Maji haya ya mvua yaanze kutunufaisha

11Jun 2019
Gaudensia Mngumi
Nipashe
Mjadala
Maji haya ya mvua yaanze kutunufaisha

KWA wakazi wa Dar es Salaam na ukanda wa mzima wa pwani  kinachoonekana sasa ni upepo ambao  licha ya kuleta magonjwa, kama  vikohozi na matatizo ya macho, kwa upande mwingine hutishia maisha kwa kuvunja miti na kuezua mapaa.

Habari mbaya inayoambatana na upepo huo ni kukausha maji kwenye vyanzo mbalimbali, kukausha ardhi na mazao pia. Upepo huo unatokea huo unaanza kuvuruga hali ya hewa, wiki tatu baada ya mvua kubwa kunyesha sehemu mbalimbali nchini.

Ni jambo la kusikitisha kuwa baada  ya mvua kujaza madimbwi, mito, mikondo ya maji, maziwa na vyanzo mbalimbali kwa mwezi mzima wa tano,  kinachojiri sasa ni ukame na ukosefu wa maji kwenye baadhi ya mikoa utakapovuma na wananchi wengi kuendelea kuteseka. Wataendelea kutegemea maji ya madimbwi, visima vifupi na hata kunywa maji ya chumvi.

Ukipita maeneo mengi ya Dar es Salaam na mikoa ya pwani na mikoa yenye upepo, utakubaliana na wataalamu kuwa muda huu haukuwa wa kuhangaika na maji kwani wananchi walitakiwa kufunzwa namna ya kuvuna maji ya mvua ambayo sasa yangekuwa yanatumika.

Kwa jinsi jitihada zinavyofanyika kusaidia kupata maji kutoka vyanzo mbalimbali, taifa halina budi kuanza mpango kabambe wa kujenga miundombinu ya kukusanya maji ya mvua na kuweka akiba ya maji hayo, yatakayotumika kwa muda mrefu.

Jitihada zinazofanywa kuwa na akiba ya chakula , ni vyema pia kuwa na akiba ya maji . Kwa kila kijiji, wilaya na mikoa. Chanzo cha akiba hiyo ni maji ya mvua.

Kwa jinsi ambavyo taifa linajitahidi kujenga miundombinu ya usafiri, shule na  hospitali ni wakati pia wa kuanza kuweka mikakati ya kujenga miundombinu ya kuhifadhi maji ya mvua ambayo ni jambo la kuhuzunisha kuwa karibu yote  hupotea na kuacha nchi na wakati kama yangevunwa watu wasingekuwa na shida ya maji.

Kama ambavyo juhudi zinafanywa kufikisha mawasiliano ya simu mijini na  vijijini , kadhalika kuwafikishia wananchi umeme wa jua na wa gridi ya taifa , vivyo hivyo kuna haja ya kuandaa mikakati ili kuwawezesha kuvuna maji ya mvua.

FAIDA ZAKE

Maji ya mvua hayana gharama yanaanguka juu ya mapaa hivyo ni rahisi kuyakusanya kwani hayatumii nguvu wala mbinu za kitaalamu au za kiuhandisi.  Ni salama kwa vile hayana  magonjwa, uchafu wala vimelea kama vile ambavyo vinapatikana kutoka kwenye maji ya ardhini.

Kwa upande wa mazingira maji ya mvua ni muhimu kwenye kupunguza uwezekano wa mafuriko unaoumiza wananchi wengi mijini na vijijini.

Ikumbukwe kila mwaka Juni 9, ni Siku ya Mazingira Duniani , taifa linapoadhimisha siku ya mazingira duniani ni vyema pia kuangalia jinsi kama nchi inavyoweza kunufaika na  kuvuna maji ya mvua yanayotiririka pembeni ya barabara, kwenye mito, mabondeni na kwenye mikondo  ili kutunza mazingira.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASA) inastahili pongezi kwa kujenga mradi wa bwawa la Kidunda mkoani Morogoro ambao pamoja na mambo mengi utahifadhi akiba kubwa ya maji ya mvua yatakayotumika jijini Dar es Salaam na mkoa na miji ya Bagamoyo, Mlandizi na Kibaha. Hili  ni jambo linaloweza kuigwa na mamlaka nyingine zikiwamo za mabonde.

Kwa mfano Mamlaka  za  Kuendeleza Mabonde la  Mto  Rufiji Bonde la Mto  Pangani, Wami –Ruvu, Bonde la Ziwa Victoria, Mto  Ruvuma na Ziwa Tanganyika kujaribu uwekezaji kwenye kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ili kusaidia kupunguza matatizo ya maji.

Ni dhahiri kuwa huenda kama maji ya mvua yangevunwa kwenye mabonde mbalimbali miji inayotishiwa na mafuriko kama Dar es Salaam ingekuwa salama wakati wa masika, lakini kila mwaka tatizo hilo hutishia maisha japo ufumbuzi wake unaweza pengine kupatikana kupitia uvunaji huo.

Kuvuna maji hayo kuna faida kwani kunapunguza ongezeka wa kuwa na makorongo makubwa, kuongezeka ukubwa wa mito, na kupanuka mikondo ya maji mijini na vijijini na kwa ujumla kunasaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira kunakotokana na maji ya mafuriko.

UVUNAJI NYUMBANI

Kuvuna maji ya mvua nyumbani yanayokusanywa kwenye mabati ya mapaa na kuingizwa kwenye visima vya familia ni njia mojawapo ya kusaidia kupunguza gharama za maji.

Gharama hizo hupungua si kwa familia pekee bali hata kampuni za majitaka na majisafi mijini kukiwa na maji hayo ya ziada hupunguziwa gharama za uendeshaji.

Gharama hizo ni kama kununua  kemikali za kusafisha maji, kutumia umeme kuyasukuma  na kuyafikisha kwenye vituo vilivyoko maeneo  mbalimbali mijini kabla ya kuwafikishia wateja.

Faida nyingine nyingi hupatikana kwa watumiaji wa nyumbani ambao watatumia maji hayo kwenye kilimo, ufugaji na shughuli nyingine nyingi za nyumbani. Ni vyema kujaribu sasa. Kama kuna nia na njia itapatikana.