Magufuli alivyozibeba Simba, Namungo michuano ya CAF

11Jan 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Magufuli alivyozibeba Simba, Namungo michuano ya CAF

NI ukweli usipingika kabisa kuwa uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuruhusu michezo kuendelea wakati nchi zingine zikiwa zimejifungia ndani kutokana na janga la ugonjwa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, pia umechangia kufanya vema kwa timu za ....

Tanzania, Simba na Namungo kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.

Simba imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuzitoa timu ngumu za Plateau United ya Nigeria kwa bao 1-0 na FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 4-1.

Timu ya Namungo FC ambayo inaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, nayo imetinga raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuziondoa Al Rabita ya Sudan Kusini kwenye mechi ya awali na kwenye raundi ya kwanza iliichapa Al Hilal Obeid ya Sudan kwa jumla ya mabao 5-3, ikishinda 2-0 nyumbani na kutoka sare ya mabao 3-3 ugenini.

Mei mwaka jana, Rais Magufuli, pamoja na mambo mengine, aliruhusu kuendelea kwa michezo yote, ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ni nchi pekee kama si chache Afrika kuendelea na ligi.

Kitendo cha kuendelea na michezo kimeonekana kuleta faida kubwa, kwani ushindi wa timu zote za Simba na Namungo, pamoja na mipango ya viongozi na mabenchi ya ufundi, uwezo wa wachezaji, lakini kuna ukweli kuwa timu nyingi bado haziko fiti sana kutokana na nchi zao kukaa muda mrefu bila kucheza soka.

Wakati nchi zingine zikianza kuruhusu soka kuchezwa na Shirikisho la Soka Afrika kuruhusu kuanza kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho, wachezaji wanaocheza Ligi Tanzania imewakuta wako fiti kimwili kutokana na wao waliendelea kucheza, huku wachezaji wa timu nyingi za nje pamoja na uwezo wao, lakini walionekana kukosa utimamu wa mwili kutokana na kukaa muda mrefu na bado hawajaanza kuchanganya.

Timu za Tanzania zinaweza kuendelea kuipata faida hii kwenye mechi zinazofuata, kwani wakati wachezaji wa timu zingine wakianza kuchanganya, tayari wanaocheza soka Tanzania watakuwa mbali sana.

Simba imepangwa Kundi A, ikiwa na timu za AS Vita ya Congo DR, mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri na Al Merreikh ya Sudan.

Imepangwa kwenye kundi lenye timu ambazo ilikuwa nazo mwaka 2019, kasoro JS Saoura ya Algeria ambayo imeipisha Al Merreik. Kuna baadhi ya mashabiki wanaona kama itakuwa ngumu mno kwa Simba kupenya kwenye kundi hilo, lakini kama itakuwa imejizatiti inaweza kutinga hatu ya robo fainali kama ilivyofanya mwaka 2019. Tena inaweza kuwa ni rahisi zaidi kwao kwa sababu safari hii itakuwa inacheza ugenini kukiwa hakuna mashabiki, huku Tanzania yenyewe ikiruhusiwa kuingiza asilimia 30 ya mashabiki uwanjani.

Rais Magufuli aliwaambia wananchi waendelee na shughuli zao, badala yake wamuombe mwenyezi Mungu kuiondoshea nchi ugonjwa huu na kwa kiasi kikubwa imefanikiwa, na imekuwa faida kubwa hata kwenye michezo.

Tumeona Simba ikicheza Nigeria na Zimbabwe viwanja vikiwa na watu wachache sana, na hiyo ikiendelea itakuwa faida kwa wawakilishi hao wa Tanzania na sidhani kama wanaweza kufungwa tena mabao matano ugenini.

Wakati Simba ikicheza raha mustarehe ugenini, hapa nyumbani timu za ugenini zinakutana na mashabiki wanaoruhusiwa kuingia uwanjani, hivyo kuwa na wakati mgumu mno.

Namungo ambayo pia imenufaika na hilo, nayo pia itapambana na Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola kwenye mechi ambayo kama ikishinda itakuwa imetinga kwenye hatua ya makundi ya shirikisho.

Wawakilishi wa Tanzania, Simba na Namungo, zinaweza kuishangaza Afrika mwaka huu kwa kufika mbali kwenye michuano hiyo, mbali na sababu za kiufundi, lakini uamuzi wa Rais Magufuli kuruhusu michezo kuendelea, lakini mashabiki kuruhusiwa viwanjani kuzishangilia timu hizo, wakati kwao kwa sasa hakuna vitu kama hivyo, na kuzifanya mechi zao za nyumbani zisiwe tishio sana kwa timu za Tanzania.