Magufuli piga kazi waachie Kiingereza chao

14Feb 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Magufuli piga kazi waachie Kiingereza chao

“NIMEFANYA PhD (shahada ya uzamivu) bado wanasema sijui Kiingereza, na nikaka mwaka mzima Uingereza, sijui nilikuwa nazungumza Kisukuma kule! Wakasema sijui Kiingereza, niliamua kuzungumza Kiswahili na kuki-promote (kukitangaza), kwa sababu ni lugha iliyoachwa na Baba wa Taifa.”

Hiyo ni kauli ya Rais John Magufuli alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Miaka 100 ya Mahakama Tanzania, alipokuwa akishajihisha umuhimu wa Kiswahili kutumiwa mahakamani, hususan katika uandishi wa mwenendo wa kesi na hukumu.

Si ma raya kwanza Rais analalamika dhidi ya wanaomzushia kuwa haujui Kingereza, eti kwa sababu tu hakitumii kwenye shughuli zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na hotuba. Mimi ningemwomba Rais awapuuze wanaomlaumu kwa hilo.

Kabla sijasema nalotaka kulisema hapa, natangaza maslahi binafsi kwake kwamba mbali na kuwa ni Rais wangu na mwanachama mwenzangu, nimesoma naye darasa moja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hivyo namfahamu.

Miongoni mwa waliokuwa marafiki zake name najigamba kuwa mmoja wao na hataalipokuwa ameingia kwenye siasa na mpaka kuwa Waziri na sasa ni Rais, ameendelea kuwa rafiki yangu, kwa sababu madaraka si ukuta wa kutuzuia. Hivyo namfahamu fika.

Namfahamu alivyo nguli katika kuzungumza lugha mbalimbali, zikiwamo za makabila ya ndani ya nchi, nikiwa na uhakika kabisa wa Kisukuma, Kihaya, Kisubi na hata Kikerewe na ndiyo sababu baadhi ya marafiki zake walikuwa wa makabila hayo.

Tukiwa pamoja UDSM, tulishiriki naye semina za kimasomo darasani, ambazo ziliendeshwa kwa Kiingereza na hata kufanikiwa kumaliza masomo yetu ya Shahada ya Kwanza mwaka 1988 bila‘ kuvutwa shati’ wala ‘kudisco’. Mitihani yote ikifanywa kwa Kiingereza.

Akasoma Shahada ya Uzamili kwa Kiingereza, ya Uzamivu kwa Kiingereza, akafundisha sekondari kwa Kiingereza, amekuwa mbunge, naibu waziri na waziri, kote huko akiwasiliana kwa Kiingereza kimaandishi na kimazungumzo. Vivyo hivyo kwenye urais.

Sasa kaugua ugonjwa gani Yarabi, hivyo sasa asiweze kuwasiliana kwa Kiingereza? Au yeye kutaka kuimarisha na kukienzi Kiswahili ni dhambi? Rais anayeongoza Watanzania ambao asilimia kubwa ni Waswahili atakiwe kuzungumza Kiingereza? Kinatusaidia nini Watanzania?

Kama ilikuwa lazima tuwe na Rais wa aina hiyo, basi ni vyema tukachaguliwa Rais na Waingereza na atoke London. Nadhani Watanzania tufike mahali hata kama tu wapinzani, kukumbatia masuala yenye uzito na umuhimu kwa jamii, kuliko haya madogo yasiyo na tija.

Tunaona serikali yake inayoyafanya, kwa sababu reli ya kisasa haijengwi kwa Kiingereza, Bwawa la Umeme la JK Nyerere halijengwi kwa Kiingereza, si hospitali, zahanati wala vituo vya afya.

Hivi siku Rais Magufuli akiamua kuitisha mkutano wa hadharaa kazungumza Kiingereza mwanzo mwisho, atasemwaje? Hawatasema amedharau Kiswahili wakati anazungumza na Watanzania?

 Wanaotaka Rais wa Kiingereza wasubiri muhula huu wa mwisho wa miaka mitano uishe ili tuone kama kweli Watanzania watataka Mwingereza awaongoze ili awe anawasiliana nao kwa Kiingereza.

Tumwache Rais ajenge nchi, tumpe ushirikiano atuokoe na magumu tunayopitia ili ifike siku Waingereza nao watuone tunastahili kujivunia Kiswahili, ambacho ndicho kinachotuletea maendeleo tunayoyashuhudia hivi sasa. Dk. Magufuli piga kazi tuko nyuma yako.

Kuna usemi wa Kifaransa, kwamba ‘Le chien a bois la caravan e passe (kubwe ka kwa mbwa hakuzuii lori kupita). Waingereza- Wabongo endeleeni na Kiingereza chenu. Alamsiki!