Magufuli 'vimemo' vya CCM visikuzuie kutumbua majipu

02Mar 2016
Leonce Zimbandu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Magufuli 'vimemo' vya CCM visikuzuie kutumbua majipu

JUNI, mwaka huu rais John Magufuli anatarajia kukabidhiwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa kama mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.

Wakati Dk Magufuli akikabidhiwa ramsi chama hicho, kuna haja ya kushauri kiundani kwamba ajitahidi asiwe kama waliomtangulia.

Miaka 20 iliyopita naweza kusema CCM ilisahau sana shida za Watanzania na matokeo yake kila mtu aliyaona hususani ulipofika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kundi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira lilikuwa na chuki na chama hicho pamoja na serikali yao.
Chuki hiyo ilisababisha ushindani mkali wa kisiasa pale CCM ilipokabiliana na Ukawa.

Binafsi naunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa ukusanyaji mapato na kuchukua hatua kwa viongozi ambao wameshindwa kutekeleza wajibu wao na kuisababishia serikali hasara.

Hatua hizo zimewafanya wananchi kujenga imani kwa rais Magufuli kwa kuwa ameanza kuimarisha mfumo wa uwajibikaji.

Baada ya rais Magufuli kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na kukabidhiwa Ilani, wananchi hao wanadai itakuwa vigumu kuendeleza kasi hiyo ya utumbuaji majipu.

Kama kweli misingi ya CCM ni kulindana, kuoneana aibu na kuogopana, hilo litaonekana dhahiri.
Katika hili wananchi wanahitaji kupata taarifa za uchunguzi za wakurugenzi waliosimamishwa taasisi mbali mbali za serikali ili kujua hatua zitakazochukuliwa dhidi yao.

Baadhi ya vigogo walioshindwa kutekeleza wajibu wao ni pamoja na wakurugenzi wanne wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) na vigogo wawili wa shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Februari 16, mwaka huu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kuwasimamisha kazi mara moja wakurugenzi wanne wa taasisi hiyo kutokana na tuhuma matumizi mabaya ya Sh bilioni 1.5.

Wakati huo waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akichukua hatua hiyo, naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye aliwasimamisha kazi vigogo wawili, akiwamo Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Matukio wa TBC Mbwilo Kitujime.

Mwingine ni Meneja wa Vipindi wa shirika hilo, Edna Rajab na kuagiza kufumuliwa kwa Idara ya habari na matukio ya TBC kutokana na utendaji usioridhisha.

Hatua hizo za kusimamisha viongozi wa taasisi za serikali zimeongeza ufanisi kwa watendaji kutekeleza wajibu wao.
Ili kudumisha nidhamu kazini huo siyo jukumu la rais Magufuli pekee bali inapaswa kujenga misingi ya uwajibikaji katika sekta za umma na binafsi kwa kila mmoja kuwajibika na kuleta mabadiliko.

Hali hiyo italeta heshima kwa watumishi kufanyakazi kwa bidii na kuepuka ofisi za umma zisigeuzwe kuwa vijiwe kama ilivyokuwa awali wakati watumishi walipokuwa wakiingia kazini kusaini, kupiga soga na wengine kwenda kunywa pombe.
Lakini tangu kasi ya utumbuaji majipu ianze tumeshuhudia hata wahudumu katika Hospitali jijini Dar es Salaam wanafanyakazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa vizuri.

Hivyo naiomba serikali isibadili msimamo wake wa kurudisha heshima ya uwajibikaji kazini kwa watendaji wa sekta za umma.

Naamini heka heka iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano kusafisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imejenga heshima ya kukusanya mapato na kukuza uchumi.