Madereva wa daladala tuheshimu miundombinu

05Jan 2018
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Madereva wa daladala tuheshimu miundombinu

MADEREVA kulikoni kupitisha magari katika matuta? Serikali imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kuboresha miundombinu yake lengo, ni kuifanya iwe na mwonekano mzuri na ulio bora.

Lakini, pamoja na jitihada hizo za serikali, kuna baadhi ya madereva ambao hawathamini jitihada hizo na kuamua kuvunja sheria za usalama barabarani.

 

Tunapozungumzia suala zima la usalama barabarani, tunaelewa kuwa kila mmoja wetu anatakiwa kuzifuata sheria hizo, ili asije kuzivunja na kuchukuliwa hatua.

 

Lakini ni ubishi wa baadhi ya madereva kuvunja kwa sheria ni kitu cha kawaida katika maisha yao kutokana na kujijengea kuwa hakuna mtu ambaye anawafuatilia.

 

Hiyo inawezakana, labda kuwapo na idadi ndogo ya polisi wa usalama wa barabarani, kunasababisha maeneo ambayo hawafiki, madereva wanatumia mwanya huo kuvunja sheria za usalama barabarani.

 

Tumekuwa tukiona katika vyombo vya habari hata matangazo kuwa uvunjaji wa sheria barabarani ni kosa na faini yake haipungui kiasi cha

Shilingi elfu 30,000.

 

Lakini kwa nini tuvunje sharia, ili tulipe faini hiyo? Hizo fedha tunazotaka kuzilipa katika faini za kujitakia. Kwa nini zisitumike katika kutuongezea vipato?

 

Sasa nianze na hili la madereva wa kituo cha mabasi cha Gerezani – Kariakoo.

 

Hicho kituo kimejengwa na kimetumia mabilioni ya fedha mpaka

kuanza kufanya kazi, lakini leo hii ukiona baadhi ya Watanzania wenzetu wasio na huruma, wameanza kuharibu miundombinu yake kwa

makusudi.

 

Unakuta gari linatoka Tandika, Mbagala, Gongo la Mboto, badala ya kuzunguka ukuta ili kuingia katika foleni yake, lakini unakuta madereva hao wanaupanda ukuta, ili kuwahi abiria.

 

Sasa tujiulize, hivi hao walioweka ukuta na kuwataka muuzunguke hawakuwa na akili?

 

Yaani unaona dereva wa daladala anatoka na spidi yake huko, anapita katika ukuta na anauharibu kabisa, lakini hilo halioni. Yeye anawahi kuchukua abiria.

 

Kuna haja katika vituo  vilivyotengenezwa, kuwapo polisi jamii wapambane na madereva hao walio wenye tabia mbaya katika maendeleo ya taifa.

 

Ukija katika Barabara ya Kilwa katika maeneo ya Mbagala, napo madereva wa daladala wamekuwa wakipanda ukuta kupitisha magari yao, bila ya kuwa na woga kuwa huenda gari hilo likaanguka kutokana na kuyumba.

 

Kwa madereva wa bodaboda, nao wanaharibu miundombinu kwa kupita katika maeneo ya mabasi ya mwendokasi, ambako hawaruhusiwi kupita.

 

Unakuta bodaboda inapita katika miundombinu ya mwendokasi tena akiwa kapakia abiria bila ya kuwa na woga wamba, anaweza kumwangusha abiria huyo.

 

Kuna kila sababu hata sisi abiria kuwa na sauti katika hivi vyombo na kama tutaendelea kukaa kimya siku ajali itakapokukuta ndio utajua

kukaa kimya sio ishu.

 

Unakuta mtu kapakiwa katika bodaboda, tena wapo mishkaki, anapita katika maeneo ya hatari ambayo mabasi ya mwendokasi yanapita anakaa kimya hashtuki, siku akipata ajali ndio atajua ni muhimu kutoa neno pale unapoona hauridhiki na uvunjwaji wa sheria unaofanywa na madereva wa bodaboda au daladala.

 

Tukumbuke kuwa ajali ikitokea, kuna mambo matatu yanayoweza kutokea,

mojawapo ni kufa, pili ni kupata ulemavu wa kudumu la tatu ni kuchubuka.

 

Sasa upate bahati uchubuke, lakini usife au kupata ulemavu wa kudumu.

 

Pia, tukumbuke hivyo vyombo hata kama vitakusababishia ajali, huwezi kupata msaada wowote wa kulipwa bima kutokana na vingi kutokuwa na bima na vinaendeshwa kiwiziwizi.

 

Kama hukubaliani na hilo, pata ajali kutoka katika hivyo vyombo uone

kama utalipwa na bima.