Madhara ya kutomaliza dozi ya dawa-2

07Feb 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Madhara ya kutomaliza dozi ya dawa-2

Katika sehemu ya kwanza Jumapili iliyopita, tuliona madhara ya kutomaliza dozi ya dawa ambazo mgonjwa ameandikiwa na daktari na kupewa kwenye dirisha la dawa.

Tulijifunza kuwa kuna bakteria wa aina tatu, kuanzia wale ambao ni wadhaifu katika kupambana na dawa husika mpaka walio na uwezo mkubwa wa kustahimili nguvu ya dawa. Hivyo kitendo chochote cha kutomaliza dozi kinafanya baketeria hasa walio sugu wajenge usugu zaidi wa dawa ambayo dozi yake imekatishwa na kuiondolea uwezo wa kutibu mgonjwa husika...

UMUHIMU WA KUMALIZA DOZI
Katika hali ya kawaida, endapo mgonjwa ameanza kumeza dawa na kutokatisha dozi basi hata wale bakteria sugu hushindwa kustahimili ile sumu ya dawa na hivyo baada ya muda huangamia wote na kuacha mwili ukiwa salama. Ni lazima kuhakikisha kuwa mgonjwa anamaliza dozi kila mara.
Zifuatazo ni sababu nne za kwanini ni muhimu kumaliza dozi uliyoandikiwa na daktari.
1. Unapositisha kumalizia dozi kabla ya muda uliopangiwa na daktari kuisha, bakteria waliopo mwilini mwako wana uwezo wa kukua tena na katika kasi kubwa zaidi. Bakteria hao wana uwezo wa kuzaliana na kusababisha upya dalili za awali za ugonjwa husika.

2. Unapotumia dawa ya kuua bakteria (antibiotic) mwilini, kunatokea mpambano kati ya ile sumu ya dawa na bakteria waliosababisha ugonjwa husika. Wakati wa mpambano baina ya dawa na bakteria, bakteria hujaribu kujibadili waweze kusalimika dhidi ya sumu ya ile dawa kwahiyo endapo mgonjwa atakatisha dozi bakteria kadhaa watasalia mwilini na hawa ni wale ambao walishapambana na dawa na kupona. Bakteria hawa watakuwa wameshajitengenezea namna ya kupambana na dawa husika kwahiyo kuweza kusafirisha uwezo huu wa kuhimili dawa kwa bakteria wengine watakaozaliwa. Iwapo mtu huyu ataugua na kutumia dawa hiyo hiyo, bakteria alionao wanakuwa wameshakuwa sugu dhidi ya dawa husika na hivyo kutoathirika kabisa na dawa.

3. Katika harakati za kupambana na bakteria wa ugonjwa, lazima kuhakikisha kuwa vijidudu vyote vimeuwawa na kwisha kabisa mwilini kwa kumaliza dozi. Iwapo mgonjwa hatamaliza dozi bakteria hao watajitokeza tena na kwa wakati huu wa pili wanakuwa ni hatari zaidi ya awali.

4. Njia kubwa ya kuwafanya bakteria kuwa sugu wa dawa ni kuwatibu pasipo kumaliza muda wa matibabu (kukatisha dozi). Kinachotokea ni kwamba, bakteria hawa wanapozaliana hujibadili vinasaba (DNA) na kujiweka sugu wa dawa. Kwa hiyo mtu aliekatisha dozi huishia kuwa muhifadhi wa bakteria wasiosikia kabisa dawa hali ambayo ni hatari sana kiafya.

Yafuatayo ni mambo machache unayoweza kufanya ya kakusaidia kukumbuka kutumia dawa na hatimaye kumaliza dozi.
1. Kama unadhani kuwa wewe ni msahaulifu na usiyependa kumeza dawa za muda mrefu, basi zungumza na daktari wako akuandikie dawa ambazo utapaswa kumeza mara moja au mbili kwa siku.
2. Beba dawa zako katika mkoba asubuhi ili usiache kumeza wakati unapofika; pindi unapokuwa mbali na nyumbani
3. Chora ratiba maalumu ya kumeza dawa na uiweke mahali panapoonekana ikiwa ni nyumbani au sehemu ya kazi, ili ukumbuke kumeza dawa pindi utakapoiona ratiba.

Simu: 0784 86 56 16