Makufuli chunga ‘wasikuSankare’

14May 2016
Nkwazi Mhango
Nipashe
Hekaya za Mlevi wa Canada
Makufuli chunga ‘wasikuSankare’

WIKI juzi nilipoandika waraka wa kufurahia kutangaza vifo vya mafisadi kuna mafwisadi au makuwadi wao kama kumi na ushei hivi waliniandikia emails za matusi, wasijue nshatukanwa mitusi aina zote na huwa sijali. Naona ni maneno tu.

Hayawezi kuvunja mfupa, tena fupa lenyewe la mlevi aliyezoea kila aina ya sulubu kwenye kaya ya sulubishi.

Hivyo, kunitukana ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Watukane wasitukane, nitaendelea kusherehekea pale mafwisadi yanapopukitika iwe ni kwa presha au ngoma kama si mkono wa Bwana God.

Hata hivyo, sikuwaacha wanaizaya hawa ambao wazazi wao walipata hasara kuzaa mijizi. Niliwaporomoshea mvua na vimbunga vya mitusi tena ya nguoni hadi wakanywea. Sipokei email nyingine za kishenzi na kichovu kama hizo.

Walidhani wanaweza kunitisha fyatu kama mimi wasijue nilishajifia nikingoja kuzikwa hasa usawa huu ambapo mijizi michache inahaha baada ya rais daktari Joni Kanywaji Makufuli, kutema moto si cheche kama tulivyomzoea.

Aliwapa laivu walanguzi na mafisadi wanaoficha sukari ili iadimike walangue huku serikali ikichukiwa.

Alikuwapo pale Katesh alipofyatua kombora lake kuwa wote walioficha shuga wajiandae kunyang’anywa na kuigawa kwa walevi.
Mifisadi hii uchwara imezoea vijiserikali ilivyokuwa inaviweka mifukoni isijue Makufuli ni mtambo mwingine.

Sasa mtakoma na kukomaa kama siyo kunyea debe, kumbafuni zenu mafwisadi wote kayani na wale waliowaendekeza na kuwaabudia wasijue yana mwisho. Yako wapi sasa kumbafuni zenu tena?

Leo naandika waraka mwingine adhimu na muhimu tena kwa mtu muhimu ambao kwa wasiojihangaisha kuangalia mambo kama yalivyo watadhani namuwangia rahis wetu mpendeka anayelenga kuwakomboa walevi na wachovu wote kayani.

Wapo waliodhani hawawezi kutumbuliwa wakaishia kutumbuliwa tena kavu kavu bila kutarajia. Wako wapi sasa? Unafanya mchezo na mimi siyo usijue ulevi wangu si wa hasara bali busara na faida.

Anayedhani najifagilia, ajiulize kama anaweza kuyachora haya ninayoyachora. Au mnataka anitwangie simu au kuniandikia email. Na bado nina mpango wa kuwatumbulisha akina IPTL, UDA na manyang’au wengine ukiachia mbali wale waliokuwa wakiwakingia kifua.

Hata mzee aliyejibinafsishia akiwa Ikulu nitambulisha atake asitake. Hivyo basi, naandika bila woga wala kupinda maneno kumtaka achukue tahadhari na wanaizaya hawa wasijemfanyia kitu mbaya hasa baada ya kuwashika pabaya.

Pamoja na ulevi wangu, bado naikumbuka kuisoma vizuri historia. Narejea mashujaa waliofanyiwa kitu mbaya kama vile rafiki yangu kipenzi Rais Thomas Sankara wa Burkinafasso wanakoishi wa Burkinabe bila kumsahau Waziri Mkuu wa zamani wa Kongo, Patrice Lumumba, waliokatizwa maisha baada ya kukamia kuwakomboa wanyonge hasa walevi toka kwenye mikono michafu ya mafisadi wa kitaifa na kimataifa.

Leo tena bila kupiga mma wala kuvuta bangi nakuja na wosia muhimu kuliko zote na kwa mtu muhimu sana kwa kaya yetu. Napendekeza afanye yafuatayo:

Mosi, anapogundua jipu, atumbue waliotumbuliwa watatoa sauti wenyewe. Asitoe tishio au onyo ambavyo vinaweza kutumiwa na mashetani hawa kumhujumu kwa namna yoyote. Simba mwendapole na mkimya ndiye hula nyama.

Hapa la kufanya si kuyatishia majambazi haya bali kuyapiga marufuku ikiwezekana kuyatupa lupango yakaonje joto ya jiwe na kutumia vyoo vya mtondoo. Asihau kuwa majipu mengine anatembea nayo ila hajayagundua. Kwenye msafara wa kenge mamba wamo.

Pili, kama sukari tajwa, alipaswa kuvamia maghala na kuinyakua na kuigawa kwa walevi badala ya kutangaza ili haya mafisadi yajue kaya hii ina wenyewe na wenyewe ni sisi na si yenyewe kama yalivyozoea.

Tatu, badala ya kuyazodoa na kuyaonya, ilibidi baada ya kukamata sukari na kuyatupa lupango, ayatwange faini wakati yakingoja kesi kamambe ya kuhujumu uchumi.

Nne, akumbuke historia ya mashujaa Sankara na Lumumba, nao walifanya kama yeye wasijue haya majitu hayana utu wala hayathamini uhai. Najua shujaa Sankara alipodedishwa kwa kukataa ufisadi na uombaomba, Dk Kanywaji kama mimi alikuwa shule au jeshini.

Hata hivyo, anajua chanzo na sababu ya ‘kuSankariwa Sankara.’ Najua anaweza kusema yule aliuawa na rafiki yake Blaise Compaore wakati yeye hana rafiki kwenye utawala wake. Mchezo ni ule ule angalia na tahadhari waliokuzunguka ili uchukue tahadhari.

Adui mwingine mkubwa anayemnyemelea Dk Kanywaji si mwingine bali genge lake. Limejaa mijitu yenye roho mbaya na minyama inayoweza kunyotoa mja roho hata kwa kuikosoa.

Just imagine; kama mijitu ilizoea bao la mkono kwenye uongozi na sasa amesababisha mijanja hiyo ikose anategemea impende?

Fikiria huyu anayetishia maslahi yao uchwara ukiachia mbali kutaka kufumua mfumo uliozooza na wa hovyo wa muda mrefu. Kutokana na kukataa uchakachuaji.

Wanaohaha na washitiri wao unadhani wakipata fursa watamfanya nini anayetishia kuwatumbua wakubwa na wadogo katika genge hili? Hamuoni jamaa anavyogwaya kuachia ukiti akiogopa kutumbuliwa. Hata agomee vipi ataachia na kutumbuliwa.