Makundi maalum yajiandae kuelekea 2020

02Mar 2016
Theodatus Muchunguzi
Nipashe
Mjadala
Makundi maalum yajiandae kuelekea 2020

KUNA malalamiko mengi kutoka makundi maalum katika jamii yanayowahusisha wanawake, watu wenye ulemavu na vijana kwamba hawatendewi haki wakati wa uchaguzi.

Malalamiko hayo yamekuwapo muda mrefu Tanzania Bara na Zanzibar. Malalamiko hayo yanahusu mambo mengi, lakini kwa kutaja baadhi ni kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi au kwa lugha nyingine uwezo mdogo wa kiuchumi.

Kwamba wanahitaji fedha za kutosha kwa ajili ya kuendesha kampeni ndani ya vyama vyao wakati wa mchakato wa uteuzi kupitia kura za maoni na baada ya hapo gharama nzima za kugombea na kushindana na wagombea wa vyama vingine.

Gharama hizo zinahusisha usafiri kutoka eneo moja kwenda lingine, kukodi vifaa kama vipaza sauti, viti,
Lugha za matusi na udhalilishaji majukwani zinalalamikiwa kuwa kikwazo kwa makundi hayo hususan kundi la wanawake ambao wanalalamika kuwa wanapokwenda katika mkutano ya kampeni wanaulizwa maswali ya kudhalilishwa yasiyohusiana na uchaguzi yakiwamo kuulizwa kama mhusika ameolewa.

Wengine wanakwenda mbali zaidi wakidai kuwa wakati mwingine wanatukanwa kwa kuitwa majina mengi ambayo hayana uhusiano kabisa na uchaguzi.

Makundi hayo kadhalika yanalalamikia kutopata nafasi ya kuvitumia vyombo vya habari kwa ajili ya kujitangaza na kuwaeleza wapigakura mipango yao, mikakati na ahadi wanazokusudia kuzitekeleza watakapochaguliwa. Wanavilalamikia vyombo kadhaa vya habari kwa kutowapa fursa hiyo, badala yake kuandika na kutangaza habari za wagombea wenye uwezo wa kiuchumi na wanaogombea kupitia vyama vikubwa vya siasa.

Wagombea wanawake vilevile wanalalamikia mfumo dume ndani ya vyama kwamba vyama haviwaamini kama wanaweza kuteuliwa wakagombea na kushinda na kwamba mtazamo huo umekuwa kikwazo kwa wanawake na matokeo yake ni kuendelea kuwapo na idadi ndogo ya wanawake katika nafasi za uongozi wa kuchaguliwa.

Kwa ujumla, makundi hayo matatu yanalalamikia mambo yanayofanana, isipokuwa kundi la wenye ulemavu linabainisha pia kwamba linakwamishwa na kutowekewa miundombinu rafiki wakati wa uchaguzi ikiwamo watu wenye ulemavu kushindwa kupigakura.

Nimeamua kuandika mada hii kuhusiana na suala hili, baada ya kuhudhuria warsha iliyowajumuisha wadau na wagombea kutoka makundi hayo kujadili changamoto kadhaa waliyokutana nazo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kimsingi, ninakubaliana na mambo mengi waliyoyabainisha kwamba yaliwakwamisha aidha wasiteuliwe na vyama vyao au kugombea na kushindwa kwenye uchaguzi huo.

Ninakubaliana na suala zima la bajeti kwamba ni muhimu kwa mgombea kwa kuwa bila fedha za kutosha siyo rahisi kujiandaa vizuri kupambana. Jambo la msingi ni kwa mgombe mwenyewe kuanza maandalizi mapema kuomba ufadhili kwa marafiki, jamaa na taasisi zinazosaidia makundi maalum.

Kitu muhimu kukijua ni kuwa maandalizi ya huanza mapema kwa mfano, kama kuna mtu anataka kugombea mwaka 2020, wakati wake wa kuanza maandalizi ni sasa kwa kuanza kukusanya kidogo kidogo ili wakati mwafaka ukifika itakuwa rahisi kuwa na uwezo wa kugharimia mambo kadhaa.

Hata hivyo, sikubaliani na madai kuwa vyombo va habari havitoi fursa za wagombea kutoka vyama vidogo, makundi maalum wala wagombea wasio na uwezo wa kiuchumi. Uzoefu katika chaguzi zilizopita umeonyesha kuwa wagombea wengi kutoka vyama vidogo na makundi maalum wanashindwa kujitokeza na kuvitumia vyombo hivyo kujieleza.

Kwa mfano, katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, vyombo vya habari vilikuwa vinachapisha na kutangaza habari nyingi za wagombea kutoka vyama vikubwa vya CCM, Chadema, CUF na ACT-Wazalendo kwa sababu wagombea wake walikuwa wanaweka wazi ratiba zao za kampeni pamoja na maeneo ya kufanyia mikutano hiyo. Kadhalika, walikuwa wanakwenda moja kwa moja katika vyumba vya habari vya vyombo hivyo na kufanyiwa mahojiano, hivyo habari zao kuchapishwa au kutangazwa mara kwa mara.

Hiyo inapaswa kuwa changamoto kwao kwamba kuanzia saa wajenge utamaduni wa kuwa karibu na vyombo vya habari na kuanza kuvitumia kuanzia sasa kwa kuwa uchaguzi ujao hauko mbali. Aidha, asasi za mbalimbali zinazopigania haki za wanawake kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) na Ulingo kwa kutaja baadhi vinawajibu wa kuwasaidia wagombea wa makundi maalum kwa kuendelea kuwapatia mafunzo ya kuvitumia vyombo vya habari kwa ajili ya uchaguzi ujao.

Njia pekee ya kukabiliana na lugha za matusi na kudhalilishwa majukwaani dhidi ya wanawake, ni mhusika kujiandaa mapema kwa kuwa na majibu dhidi ya maswali atakayoulizwa majukwaani. Mgombea aliyejiandaa na kujiamini atakuwa na majibu ya kuwajibu wanaouliza maswali yasiyo na tija au matusi.

Wagombea wa makundi maalum wanapaswa kuelewa kuwa lugha za matusi, kashfa, kejeli na kuzomea ni sehemu ya changamoto katika uchaguzi, hivyo, yote haya yanamtaka mgombea ajiandae kukutana nayo, lakini jambo la msingi ni kujiamini na kutoyajali.

Kwa muda mrefukinamama wamekuwa wakilalamikia mfumo dume kuwa ni kikwazo kwao hata hivyo, suluhisho lake ni kupambana.

Wako kina mama wengi walipambana na hata kufanikiwa kushinda nafasi za kugombea za ubunge na udiwani katika majimbo na kata. Iko orodha ndefu, lakini kwa kutaja baadhi wamo wabunge kama Halima Mdee, Esther Bulaya, Jenister Mhagama, Ester Matiko, Bonnah Kaluwa, Magdalena Sakaya na Susan Kiwanga kwa kutaja wachache.

Kwa wagombea wa kundi la wenye ulemavu iko haja kwa vyama vyao kuwatambua na kuwawezesha kwa bajeti, vifaa na kuhakikisha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi inawawekea miundombinu rafiki ili washiriki katika uchaguzi huo bila vikwazo.

Nimalizie kwa kusema kuwa pamoja na nia ya kuyaongezea makundi maalum hususan wanawake fursa zaidi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi, kama ilivyo kwa wanaume, lengo hilo litatimia ikiwa watajiandaa mapema kwa ajili ya kupambana. Kulalamika hakutawasaidia ila kuzifanyia kazi changamoto walizokutana nazo katika uchaguzi uliopita ndiko kutakaowafanya wafanye vizuri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.