Machinga kuuza panga, upinde, hakuna usalama

28Feb 2020
Sabato Kasika
Nipashe
BUFE
Machinga kuuza panga, upinde, hakuna usalama

NI rasmi marufuku kwa ujasiriamali mitaani kwa nyenzo na silaha hatari kama mapanga, visu, majambia, lakini, ukweli tunaokutana nao mitaani, tangazo na agizo hilo la kiserikali limeingia sikio moja na kutokea lingine.

Hii inatokana na ukweli kwamba hakuna mabadiliko kwa wajasiriamali, mambo ni kama siku zote, wanauza silaha hizo kwenye mkusanyiko wa watu na wengine kuzipanga barabarani.

Lakini, ikumbukwe wakati akiwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alipiga marufuku kwa yeyote au kikundi kuuza mapanga, visu, manati, pinde na mishale barabarani.

Kuchukuliwa hatua hizo, ni kuwakumbusha wauzaji mtu hawezi kufanya biashara hiyo bila ya kuwa na leseni na kwamba hizo ni silaha ambazo jeshi linafahamu vilivyo madhara yake, hivyo ni muhimu wauzaji wafuate taratibu.

Mmachinga anaweza kuuza panga barabarani kwa nia nzuri, lakini kukawapo ugomvi jirani na anapouzia silaha hizo na kujikuta, inaegeuzwa ama kwa hiari au nia tofauti watu wanamnyang'anya na kuzitumia kusababisha madhara makubwa.

Baadaye Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alipokuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, naye alipiga marufuku biashara hiyo, lakini kama nilivyosema, bado silaha zimeendelea kuuzwa kama kawaida.

Mbaya zaidi, zinauzwa kwenye mkusanyiko wa watu wa aina mbalimbali, hali inayoonekana kuwa ya kawaida sana, kumbe ni hatari dhahiri. Hivyo, kuna haja ya kuchukuliwa hatua kabla madhara kutokea.

Uuzaji silaha kwenye mkusanyiko wa watu mbalimbali, daima siyo salama. Ni kwa sababu, hata wasiokuwa na akili timamu nao wamo na wanaweza kuzitumia kuwadhuru wengine.

Matukio ya kutumika silaha kuumiza au kuua watu wengine, yanaweza kutokea katika mazingira popote, lakini kuuza silaha hizo kwenye mkusanyiko wa watu, madhara yake yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Ninasema hivyo, kwa sababu watu wanaweza kuhoji mbona tindikali haiuzwi madukani, lakini watu wanamwagiwa, au kwamba kupiga marufuku uuzaji wa silaha hizo kwenye mkusanyiko hakuwezi kuzuia madhara.

Inawezekana hilo likawa na ukweli. Tusimame katika usemi, kinga ni bora kuliko tiba. Kwanini kusubiri hadi madhara yatokee, ndipo hatua zichukuliwe?

Kwa kuwa Jeshi la Polisi lilishapiga marufuku, basi kinachotakiwa sasa ni hatua ya utekelezaji wake.

Ikumbukwe, katika mkusanyiko huo, mtu anaweza kuchukua kisu kinachouza au panga na kujeruhi wengine, hapa muuzaji na aliyeumiza wengine atachukuliwa hatua za kisheria.

Hivyo, sioni kwanini wauzaji wanashindwa kutambua madhara ambayo wanaweza kusababisha na badala yake wanaendelea kufanya biashara hiyo kwenye mkusanyiko kama kawaida.

Nakumbuka kuna wakati katika marufuku ya Kamanda Kova, alisema jeshi lipo katika mchakato wa kupendekeza sheria mpya ya matumizi ya silaha na umiliki, ili kudhibiti matumizi mabaya, yakiwamo uuzaji wake holela.

Ni vyema, vijana wanaojishughulisha na umachinga wakauza vingine kama nguo na viatu, kuliko hayo ya silaha ambazo zimezuiwa kuuzwa kiholela.

Vinginevyo, wanaweza kujikuta wakasababisha madhara makubwa bila wao kutarajia na hawawezi kujitetea, kwa sababu tayari Polisi lilishapiga marufuku, lakini bahati mbaya wauzaji na hata wanunuzi wamekuwa wagumu kuelewa.

Wanachokifanya baadhi ya Machinga kwa sasa, ni kwamba wameshasikia marufuku hiyo ya serikali ikaingia katika sikio moja na kutokea lingine, hali inayosababisha waendelee na ubishi kung’ang’ania biashara hiyo.

Uuzaji holela wa panga, visu, jambia na silaha nyinginezo za jadi katika maeneo ya mjini kama Dar es Salaam, unaibua hofu kwa wengine, hivyo ni vyema ikaachwa.

Wakati mwingine, mtu anaweza kukuta Machinga wanavizia foleni za magari na kwenda kutafuta wateja ambao ni abiria. Ni utaratibu usio salama kwa watu wote. Hapo polisi ikaingilia kati kupiga marufuku.