Mambo haya yarekebishwe kufikia Uchumi wa Viwanda

02May 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mambo haya yarekebishwe kufikia Uchumi wa Viwanda

Tangu kuingia madarakani kwa Rais Dk. John Magufuli, msisitizo umekuwa uanzishaji, ufufuaji na uendelezaji wa viwanda nchini.

 

Tangu kuingia madarakani kwa Rais Dk. John Magufuli, msisitizo umekuwa uanzishaji, ufufuaji na uendelezaji wa viwanda nchini.

 

Ripoti ya Hali ya Ufanyaji Biashara (Doing Business Report 2018) inayotolewa na Benki ya Dunia kila mwaka, inaonyesha Tanzania inakabiliwa na vikwazo vinne katika kuboresha mazingira ya biashara, ambavyo inavitaja kuwa ni: Vikwazo vya kiserikali,  utitiri wa kodi na vikwazo mpakani.

 

Eneo la kodi linalolamikiwa na wawekezaji wengi ni kilio cha muda mrefu cha, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), ambayo tangu serikali iliyopita, walilia kodi kuwa kikwazo kikubwa na kuiomba serikali kuunganisha baadhi ya mifumo na taasisi zake, kuepusha usumbufu na kodi nyingi.

 

Mara kadhaa, kilio hicho kimetolewa na wawekezaji wanaofika wakinuia kuwekeza, kwamba kodi zimekuwa nyingi na siyo rafiki, jambo linalotajwa kinawakwaza wawekezaji wengi.

 

Katika kudhihirisha kwamba bado ni tatizo kubwa linalowaathiri walio serikalini na sekta binafsi, hivi karibuni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kililalamikia maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufunga biashara za wawekezaji.

 

Mkurugenzi wa TIC, Geoffrey Mwambe, alinukuliwa akisema kitendo cha kuwafungia wafanyabiashara na viwanda sababu ya kodi au vibali vingine, kinafifisha hamasa ya uwekezaji nchini.

 

Anashauri hatua ya kufunga biashara au viwanda, ingekuwa ya mwisho badala ya inavyofanyika sasa.

 

Kilio hicho siyo cha bure. Maana yake ni kwamba, kuna jambo kubwa lenye madhara makubwa kwa wawekezaji na taifa kwa ujumla, kwa kuwa wawekezaji watashindwa kufanya biashara. Maana yake ni kwamba, watu watakosa ajira na hawatachangia pato la taifa.

 

TIC na TRA ni asasi za serikali. Hivyo, inapofikia hatua zikalalamikiana hadharani, maana yake kuna kitu hakijakaa sawa, kwa kuwa kilichotarajiwa watoto wa baba mmoja kuyazungumza ya ndani ya familia na kuyamaliza kimya kimya.

 

Inapofikia Mkurugenzi wa TIC, anakwenda mbele ya vyombo vya habari ‘kulia’ dhidi ya ndugu yake TRA, maana yake kunahitajika mamlaka zinazowasiomamia, kusaidia kuweka mambo sawa katika familia hiyo.

 

Tanzania inajitangaza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, lakini kilio cha kodi kimekuwa cha wote na kila wanapopata nafasi huimba serikali, kuliangalia hilo kwa jicho la kipekee.

 

Yapo maboresho yameshafanyika, ikiwamo kuondoa riba kwa wafanyabiashara waliokuwa na madeni makubwa ya kodi, walitakiwa kulipa kodi kamili kwa muda uliotengwa na TRA.

 

Ni vyema TIC na TRA wakafanya kazi kwa kushirikiana, kuhakikisha vikwazo vyote vya wawekezaji kuwekeza nchini, katika sekta mbalimbali vinaondolewa.

 

Katika miaka ya 1990, serikali ilibinafsisha mashirika mengi ya umma yanayomilikiwa na serikali na wawekezaji mbalimbali wa nje na ndani, walimilikishwa kwa asilimia 100 na wengineo hisa mbalimbali kuanzia wastani wa asilimia 51 na zaidi.

 

Viwanda vingi vilikufa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ongezeko la kodi, ulafi na wawekezaji kuvitumia kujinufaisha kutokana na udhaifu wa usimamizi uliokuwepo.

 

Kiwanda kimojawapo kilichomilikiwa kwa hisa nyingi na serikali, ni cha kutengeneza matairi mkoani Arusha au maarufu General Tyre, ambacho Serikali ilimiliki hisa asilimia 74 na mwekezaji asilimia 26.

 

Kiwanda kilikufa kwa sababu nyingi, mwekezaji kuwa na nguvu katika ‘mazingira tata’ kuliko mwenye hisa nyingi na hata kufa kwake, mazingira yake hayakuwa wazi kwa wengi wetu.

 

Upo umuhimu mkubwa, kwa TIC na TRA kukutana na kujadiliana kwa kina changamoto za kodi kwa wawekezaji ili kuhakikisha malalamiko ya wawekezaji yanasikilizwa na kufanyiwa kazi.

 

Tanzania ya viwanda itawezekana, ikiwa pande zote mbili zitakutana na kujadili changamoto zilizopo, ili kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji ambao wataitangaza vyema nchi.