Malezi mema kwanza, si kudekeza watoto

26Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Malezi mema kwanza, si kudekeza watoto

BAADHI ya wazazi na walezi wamekuwa wakichangia kukosekana kwa maadili ya watoto wao kwa kushindwa kuwasimamia na kuwaacha huru huku wakiwadekeza wakifanya wapendalo.

Watoto wapo huru kufanya kile wanachokiona kama ni kutembea usiku, kwenda disko, vibanda umiza na hata ngoma za 'vigodoro' huku wazazi au walezi wakiwaachia hata kama umri hauruhusu.

Suala la maadili ni jambo nyeti ambalo linatakiwa kuzingatiwa na wote, lakini hatua ya kwanza ni kwenye makuzi ya mtoto nyumbani kwenye familia, wazazi na walezi.

Kuna msemo ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.’ Kwamba ukimkuza katika mienendo mema hawezi kubadilika kwa kuwa tayari umemjengea msingi bora tangu alivyokuwa mdogo.

Imenilazimu kuzungumzia jambo hili kwa kuwa wapo baadhi ya wazazi na walezi hawajali maadili kwa watoto inayozalisha kizazi kisicho na maadili.

Malezi ya aina hiyo, huwaingiza watoto kwenye vitendo viovu katika umri mdogo kwa kuwa wapo huru kufanya wapendavyo.

Nia si kumtafuta mchawi kwani suala la malezi ni jukumu la wote, hivyo kila mmoja awajibike kumkuza mtoto katika malezi bora na yanayokubalika. Ni muhimu kwa wazazi na walezi kutambua makosa wanayoyafanya katika malezi na kujirekebisha.

Cha muhimu ni kumfundisha kuelewa kuwa maisha yanabadilika, awe na maadili, heshima na kumjua Mungu na kumheshimu. Afahamu uaminifu, heshima na kusema ukweli.

Mtoto afahamu kuwa kuna wakati unaweza kuwa nacho na siku nyingine huna hivyo ni vyema, ajue kukabiliana na hali zote iwe kupata au kukosa kuliko kumtimizia kila anachohitaji hata kama hauna uwezo wakati huo.

Aidha, kumsifia mtoto kwa kila jambo bila kumpinga ni hatari kwa malezi kwa vile watoto wana tabia ya kukariri mambo hivyo mzazi au mlezi wawe makini kuwakosoa si tu kuwasifia au kuwaunga mkono kwa kila wanalofanya.

Pia kutokutoa ushirikiano unapopata taarifa mbaya kumhusu mtoto ni kosa linalofanywa na wazazi au walezi hasa zinapohusu matendo mabaya, wengi wanawatetea hata kama kuna ushahidi.

Hali hii husababisha watoto wengi kuendeleza mienendo mibovu, kama udokozi, wizi na utukutu. Hivyo ni muhimu kwa wazazi kutoa ushirikiano wanapokea habari za mienendo mibaya ya watoto wao.

Kutumia lugha chafu wakati wa mazungumzo ni kosa linalofanywa na wazazi au walezi wanapozungumza wao kwa wao au wanapoongea na mtoto.

Si vizuri kuongea matusi au maneno yasiyofaa mbele ya mtoto kwani hukariri lugha au maneno kama hayo na kuyatumia pia katika mazungumzo yao.

Kuandaa mazingira yasiyomjenga mtoto kukua katika malezi bora. Katika kujadili suala la malezi pia mwanasaikolojia Duee Wilson anasema: "Mtoto anaweza kuchukua tabia nzuri au mbaya hata kabla hajazaliwa, kwa mfano kuwa na tabia za chuki kutokana na baba na mama kutokuelewana.”

Aina ya malezi mzazi au mlezi anayomjengea mtoto, kama tabia zisizofaa hutegemea na mazingira, wanaowazunguka, muda wanaotumia katika maisha ya kila siku.

Lakini tabia zinaweza kusababishwa na aina nne za malezi mojawapo ni malezi ambayo mtoto na wazazi au walezi wanakua na mahusiano chanya.

Uhusiano kati ya mzazi na mtoto unakuwa mbaya mfano ukali na adhabu kali apewazo, utii unapewa kipaumbele zaidi, sheria zinazowekwa na wazazi au walezi zinakuwa hazitolewi maelezo, lakini mtoto hasikilizwi. Hivyo ni vyema kuweka mizani na kuhakikisha mtoto ananyooka.