Mabinti waimarishwe kuepuka mitego ya mafataki

22Sep 2016
Jenifer Julius
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mabinti waimarishwe kuepuka mitego ya mafataki

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme alipokuwa akifungua mafunzo ya walimu watakaosimamia mitihani ya taifa ya darasa la saba,alisema kuwa katika mkoa huo wanafunzi sita walikatisha masomo yao kwa sababu ya kupachikwa ujauzito hivyo hawakupata fursa ya kufanya mtihani wa kuhitimu .

Msimamo huo, ulimaanisha kuwa wanafunzi sita wamepungiziwa fursa za kuendelea na masomo ya sekondari na elimu ya juu baada ya hapo kupitia mfumo rasmi.

Kwa namna yoyote ile, inasikitisha kusikia au kushuhudia ndoto za wanafunzi wa kike zinakatishwa kikatili kabisa kwa sababu ya kupewa ujauzito.

Ndoto za binti wadogo zinakatishwa wakiwa hawajafikia hata robo ya ndoto zao huku watendaji wakiendelea kuwa huru kutimiza malengo yao kama kawaida.

Inasikitisha zaidi kuona baadhi ya wanaume wanachukulia changamoto zinazowakumba wasichana kama njia ya kumaliza haja zao za kimwili kwa gharama ndogo tu ya chips-mayaiau kumpa lifti, bila ya kujali madhara atakayoyapata binti huyo ikiwamo kupata ujauzito au maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo Ukimwi katika umri mdogo ambayo huchangia kukatisha ndoto zao na maisha kwa ujumla.

Licha ya sheria kubainisha adhabu kali kwa mafataki hao ikiwamo kifungo cha miaka 30 jela, bado watu hao hawajabadilisha mienendo yao huku wakiendeleza vitendo hivyo kama kwamba hawaoni vibaya au kuwa na chembe ya utu kwa wasichana na maisha yao kwa ujumla.

Swali kubwa la kujiuliza, inamaana watu hao hawawaoni wanawake wanaolingana nao kiumri hadi kujenga tabia ya kuwafuata watoto wadogo ambao akili zao bado hazijapevuka?

Serikali inapaswa kuchukua hatua za makusudi kabisa za kuhakikisha elimu zaidi inatolewa kwa jamii kubadili mitazamo kwa wasichana hao wadogo na wasichana kuelimishwa namna ya kujilinda na kuepuka mitego ya wanaume ambayo mara nyingi imekuwa ikiwatumbukiza kwenye matatizo matupu.

Ni muhimu pia wazazi kuongea na watoto wao kwa karibu zaidi bila kuchoka kuhusu athari za kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo. Usimuonee mtoto wako haya eti kwa kuwa ni mdogo,kwa kuwa kuna watu huko nje huwaona wakubwa na kupenyeza yao.

Usipomuwahi mapema kumjengea msimamo binti yako ufahamu kuwa, watatokea mafataki kumrubuni na matokeo yake ndio kama haya ya kujikuta maisha yao yakivurugwa hata kushindwa kutumiza ndoto zao na kuchangia ustawi wao, jamii na ukuzaji wa uchumi kwa ujumla