Maeneo ya kuwekeza fedha zako

10Jun 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Maeneo ya kuwekeza fedha zako

WIKI iliyopita tuliangalia kanuni tatu muhimu za fedha, ambazo mfanyabiashara wa ngazi yoyote ile ama mtu mwingine, anapaswa azitumie ili maisha yake ya kifedha yaweze kumnyookea.

Kwanza ni ile ya kulipwa kulingana na thamani ya kile ambacho mfanyabishara ama mtu yeyote anazalisha ama kuingiza sokoni.

Kwamba utatengeneza fedha iwapo utawekeza vya kutosha kulingana na thamani ya shughuli yako ya kiuchumi, iwe kazi ama biashara.

Kanuni ya pili tuliyoiona ni ya kuhifadhi ama kutunza fedha baada ya kuwa umezitengeneza.

Kwamba badala ya kukimbilia kuzitumia bila mpangilio maalumu, kwa mfano kwa kununua vitu ambavyo siyo muhimu, unapaswa uzitunze kwanza, kwa muda fulani.

Kwamba atumie muda huo wa kuzitunza kwa kutakafari kwa kina, namna atavyozitumia kwa ustawi zaidi wa kazi ama biashara yake.

Na kanuni ya tatu tuliyoiona ni ile ya kuifanya sasa fedha hiyo ikuzalishie zaidi kwa kuiwekeza kwenye maeneo yanayolipa.

Kwa maana hiyo, mtu anapaswa kuwa mwangalifu katika kufanya uchaguzi wa wapi unataka kwenda kuwekeza, kitu ambacho ndiyo mada yetu ya leo.

Kuna maeneo mengi yenye tija ambayo mtu anaweza kupeleka fedha zake, ili yamzalishie zaidi.

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuongeza mtaji kwenye biashara uliyonayo na hivyo kuifanya ipanuke na kutengeneza faida zaidi.

Eneo lingine unaloweza kuwekeza na ukawa na uhakika wa faida, ni lile la mali zisizohamishika kwa maana ya ardhi kama vile ujenzi wa nyumba.

Lakini vilevile katika siku za karibuni, kumeibuka eneo la uwekezaji lenye uhakika, na waliobahatika kulitambua kabla na kuitumia fursa hiyo kikamilifu, wamefaidika sana na wanaendelea kufaidika kila siku.

Nalo ni la kuwekeza kwenye masoko ya fedha kwa njia mbalimbali.

Katika hili mfanyabiashara anaweza akanunua hisa kutoka kwenye makampuni yaliyojisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Ni juu ya mfanyabiashara ama mtu kupata taarifa sahihi ya kampuni zinazofanya vizuri zaidi na kununua hisa zake.
Hii ni njia ya uhakika ya kutunza fedha na kupata faida kwa sababu mfanyabiashara atakuwa na uhakika na usalama wa fedha yake, lakini pia atapata faida kupitia gawio la hisa zake.

Lakini kwenye masoko ya fedha, kuna fursa pia ya kununua dhamana ama hati fungani zilizoko sokoni kwa hivi sasa.
Kwa mfano serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inauza hatifungani ama dhamana za serikali za muda mfupi, na za muda mrefu.

Mwekezaji hapa atakuwa na uhakika wa usalama wa fedha zake, lakini na faida itokanayo na riba inayolipwa.

Ukiachana na dhamana za serikali, kuna makampuni binafsi ambayo sasa yameruhusiwa kuingiza hati fungani zao, mfano benki ya NMB.

Ni muhimu ukazingatia kuwa, sehemu unayoweka fedha yako, ina faida zaidi.
Nasema hivyo kwa sababu, kuna sehemu ambazo watu hufikiri wamewekeza, lakini ukweli wanapoteza fedha zao.

Baadhi ya sehemu hizo ni pamoja na kuweka fedha benki ukiamini unapata riba, kununua vitu vya matumizi kama magari ya kutembelea, ukiamini kwamba ukiwa na magari mengi ya kutembelea ni mali zinazokuzalishia, kumbe patupu.
Ni bora basi ukachagua maeneo salama na yenye faida ya kutosha kama niliyoyaeleza hapo juu, kwa ustawi wako.