Makocha Warundi wawazindue Wabongo

13Nov 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Makocha Warundi wawazindue Wabongo

NADHANI si watu wengi waliogundua kitu kinachoendelea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.

Wapenzi wengi wa soka bado wako kwenye kubishana wachezaji Kelvin Yondani na Papy Tshishimbi walishika mpira kwenye mechi kati ya Simba na Yanga, hivyo zilikuwa penalti dhahiri.

Wengine pia wako kwenye ubishi wa mchezaji Shiza Kichuya alikuwa ameotea au la kwenye bao alilofunga dhidi ya Mbeya City.

Wakati watu wakijadili kitu ambacho hata wakeshe mwezi wanazungumza, lakini hawatoweza kubadili maamuzi ya matokeo ya mechi ya Simba na Yanga, wala Simba dhidi ya Mbeya City, wanashindwa kung'amua kuwa makocha kutoka nchini Burundi wameanza kumiminika nchini.

Kwa afya ya soka letu la Tanzania, ilibidi hili ndilo lingeng'ang'aniwa zaidi kuzungumzwa na wapenzi wa soka nchini na kutafuta kiini chake ili makocha wetu nao wafuate nyayo zao.

Mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania kuna makocha wanne kutoka nchini Burundi.

Makocha hao ni Ettiene Ndayiragije wa Mbao FC, Nsanzurimo Ramadhani wa Mbeya City, Niyongabo Amas wa Stand United na Masudi Juma wa Simba.

Kati yao, ni Masudi peke yake ndiyo kocha msaidizi, lakini akiwa na hadhi ya kuwa kocha mkuu.

Kuna tetesi kuwa huenda akawa kocha mkuu wakati Mcameroon Joseph Omog atakapomaliza mkataba wake.

Ujio wa makocha hawa wa Kirundi nchini Tanzania haukuja kwa bahati mbaya.

Na huenda mpaka Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakapomalizika tunaweza kushuhudia makocha wengi zaidi ya hawa.
Pia msimu ujao tunaweza kushuhudia idadi kubwa ya makocha kutoka nchini humo.

Kwanza kabisa, binafsi nadhani makocha kutoka nchini Burundi wameanza kuaminiwa na kuajiriwa na klabu za Tanzania kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na kocha wa Mbao FC, Ndayiragije.

Huyu alifanya kazi nzuri mno msimu uliopita, akiisuka timu iliyopandishwa daraja na TFF na kuwa moja ya timu tishio, si kwa klabu za Simba na Yanga tu, bali timu zote za Ligi Kuu ikiwamo kufika fainali ya Kombe la FA na kufungwa kwa tabu na Simba.

Akiwa na wachezaji vijana tu 'wasio na majina', kocha huyo aliwatengeneza na kuwa wachezaji shupavu, wanaocheza soka la nguvu na akili kwa pamoja.

Hata msimu huu, pamoja na kwamba haijafanya vizuri sana, lakini pia haijafanya vibaya sana na pia haijapoteza aina ya uchezaji wao wa msimu uliopita, licha ya kwamba imeondokewa na wachezaji wengi.

Ndayiragije alianza kuhusishwa na kujiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu, baadaye Mbeya City, kisha ikadaiwa angetua Stand United, lakini mwishowe ilidaiwa kuwa Yanga ilikuwa iingie naye mkataba. Lakini hadi leo amebaki Mbao FC, huku timu tatu kati ya hizo zilizomkosa, zikiwa tayari na makocha kutoka Burundi.

Hii inaonyesha kuwa kocha huyo amepalilia njia ya makocha wenzake.

Inaonekana Warundi hawa wamekuwa na uwezo wa kufundisha soka la kisasa na la kutumia nguvu linalochezwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na mazingira ya viwanja vyetu.

Ukiwaangalia makocha hao bado ni vijana, na hii inaonyesha kuwa wenzetu Warundi kwa sasa wameamua kupeleka wachezaji wengi waliostaafu soka kwenda kusomea ukocha.

Nadhani pia wenzetu wanabebwa zaidi na uhusiano mzuri wa watawala wao kabla ya uhuru, Ufaransa ambao wamekuwa na tabia ya kusaidia nchi ilizozitawala kwenye nyanja mbalimbali kama za michezo na utamaduni.

Kwa sasa wameanza kurejea kwao na kutapakaa nchi jirani kama Kenya, Uganda, Tanzania, Djibouti, Sudan Kusini na Rwanda kufundisha timu mbalimbali kwa mafanikio.

Naanza kuiona Burundi ya miaka mitano ijayo kisoka. Tukifanya masihara siyo tu kama itakuwa mbali na sisi kwenye viwango, lakini wanaweza pia kucheza hata AFCON huku sisi tukiwa pale pale kwa miaka yote.

Makocha wa Burundi wamekuwa si waoga, kwani wameanza kuwa na uthubutu wa kuondoka kwao kwenda kutafuta malisho nje ya nchi wakati wa kwetu waking'ang'ana kufundisha klabu za Daraja la Kwanza Tanzania Bara na kuzipandisha, zikishaingia Ligi Kuu wanaachwa au kuwa makocha wasaidizi, halafu wanarudi tena kutafuta timu nyingine za kuzipandisha, wakiogopa kuomba kwenda kufundisha nje ya nchi. Kuzalisha makocha vijana kwa wingi ni moja kati ya njia ya kuinua soka kwenye nchi husika.

Nadhani kwa hili la makocha wa Burundi, kuna cha kujifunza kuanzia kwa serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), makocha wa sasa wa Kitanzania, wachezaji wanaotarajia kustaafu na wanaostaafu, na wapenzi wa soka kuwa hakuna njia ya mkato kwenye soka.