Maji umbali usiozidi mita 400, unapunguza ukatili kijinsia

06Aug 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maji umbali usiozidi mita 400, unapunguza ukatili kijinsia

SERA ya Maji ya Mwaka 1991, ililenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2000, wananchi wote wawe wamekwishapata majisafi na salama, kwa kiwango cha kikidhi mahitaji yao.

Maji yalitakiwa yapatikane umbali usiozidi mita 400 ifikapo mwaka 2002, ili kuwaondolea usumbufu wa kupata huduma hiyo, kwa kutembea umbali mrefu ambao wakati mwingine si salama kwao.

Hata hivyo, lengo la sera hiyo bado halijatimia hasa kwenye baadhi ya vijiji, hali inayosababisha wanawake na wasichana kutembea umbali mrefu, kufuata huduma hiyo muhimu.

Pamoja na juhudi za serikali kuwapatia wananchi maji, kuna dokezo la kiuchambuzi kwamba, sera ilitajwa kuwa na upungufu wake, ikiwamo kutokushirikisha sekta binafsi na wananchi wakati wa kuipanga, kutekeleza na usimamizi wake vijijini.

Mengine yanahusu uwekaji msisitizo katika usambazaji, kuliko utunzaji, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali maji katika maisha ya binadamu, hali kadhalika kukosekana mikakati mahsusi ya kuitekeleza.

Kutokana na hali hiyo, serikali iliandaa sera nyingine mwaka 2002 iliyozingatia kuziba mianya ya upungufu uliojitokeza katika sera ya awali, lengo ni kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wingi.

Taarifa za Wizara ya Maji inaeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kumaliza kero zinazojitokeza, ikiwamo watumiaji kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Mtazamo uliomo katika mkakati huo, unaelezwa kuwa muhimu zaidi katika upatikanaji maji kwa wingi, jambo linaloelezwa litasaidia kuwanusuru kinamama na mabinti ambao ndio waathirika wa kwanza.

Inapotokea maboresho katika eneo hilo, ina maana ya faraja kubwa, kundi hilo kuwa mbali na hatari ya kukumbwa na ukatili wa kijinsia, pindi wanapotembea umbali mrefu kufuata maji.

Uzoefu unaonyesha kwamba kundi hilo la wanajamiii pindi wanapotembea umbali mrefu kufuata maji, kuna wakati wanapita katika mazingira hatari rahisi kukumbana na ukatili kama ubakaji na kuhatarisha maisha yao.

Hivyo, juhudi zinahitajika kuhakikisha maji yanapatikana nchi nzima katika umbali uliopendekezwa na sera, chini ya mita 400. Hapo inabeba maana kwamba, kinahakikishwa usalama wa afya za wanawake na wasichana kuliko walivyo sasa.

Tunafahamu kuwapo juhudi mbalimbali zinachukuliwa na serikali kuhakikisha maji yanapatikana, ikiwamo kuanzisha Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (Ruwasa), kasi ya usambazaji huo iongezwe.

Upatikanaji maji katika maeneo jirani na wananchi, utasaidia kuwaondolea hatari ya kukumbana na vitendo vya ukatili, hasa kutokana na ukweli kwamba dunia ya leo, baadhi ya binadamu hawana huruma.

Hapo RUWASA wana wajibu wa kusanifu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maji vijijini, kutafiti yanayohusu maji ardhini, kuchimba visima na ujenzi wa mabwawa, kusajili na kuviwezesha vyombo vya watumiaji maji vijijini.

Vilevile, kuna jukumu la kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya maji vijijini na kumshauri Waziri wa Maji, yanayohusu uendeshaji sekta ya maji vijijini, kwamba yafanyike kwa ufanisi ili kuharakisha upatikanaji wake.
Kwa wanaoishi vijijini watakuwa wanaelewa vyema wanachokieleza, kwani upatikanaji maji kwenye maeneo yao bado ni tatizo linalohitaji kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kukosa maji katika baadhi ya maeneo ya vijijini na mijini unaibua wadau wa kutetea haki za wanawake na wasichana, kukihimizwa haja ya bajeti yake kuwa na mrengo wa kijinsia.

Huduma ya maji inahitaji bajeti ya mrengo wa kijinsia, kwa vile wenye jukumu la kuchota maji katika familia ni wanawake, hivyo maji yanapopatikana katika maeneo karibu ni nafuu kwao.

Ofisa Habari wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Monica John, anaunga mkono kwamba asasi yao inaamini kukiwapo bajeti ya aina hiyo inayowagusa wanawake, ni ishara ya ukombozi kwao.

Ukweli unaotawala ni kwamba, katika harakati yoyote ya kusaka maji ya kutumia, mzigo mkubwa unawaangukia kinamama, wanaogawanyika katika makusudi makuu mawili ya wasichana na watu wazima, wote wanatembea umbali mrefu kufuatilia na ndipo inajenga hoja ya sasa yapatikane jirani, umbali usiozidi mita 400.