Machinga wasaidiwe kuepuka janga hili

08Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Machinga wasaidiwe kuepuka janga hili

WAFANYABIASHARA wadogo, maarufu kwa jina la Machinga wanafanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali, huku mamlaka husika zikiwatafutia sehemu rasmi za biashara.

Ni sehemu wanazotakiwa kufanyia biashara zao katika masoko yaliyotengwa na manispaa au halmashauri, lakini zikiwa na huduma zote za msingi kuanzia maji, vyoo, usafiri na nyingine.

Ingawa agizo la kuboresha masoko yao ni la muda mrefu, inawezekana halijafanyika na ndiyo maana wameendelea kuwapo kando ya barabara wakiuza bidhaa zao kama kawaida.

Pamoja na kuruhusiwa kufanya biashara za katika maeneo mbalimbali na hasa kando ya barabara kama nilivyosema, angalizo kubwa ni kuhakikisha hawachafui mazingira ya maeneo yanayofanyia biashara.

Hata hivyo, angalizo linaonekana kuwa gumu kwa baadhi yao, kutokana na jinsi wanavyoendelea kuchafua mazingira kana kwamba ni jambo la kawaida kwao kukaa katika uchafu.

Mfano mmojawapo, ni wamchinga walioko eneo la Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, ambako hivi sasa wameamua kupanga vitu vyao hadi katika mitaro na wengine kuweka mbao juu ya mitaro hiyo na kupanga biashara.

Kimsingi ni kwamba, serikali kwa kiasi kikubwa inaboresha miundombinu ya barabara jijini, ikiwamo mitaro ya kupitisha maji ya mvua, ili yasisambae mitaani na kuleta usumbufu kwa watu.

Pamoja na juhudi hizo, huenda miundombinu hiyo ikaharibika kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kugeuza sehemu hizo za kupanga bidhaa wakisubiri wateja.

Mtindo huo nimeushuhudia eneo la Mbezi Mwisho kwa wachuuzi, wakiwamo wanaouza matunda, mboga na bidhaa nyinginezo. Wanazipanga ndani ya mitaro na muda wa kufanya biashara unapoisha, huacha taka zao mitaroni.

Kwa hali kama hiyo, ni wazi kwamba huenda ikasababisha mitaro ikaziba na kusababisha uchafuzi wa mazingira na hivyo kuwa kero kwa wengine.

Maendeleo ni muhimu kwa binadamu yoyote, lakini maisha bora hayawezi kufikiwa iwapo watu hawatakuwa na utamaduni wa kukitunza kilichopo kama, ambavyo wafanyabiashara hao wadogo wamekuwa wakifanya.

Serikali inapanua Barabara ya Morogoro, ili kupunguza foleni za magari, lakini sasa mitaro ya barabara hiyo imegeuzwa sehemu ya kupanga biashara, ambayo si salama kabisa.

Nitamke, wamachinga hawabaguliwi na ndiyo maana serikali ikaandaa vitambulisho na kuwagawia, kwa sababu inatambua shughuli zao kwenye jamii. Lakini, niwasahauri kwamba, nao wanapaswa kufika mahali wanazingatia maelekezo kwa kutochafua mazingira.

Jambo wanalotakiwa kulishika sana, ni kwamba wakati wakijengewa mazingira bora ya kufanya biashara, ni muhimu wakazingatia usafi wa mazingira, kuliko kuendelea na hali ya sasa.

Binafsi, siamini kwamba maeneo ya biashara yameisha hadi waamue kupanga bidhaa zao ndani ya mitaro, au waweke mtaroni na kupanga bidhaa.

Nadhani kuna tatizo mahali fulani, waelekezwe ili waache mtindo huo. Wapo wanaopanga bidhaa hadi kwenye hifadhi ya barabara, hali ambayo ni hatari kwa usalama na vyema wakaacha kufanya hivyo, ili kuepuka ajali za barabarani.

Ni muhimu kwa mikoa na halmashauri zote, nikiamini kila mahali waendelee kutimiza malengo ya kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo, kwa kutenga maeneo rasmi ya biashara.

Pia wasichague mazingira na wakati huohuo ni faida kwao ya kupuke ajali dhidi yao.

Kimsingi, Machinga hawapaswi kubughudhiwa bali kutengewa maeneo na suala hilo lilikwisha kuagizwa na Rais John Magufuli, kwamba halmashauri zote zifanye hivyo, ili wapate maeneo ya uhakika kufanyia biashara.

Wakati wakisubiri hilo, basi ni muhimu wazingatie usalama wao, pamoja na usafi wa mazingira kwa kutopanga bidhaa zao kando ya barabara na ndani ya mitaro.

Wengine huziba hata njia za waendao kwa miguu na kusababisha usumbufu, na kama nilivyosema, siamini kwamba wanakosa sehemu hadi wafanye hivyo.

Sababu inayoelezwa na baadhi yao hadi kufikia hatua hiyo, ni kutaka kupanga bidhaa mbele ya wengine, hadi wanaangukia kuiweka mitaroni, ili wawahi kupata wateja wengi na kwa haraka zaidi.

Imani ya aina hiyo ni kwamba, wakipanga biashara mbele kwa kuweka hadi mitaroni, ni namna ya kuwapata wateja wengi. Hilo halifai kabisa. Wanatakiwa kutambua kuwa hata wakiwa nyuma ya wateja, bado watawafuata huko huko waliko.