Malezi mtoto kila kukicha, dawa inayomfikisha salama

24Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Malezi mtoto kila kukicha, dawa inayomfikisha salama

MALEZI mara zote ni suala nyeti sana, hasa kwa malezi ya watoto wanaoanza kukua na hii ni pale tu mtoto anapoingia kwenye rika ya ukuaji, jambo linalomfanya kijana na hasa binti apate malezi sahihi, pia mvulana, inagawaje kwa watoto wa kike unahitaji unyeti wa kutosha.

Nitapenda kutambua na kutumia nafasi ya wazazi,walezi na jamii kwa ujumla, kuwapongeza kwa malezi bora wanayowapa watoto wa kike na wa kiume wakiwajenga kwenye maadili mema 

Lakini, pamoja na kwamba wazazi wanapambana kumlinda na kumkumbusha mtoto maadili mema, bado ulinzi kwa watoto wa kike unahitaji kutiliwa mkazo wa kutosha.

Hii si nyumbani pekee, hata anapotoka  nyumbani kuelekea shuleni na mitaani jama vile sokoni au anapoaga kuelekea kwa marafiki zake.

Nazungumza hili, kwa sababu watoto wengi wanapotoka nyumbani hawana uangalizi mkubwa. Ni hali ambayo inachangia wengi kutokufikia maeneo sahihi waliotakiwa na badala yake wanaishia kusimamishwa mitaani.

Hiyo ni hasa vichochoroni wakiwa na marafiki zao,vijana wengine wa mtaani na hata watu wazima. Vyote vinaangukia hatari kwa usalama wao .

Hilo limejitokeza katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na hata mikoani na ninaweza kusema kwamba, huenda ni kutokana na ‘ubize’ wanaokuwa nao wazazi katika majukumu yao, kiasi kutoka nje ya wanayopaswa.

Niseme hapo mahsusi ni kwa mazingira ambayo watoto wanatembelea, hali ambayo hawaelewi ni nini wanachofanya na wanakutana na kina nani.

Hali hiyo inaweza kuwa ya kawaida, lakini upande wa pili kuna hatari sana kwa watoto wa kike, kwani wasipoangaliwa kwa umakini stahiki, wanaweza kujikita kwenye tabia hasi kama vile kutofika shuleni.

Mengine ni kuacha kabisa shule, kuanzishaa uhusiano mapema na vijana wanaosimama nao vichochoroni, hali inayoangukia moja kwa moja hatari ya kutofikia malengo stahiki kwa mabinti wasichana hao.

Kwa mantiki hiyo, ni wito wangu na ushauri kwa wazazi na walezi kutilia mkazo suala la uangalizi kwa watoto hao punde tu anapotoka nyumbani kuelekea shuleni na maeneo mengine yanayomfanya akutane na jamii, ikiwa ni pamoja na kufatilia mienendo ya watoto hao wawaoo shuleni na hata wao mtaani.

Pia, ni vyema wazazi wakakemea mara moja wanapogundua mtoto anapokuwa marafiki wasio sahihi iwe ni wa rika lake au vinginevyo, itasaidia sana kutokomeza tabia inayomfanya asitimize ndoto zao.

Hapo ndipo rai yangi ni kwamba, jamii isimame kidete kuwalinda wasichana hao kwani siku zote malezi hujumuisha jamii, ikizingatiwa falsagfa ya "mtoto wa mwenzio ni wako.

Ni muhimu pale kila mmoja atakapohisi uchungu kumuona binti katika mazingira hatarishi.
 
Jambo hilo la kuingia kati mwenendo wake, ni msaada wa kumkumbusha mtoto huyo maadili na mwenendo anayoelezwa kila siku na wazazi wake ,walimu  na hata watu wazima kwenye jamii yake, ambayo kwa ujumla inamrejesha kuimarika kijamii.