Mamlaka za miji zichukue somo la usafi Stendi ya Mizengo Pinda

30Apr 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mamlaka za miji zichukue somo la usafi Stendi ya Mizengo Pinda

KUNA faida nyingi za usafi kwa mtu binafsi, kijiji, mji, jiji, taifa na dunia kwa ujumla wake.

 

 

 

Afya ni moja ya faida hizo, kitu chenye thamani kubwa kwa maisha ya binadamu kwa sababu afya zetu zinapokuwa timamu ndiyo mtaji mkuu katika dhima nzima ya kujenga ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla wake.

Lakini suala la usafi haliishii kwa binadamu tu, bali hata kwenye mazingira anayoishi.

Kwa mfano mazingira yenye taka ambazo hazizolewi, zilizolalala barabarani au katika mapipa ya taka yasiyofunikwa ni chanzo cha kuzalisha vimelea na wadudu na hivyo magonjwa ya kila aina yakiwamo ya kuambukiza kama vile kipindupindu.

Moja ya vitu vilivyo ndani ya uwezo wetu ambavyo tunaweza kuvifanya kwa uhakika na vikawezekana kwa maana ya kutohitaji msaada kutoka nje ni cha kuweka maeneo yetu, makazi yetu, miji yetu katika hali ya usafi.

Muungwana anasema hili linawezekana baada ya kuwa ametembelea Stendi Kuu ya Mizengo Pinda iliyoko mjini Mpanda, katika mkoa wa Katavi.

Ilikuwa Machi mwaka huu wakati alipoenda kusalimia ndugu na jamaa katika maeneo hayo.

Muungwana alifika Stendi Kuu ya Mizengo Pinda akitokea Stendi ya Treni ya Mpanda kwa usafiri wa Bodaboda, ikiwa ndiyo mara yake ya kwanza kufika katika mji huo.

Wakati aliposhushwa na bodaboda kwenye lango kuu la kuingilia stendi hiyo, alitahadharishwa na dereva wa usafiri huo kwamba kama ni mara yake ya kwanza kufika katika stendi hiyo, basi achukue tahadhari.

Achukue tahadhari ya kutotupa uchafu wowote ule uwe ni wa maganda ya pipi, matunda, chupa za maji au mwingine, zaidi ya kwenye mapipa ya taka yaliyoko sehemu mbalimbali ndani ya stendi hiyo.

Aidha, akaelezwa kwamba stendi hiyo ina njia zilizo maalumu kwa ajili ya watu kupita na pia ina sehemu zilizopandwa nyasi na maua kwa ajili ya kutunza mandhari, hivyo apite kwenye njia zilizoruhusiwa.

Kwamba akikatisha kwingine zaidi ya kwenye njia hizo kama ilivyo ‘ada’ kwa Watanzania wa maeneo mbalimbali nchini ambao hupita hata katika njia au maeneo yasiyoruhusiwa, basi atakamatwa na kukabiliwa na mkono wa sheria ikiwamo faini ya Sh. 50,000.

Baada ya kuingia ndani ya stendi, mandhari ya kuvutia na usafi ulivyo ulimfanya Muungwana aamini alichoambiwa na dereva wa bodaboda.

Karibu abiria wote na wananchi wanaoitumia stendi hiyo wakiwamo wafanyabiashara wa matunda na wenye biashara zingine kama za maduka, na za ‘kimachinga’ walionekana kuwa wastaraabu wakizingatia kanuni zote za usafi zilizoelekezwa.

Aidha, Muungwana alishuhudia askari walioajiriwa kusimamia sheria na kanuni za usafi ndani ya stendi hiyo, wakiwa kazini karibu katika kila eneo la stendi hiyo wakiwa macho kuhakikisha hakuna mtu asiyekiuka sheria na kanuni za usafi za stendi hiyo.

Alipata pia fursa ya kutumia huduma ya vyoo vilivyoko katika stendi hiyo ambavyo ni visafi kutokana na wanaoviendesha kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Mpaka anaondoka katika stendi hiyo majira ya saa sita mchana kutokea saa kumi na mbili asubuhi kuelekea kwa ndugu na jamaa zake, bado hali ya usafi ilikuwa ya juu na mazingira yake yakiwa ya kuvutia.

Hali hiyo iliacha swali la kujiuliza kwa Muungwana kwamba kwa nini Stendi ya Mizengo Pinda imeweza, wakati stendi zilizo nyingi nchini zinashindwa?

Ni rai basi ya Muungwana kwa stendi zilizoko katika miji na majiji mengine hasa jiji la Dar es Salaam, wakaitembelea stendi hiyo inayoendeshwa na Manispaa ya Mpanda kujifunza mafanikio yake.

Ninasema hivyo nikiwa ninajua hali ilivyo katika Stendi Kuu ya Ubungo, na zingine kama zile za Mawasiliano, Makumbusho, Kariakoo, Mbagala, Mbezi Mwisho…kwa kuwa ni mkazi wa jiji hili.