Madudu haya elimu yasiwe sikio la kufa lisilosikia dawa

24Nov 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Madudu haya elimu yasiwe sikio la kufa lisilosikia dawa

WALIMU wakuu wa shule za msingi kadhaa wanatuhumiwa kufanya udanganyifu kwenye mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi na kusababisha wanafunzi 1,059 kufutiwa matokeo ya mtihani huo.

Mbali na walimu hao wa shule 38, watuhumiwa wengine wa udanganyifu ni walimu wa taaluma, mgambo na wasimamizi ambao waliandaa vikundi vilivyohusisha wahitimu wa sekondari, waliowafanyia mtihani.

Hiyo ni kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, kwamba baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa wakiwamo 11 kutoka Halmashauri ya Gairo na 12 wa Mvomero mkoani Morogoro.

Watuhumiwa wengine ni 13 wa shule tatu tofauti kutoka Bariadi mkoani Simiyu, huku Halmashauri ya Sikonge mkoani Tabora wakiwamo 11 na Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro wapo watano.

Aidha, jijini Arusha wamenaswa watano, Halmashauri ya Tandahimba mkoani Mtwara saba, na ya Kiteto huko Manyara ni wanne na Buchosa mkoani Mwanza Katibu Mkuu anasema wamenaswa watatu.

Wakati hayo yakiwa yamejiri kwenye mtihani wa darasa la saba, Dk. Msonde, anasema katika mtihani wa kidato cha nne ulioanza jana, wamebaini shule 71 ambazo ziko katika mchakato wa kufanya udanganyifu.

Ikumbukwe kuwa si mara ya kwanza kuwapo kwa maonyo na hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa kwenye udanganyifu wa mitihani kwa shule za msingi na sekondari.

Serikali imekuwa ikionya na kukemea mtindo huo wa udanganyifu na wizi kwenye mitihani kuanzia ngazi ya shule za msingi na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaobainika kujihusisha na mchezo huo.

Mwaka 2014, NECTA ilitangazia umma kuwa imedhibiti wizi wa mitihani ya taifa na udanganyifu katika ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Mafanikio hayo yanatajwa kuwa yanatokana na ushirikiano uliopo kati ya NECTA na kamati za uendeshaji mitihani za mikoa na wilaya, ili kutatua tatizo la wizi wa mitihani ya taifa na udanganyifu.

Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa NECTA, Daniel Mafie, ndiye aliyetoa taarifa katika mkutano na wanahabari kuelezea mafanikio yaliyokuwa yamefikiwa na baraza hilo wakati huo.

Lakini, ajabu ni kwamba bado madudu yanaendelea kujitokeza kila mwaka, hali inayoonyesha kuwa wanaojihusisha udanganyifu huo wamekuwa ni sawa na sikio la kufa ambalo halisikii dawa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa madudu kwenye mtihani wa taifa ni ya muda mrefu ya miaka nenda rudi ingawa serikali inajitahidi kupambana nayo, lakini bado yanaendelea kujitokeza kila mwaka.

Mfano mmojawapo ni matokeo ya mwaka 2011 ya mtihani wa darasa la saba, watahiniwa 9,736 walifutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu, huku mwaka 2013, 272 wa kidato cha nne nao wakifutiwa kwa kosa hilo.

Ni vyema kukumbushana kuwa, udanganyifu katika mitihani una mchango wa kuporomosha elimu hivyo wahusika wanatakiwa kulitambua hilo na kuachana nalo.

Udanganyifu na wizi wa mitihani huzalisha wasomi wasio na manufaa kwa taifa, hivyo upigwe vita na wadau wa elimu na pia wahusika waendelee kuchukuliwa hatua za kisheria.

Haipendezi kufaulu kwa udanganyifu na kuchaguliwa kwenda shule ya vipaji maalum wakati hana sifa jambo linaloweza kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.

Wanaofanya mchezo huo huenda wanafahamu madhara yanayotokana na udanganyifu huo, hivyo ni vyema kuachana na mambo hayo yasiyo na tija kwa taifa.

Watambue kuwa, udanganyifu na wizi wa mitihani ni vitendo vyenye athari kuanzia kwa wanafunzi, walimu shule na taifa kwani ni kukwamisha hatima ya elimu.

Inasikitisha kuona wenye wajibu wa kusimamia kanuni na weledi katika mitihani, ndiyo wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo viovu badala ya kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi wanabomoa.

Yaliyopita si ndwele waliopewa dhamana hiyo wabadilike ingawa inawezekana wachache ndiyo wanaowaharibia wenzao, lakini suala la msingi ni kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za kusimamia mitihani kwa weledi.