto wa kike, mmoja kutoka mkoani Morogoro na mwingine mkoani Mbeya walipata ujauzito, lakini walirudi shule kufanya mitihani, mmoja kapata daraja la kwanza mwingine daraja la tatu.”

Suleiman Bishagazi, kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, Dar es Salaam, anaeleza kwamba katika kujipanga upya kunatakiwa kuangaliwe ni sababu zipi idadi ya watoto wa kike wanaofanya mtihani wanakuwa wachache, ilhali wenzao wanaume ni wengi.

Bishagazi anaeleza ufanisi ulioko kutoka kwa walimu wa shule za binafsi upo juu, kuliko wenzao wa kutoka shule za serikali kunakotakiwa kuwapo miundombinu wezeshi kwa shule za serikali, anakokutaja kuna changamoto lukuki.

Ufafanuzi wa mama huyo watoto wanaofaulu wanakuwa katika mazingira mazuri ya shule, ikiwamo miundombinu yao.

Ni hoja ya pongezi kwa kinadada hao, wakitamkia kwamba hata nafsi ya shule iliyoongoza mitihani ni ya watoto wa kike na Monica John, mdau kutoka TGNP Mtandao, anasema sehemu ya kujipanga ni kuendelea kuboresha miundombinu.

Anaongeza kuwa shule zinatakiwa kujifunza kutoka kwa shule zingine, pia kuwapo walimu wa saikolojia na mazingira wezeshi kwao.

Nia ninayoiona inaenda mbali katika eneo kama wasio na uwezo darasani wasaidiwe, ili nao waweze kuwafikia kwenye uwezo au hatua kubwa kitaaluma.

Wazo kuu mahali hapo ni kwamba kunapaswa kutolewa motisha stahiki kwa wanafunzi, ikiwamo hatua ya wazazi kushauriana katika mustakabali mpana wa masuala ya ulezi.

Anaongeza kwamba, kuwapo mafunzo maalumu ya walimu ofisini, inakuwa jambo la busara katika kuiwasaidia walimu kuendana na wakati.

Mimrejee Janeth John kutoka Taasisi ya Binti Makini anayesema kuwa tusherehekee ufaulu kwa watoto wa kike katika mitihani ya mwaka jana.

Pia anasema, kujipanga upya ni kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki shuleni.

Anasema shule nyingi ambazo ni binafsi zinazofanya vizuri, zikifuatiliwa kwa kina, idadi kubwa ya wanafunzi wake ni wadogo kiumri, wamejifunza Kiingereza kuanzia madarasa wakati wenzao wanaanzia madarasa ya juu kuanzia darasa la tatu.

Hance Obote anasema mazingira wezeshi  ndio yanayochangia watoto kufanya vizuri katika mitihani yao.

Nimrejee Zuwena Juma, mshiriki wa GDSS anasema motisha ni kichocheo kwa wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.