Mamalishe na babalishe uvaaji kofia muhimu katika biashara

26Feb 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mamalishe na babalishe uvaaji kofia muhimu katika biashara

MAMALISHE na babalishe wamejipatia umaarufu katika biashara yao, kutokana na kuuza chakula kwa bei ya chini inayoendana na uwezo wa kiuchumi wa wateja wao wa kutomudu kununua chakula cha bei ya juu.

Ni biashara iIiyoshamiri katika maeneo mengi nchini na hasa mijini. Imekuwa ni ajira inayowafanya wajikimu kimaisha, ikiwamo kulisha familia na kusomesha watoto wao.

Hata hivyo, kuna kosa ambalo baadhi yao wanalifanya, ambalo ni vyema mamlaka husika zikalitafutia ufumbuzi wa kudumu ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa ufanisi zaidi bila athari zozote za kiafya kwa wateja.

Ni suala la baadhi ya mamalishe na babalishe kutovaa kofia, hali inayoweza kusababisha nywele kudondokea katika vyakula na kuleta madhara kiafya kwa wateja.

Kwa kuwa ni muhimu katika uandaaji vyakula, pia ni vyema wahusika wakaelimishwa umuhimu wa kuvaa kofia, hata vitambaa maalum vifuani viitwavyo 'apron'.

Nakumbuka, yapo baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, ikiwamo Mikocheni na Viwandani, mamlaka husika hasa manispaa, ziliwahi kugawa kofia kwa mamalishe, lakini kwa sasa hawavai.

Haijulikani ni kwa nini? Sijui zimechakaa, au ni uzembe tu na kama zimechakaa, kwa nini wasishone mpya ama kuvaa hata vitambaa ili kulinda afya za wateja wao?

Kama hawajui umuhimu wa kuvaa kofia wanapokuwa katika biashara hizo, tena wateja wengi ni wa kipato cha kawaida, basi ni wajibu kwa mamlaka husika kuwapa elimu.

Kuvaa kofia si kwa afya za wateja tu, bali wanajilinda hata wenyewe. Hivyo, kuwapa elimu za kuzivaa ni jambo muhimu na linaweza kuwasaidia kuboresha biashara zao.

Binafsi huwa nimaamini, hilo liko ndani ya uwezo wao. Niseme, kuna tatizo lingine linalowakabili la ukosefu wa maeneo ya kufanya biashara, hali inayosababisha 'wavamie' hata pasikoruhusiwa.

Kukosa maeneo rasmi ya kufanya biashara, inasababisha waingie katika orodha ya wanaochafua mazingira, kwa kuwa wanakosa mahali pa kutunza taka wanazozalisha katika biashara zao.

Sasa kuna utamaduni fulani unaojengeka kimyakimya, unamkuta mamalishe na babalishe wakimwaga maji waliooshea vyombo vyao na makombo ya vyakula katika mitaro au eneo lolote la wazi.

Wanafanya hivyo, kwa kuwa hawana sehemu ya kutunzia takataka, hawako katika maeneo rasmi ambayo yangekuwa na huduma zote za muhimu kwao na hata kwa wateja wao.

Pia katika mazingira hayo ya ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara, wanajikuta mvua na jua vyao, kutokana na kwamba hawawezi kujenga vibanda vya kudumu, katika maeneo ambayo si rasmi kwa biashara.

Hivyo, njia mojawapo ya kuwasaidia, ni mamlaka husika kuwatengea maeneo rasmi ili wafanye biashara yao katika mazingira safi, huku pia wakizingatia usafi ikiwamo kuvaa kofia.

Ninaamini, Watanzania wengi wanapenda kula kwa mamalishe na babalishe, kutokana na ukweli kwamba, wanauza vyakula vyao kwa bei ambayo inalingana na uwezo wao wa kiuchumi.

Kukiuka kanuni hizo za afya na mazingira, inabebesha maana kwamba, iwapo wataboreshewa mazingira ya biashara, lakini wakaendelea kutozingatia usafi ikiwamo kutovaa kofia na kutupa takataka ovyo, basi hilo litakuwa ambalo ikibidi zichukuliwe hatua za kisheria.

Hili la sasa kina mamalishe na babalishe katika kusaka riziki, wanashughulika pasipokuwapo choo wala maji, sasa wao na wateja wanajisitiri wapi? Wanajua wenyewe!

Tunafahamu, ili wawe na huduma, sharti kuwatengea mahali penye wateja wengi, kwani upande wa pili ni hao ni wale wapigakura wa mkuu wetu Rais John Magufuli, aliyotamka juzi pale siku ya mwisho kabla ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ‘kutumbuliwa’ na kwa lugha ya kijeshi Manispaa ya Ilala ‘imekaba lofu’ nafasi yake, muda mfupi baada ya kupata mtoto.

‘Stendi ya Kimataifa ya Mbezi Luisi.’

Ni vyema kila halmashauri zote nchini, zikaangalia uwezekano wa kuwasaidia wafanyabiashara hao ili waboreshe huduma zao, badala ya kuendelea kuzifanyia katika mazingira yasiyofaa.
Asanteni.